Mkuu wa
Mkoa wa Tanga, Martine Shigella, akiongea jambo mara baada ya kutembelea eneo
la Chongoleani Mkoani Tanga, itakapojengwa Gati itakayotumika kupakua mafuta
ghafi kutoka Hoima nchini Uganda.
Mkuu wa
Mkoa wa Tanga , Martine Shigella ( Wa tano kutoka kulia), katika picha ya
pamoja na Wawakilishi kutoka Wizara ya Nishati na
Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Bandari Tanga
. Pia yupo Meya wa Jiji la Tanga Mustapha Selebosi na Mkurugenzi wa Jiji la Tanga,Daudi Mayeji
Mkurugenzi
wa Sheria, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Ibrahim Ngabo,
akizungumza na waandishi wa Habari wakati Mkuu wa Mkoa wa Tanga alipotembelea
eneo la Chongoleani itakapojengwa gati itakayotumika kupakua mafuta ghafi.
Kaimu
Meneja wa Bandari ya Tanga, Henry Arika akizungumza jambo katika eneo la
Chongoleani Tanga. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella.
Kapteni Andrew Matillya kutoka Bandari ya Tanga, akieleza jambo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa na ujumbe kutoka Wizara ya Nishati na Madini, TPDC na Bandari Tanga walipotembelea eneo la Chongoleani kuandalia maendeleo ya awali ya utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki.
Pichani ni
maandalizi ya awali ya kuandaa eneo itakapojengwa Gati itakayotumika kupakua
mafuta ghafi ya kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga yakiendelea.
Na
Asteria Muhozya, Tanga
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine
Shigella amesema, tayari Mkoa huo umeanza maandalizi ya awali ya utekelezaji wa
mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), kutoka
Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.
Shigella aliyasema hayo mwanzoni mwa
juma alipotembelea eneo la Chongoleani Tanga itakapojegwa gati ya kushusha
mafuta ili kuona maandalizi yanavyoendelea na kuongeza kuwa, Mkoa huo unaandaa
mazingira ya kutekeleza mradi husika ambapo tayari barabara ya kuelea eneo hilo
imekwishachongwa.
“Tunajenga mazingira ya kutekeleza
mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi, lakini pia tunao wajibu wa kuboresha Bandari
yetu kwa ajili ya utekelezaji huo. Yale tunayoweza kufanya sisi kama Serikali tayari
tunaanza wakati tukisubiri Marais na Mawaziri wa nchi husika kusema ni lini
ujenzi huu utaanza rasmi. Kwetu ni fursa na tunataka maendeleo.”
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa
Bandari ya Tanga, Henry Arika alisema kuwa, katika maandalizi ya mradi huo,
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imetenga jumla ya Shilingi bilioni 9.2
kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya bandari hiyo ili kuwezesha mapokezi ya
vifaa vya mradi husika.
Aliongeza kuwa, mbali na kuboresha
miundombinu, fedha hizo pia zitatumika kuongeza kina cha gati ili kuwezesha Meli
kubwa zitakazobeba vifaa vya ujenzi kuweza kutia nanga kwa urahisi.
“TPA inatarajia kupokea wastani wa
tani 250,000 za shehena za vifaa kupitia Bandari yetu wakati wa maandalizi na
ujenzi wa bomba hilo, hivyo maboresho kwetu ni muhimu sana. Tunajua kazi kubwa
iliyo mbele yetu, tunajipanga na tunajiandaa kuhakikisha kwamba mizigo inapita
kwa ufanisi na usalama,” alisema Arika.
Alifafanua kuwa, ili kuimarisha
usalama na kupanua wigo wa eneo la kuhifadhi mizigo, tayari Mamlaka hiyo
imetenga eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 2,600 litakalotumika kwa shughuli
za kuhifadhia shehena ya mizigo kabla ya kusafirishwa, ikiwemo pia maandalizi ya
ujenzi wa mashine maalum ya ukaguzi (scanner)
kwa ajili ya kukagulia mizigo ili kuimarisha usalama.
Naye, Mkurugenzi wa Sheria kutoka
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Ibrahim Ngabo alisema kuwa,
majadiliano ya mfumo wa Kisheria kuhusu mradi kati ya nchi za Tanzania na
Uganda yamekwishaanza na yanaendelea vizuri.
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa
Nishati anayeshughulikia masuala ya Petroli, Wizara ya Nishati na Madini,
Mwanamani Kidaya, alisema kuwa, amefurahishwa na namna Mkoa huo ulivyoanza
maandalizi ya utekelezaji wa mradi husika na hivyo kuwataka wananchi kuwa
tayari kuupokea mradi huo ikiwemo kutumia fursa zitakazojitokeza kupitia mradi
husika.
Katika ziara ya kutembelea eneo hilo,
Mkuu wa Mkoa alifuatana na Uongozi wa Mkoa akiwemo Meya na Mkurugenzi wa Jiji hilo, Uwakilishi kutoka
Wizara ya Nishati na Madini, TPDC na TPA.
EmoticonEmoticon