HOTUBA YA MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA SIKU YA KILELE CHA SIKUKUU YA WAKULIMA - NANE NANE 2016, UWANJA WA MAONYESHO YA KILIMO WA NGONGO MKOA WA LINDI, TAREHE 8 AGOSTI, 2016

August 10, 2016

 
 
Mhe. Eng. Dkt. Charles Tizeba  (Mb.), Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ;
 
Mhe. Hamad Rashid Mohamed (Mb.), Waziri wa Kilimo, Maliasili na Uvuvi (Zanzibar) ;
 
Mhe. Charles Mwijage (Mb.), Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwezeshaji;
 
Mhe. George Simbachawene (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa;
 
Mhe. Godfrey Zambi, Mkuu wa Mkoa wa Lindi;
 
Mhe. Halima Dendego, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara;
 
Mhe. Jaji, Edward Mwesiumo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa TASO Taifa;
 
Ndugu Hassan Wakasuvi, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika,;
 
Wageni Waalikwa;
 
Mabibi na Mabwana.
 
Habari za Asubuhi,
 
Kwanza kabisa napenda kutoa shukrani zangu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi wote nchini kupitia Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi kwa heshima kubwa mliyonipa kwa kunishirikisha kwenye sherehe hizi za kuhitimisha maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima, Nane Nane Kitaifa.
 
Kama mnavyofahamu maadhimisho haya ni ya kwanza kwangu kushiriki kama Makamu wa Rais wa Awamu ya Tano.  Kwa niaba ya Mhe. Rais John Pombe Joseph Magufuli na  Serikali kwa ujumla natoa  salamu na pongezi za Mhe. Rais  kwa waandaaji kwani bila juhudi zenu mkusanyiko huu usingekuwepo.
 
Natambua kuwa kwa miaka mitatu mfululizo Mkoa wa Lindi umekuwa mwenyeji wa maadhimisho haya ya Nane Nane. Hongereni sana wana Lindi kwa ukarimu wenu kwa wageni na kuweza kumudu kwa ufanisi mkubwa nafasi hii ya uenyeji.
 
Aidha, nitakuwa mchoyo wa fadhila iwapo sitotambua mchango mkubwa wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi pamoja na Bodi ya Wadhamini ya TASO Taifa katika kuandaa na kufanikisha shughuli hii muhimu katika kuendeleza kilimo, uvuvi, ufugaji na ushirika. Niwasihi mchukue changamoto mlizozipata mwaka huu na kuziboresha ili mwaka kesho sherehe zifane zaidi.
 
Nimetaarifiwa kuwa katika sherehe za mwaka huu kuna washiriki ambao wametoa mchango mkubwa katika kufanikisha maonesho haya. Na mimi mwenyewe nimeona mchango na  juhudi  zao katika mabanda kadhaa niliyopata fursa ya kuyatembelea. Hii inatia moyo na naomba wengi zaidi mjitokeze mwakani.
 
Kwa namna ya pekee napenda kutambua uwepo wa wananchi wote  mliojitokeza kwa wingi wenu kutembelea mabanda ya Wakala, Taasisi za Umma na Sekta Binafsi wakiwemo wajasiriamali waliojitolea kuunga mkono na kutambua juhudi hizi za Serikali. Kwa kuwa shughuli ni watu na watu ni nyinyi basi sina shaka kusema shughuli yetu imefana. Asanteni wana Lindi na Mtwara na wananchi wote kwa mapokezi mazuri ambayo nimeyapata kupitia viongozi wa Mkoa .
 
Ndugu Wananchi;
Maadhimisho ya  Nane Nane ya mwaka huu yamekuja na kaulimbiu inayosema, “Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni Nguzo za Maendeleo Vijana Shiriki Kikamilifu – Hapa Kazi Tu”. Kaulimbiu hii inawakumbusha wakulima, wafugaji, wavuvi na wanaushirika  kuwa maendeleo yanajengwa kwa kutumia viwanda vidogo, vya kati na vikubwa na kwa kutumia nguvu kazi ya vijana kama chanzo cha kuzalisha malighafi katika Sekta hizo.
 
Kama mnavyofahamu sera yetu ya  Serikali ya Awamu ya Tano ni kujikita katika uchumi wa viwanda.  Ndugu Wananchi, viwanda tunavyovikusudia ni vile ambavyo sehemu kubwa ya malighafi yake itatoka ndani hususani kweye Sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi na maliasili nyingine. Tunategemea kuwa viwanda vya aina hii vitatoa fursa ya kujenga mfumo wa uzalishaji ndani ya nchi uliofungamana na kushikamana. Tutahakikisha kuwa viwanda hivi vinazalisha ziada kwa ajili ya masoko ya nje pia. Tukifanikiwa kuzalisha kwa ajili ya soko la ndani na nje tutaweza kuongeza akiba yetu ya fedha za kigeni na kutuwezesha kutekeleza na kuendeleza mipango mingine kwa ajili ya ustawi wa uchumi wetu. Vilevile tunakusudia kuwa viwanda hivi vitazalisha ajira nyingi kwa vijana wetu ili tuweze kufikia asilimia 40 ya ajira zitokanazo na viwanda kama tulivyoahidi.
 
Ili tufanikiwe katika azma yetu hii na viwanda hivi vilete maendeleo tunayoyahitaji, tutaendelea kubana matumizi, hasa matumizi yasiyo ya lazima, kukusanya kodi inayostahiki na kwa wakati, kupambana na rushwa na ufisadi na kutovumilia uvivu na uzembe kwa watendaji wa umma.
 
Lakini ili mapambano haya yaweze kufanikiwa ni jukumu letu sote kuunga  mkono jitahada za Serikali kwa kulipa kodi kwa wakati, kutoa na kudai risiti, kujiepusha na kukemea vitendo vya rushwa na kujikita katika kufanya kazi kwa bidii ili kama taifa tuweze kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020 kama tulivyojiwekea katika Mikakati na Malengo yetu ya Maendeleo.
 
Nafahamu kuwa mna matarajio makubwa na sisi viongozi wa Serikali yenu, hivyo basi, napenda kuwahakikishia kuwa tuna dhamira ya dhati ya kuendelea kuwatumikia na kuwaboreshea huduma zote za kijamii pamoja na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla bila kujali Mikoa mnayotoka, jinsia, dini au itikadi za vyama vyenu.
 
Ndugu Wananchi;
Leo sherehe hizi za nane nane zimetimiza miaka 23 tangu Serikali ilipoamua kwa makusudi kushirikiana na Chama cha Wakulima (TASO) na wadau wengine wa kilimo, uvuvi, ufugaji na wanaushirika kuwa na jukwaa na darasa kwa ajili ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu mpya za kujikwamua kiuchumi kwa njia ya kufundisha wakulima, wavuvi na wafugaji. Maadhimisho haya yasingetimiza miaka hiyo pasipo ushirikiano wenu.
 
Maadhimisho haya ya Nane Nane ni moja katika juhudi za Serikali za kuboresha shughuli za kiuchumi katika Taifa ambapo zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wake wanajihusisha; wameajiriwa au  kujiajiri katika kilimo, mifugo na uvuvi.  Kwa  mantiki hiyo, tutaendelea kuzipa sekta hizi za  kilimo, mifugo na uvuvi kipaumbele stahiki ili zichangie kwa kiasi kikubwa mapato na hatimaye uchumi wa nchi yetu. Hivyo basi niwaombe muendelee kuiunga mkono Serikali katika jitahada zake za kuleta ufanisi katika sekta hizi.
 
Nyote mnafahamu kuwa Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya sekta ya kilimo kila mwaka. Bajeti hii imeendelea kuongezeka kutoka shilingi bilioni 233.3 mwaka 2005/2006 hadi kufikia shilingi bilioni 1,360.3 mwaka 2015/2016. Mbali na kuongeza bajeti ya Wizara hiyo, vilevile Serikali imeweka mikakati na mipango ambayo imerahisisha utendaji. Mipango hii imesaidia kuongezeka kwa  matrekta makubwa na madogo kutoka 7,491 mwaka 2005/2006 hadi 16,478 mwaka 2015/2016  na hivyo kupunguza matumizi ya jembe la mkono kutoka asilimia 70 hadi asilimia 62.
 
Vilevile Serikali imeongeza idadi ya Maafisa Ugani katika kilimo, kutoka 3,379 mwaka 2005/2006 hadi 8,756 mwaka 2015/2016. Pia vituo vya utafiti wa kilimo vimeongezewa rasilimali fedha, watu na vitendea kazi. Kwa upande mwingine Serikali imefanya jitahada mahsusi za kufufua mashamba ya mbegu kwa kuhusisha sekta binafsi, Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa katika kuzalisha mbegu bora za mazao ya chakula.  Aidha, Wakala wa Mbegu za kilimo (ASA) iliongezewa fedha ili kuongeza uzalishaji.  Mkakati huo, umezaa matunda kwa kuongeza uzalishaji wa mbegu bora kutoka tani 10,477.17 mwaka 2005/2006 hadi tani 32,340 mwaka 2015/2016.
 
Vilevile katika kuendeleza kilimo, Serikali ilizindua rasmi Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) tarehe 8 Agosti, 2015. Benki hii ilianzishwa kwa malengo makuu mawili ambayo ni: kusaidia upatikanaji wa utoshelevu wa chakula ambao ni endelevu nchini; na pili kusaidia katika kuleta Mapinduzi ya Kilimo kutoka  kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi wa Taifa na kupunguza umaskini.
 
Benki hii ya Maendeleo ya Kilimo tayari imeanza kutekeleza majukumu yake kwa kuvijengea uwezo vikundi vya wakulima 89 vyenye jumla ya wakulima 21,526 ambapo jumla ya mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.006 imetolewa.  Jitahada hizi za Serikali  zimezaa mabadiliko mengi chanya kama vile kuongezeka kwa tija na uzalishaji katika nyanja mbalimbali ambako kumetokana na kuongezeka kwa teknolojia na matumizi sahihi ya pembejeo ikiwemo mbolea na mbegu bora.
 
Ongezeko la ubunifu wa teknolojia ndiyo msingi wa kuendelea kuwa na sherehe hizi za maonesho ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la kuzisambaza kwa njia mbalimbali na kuzitumia kwa ufanisi zaidi ili kuboresha hali ya maisha ya mtanzania kiafya na kimapato.
 
Ndugu Wananchi;
Japokuwa tumeweza kuongeza uzalishaji bado kumekuwa na changamoto mbalimbali kama vile upatikanaji wa masoko ya uhakika na bei nzuri kwa mazao ya wakulima, wafugaji na wavuvi; na uchache wa maghala ya kuhifadhi mazao ambao hupelekea mazao mengi kuharibika kabla ya kufika sokoni. Mbali na changamoto hizi vilevile kuna changamoto nyingine kama
  1. uhaba wa pembejeo;
  2. migogoro ya wakulima na wafugaji;
  3.  tatizo la masoko;
  4. wakulima  kukopwa mazao yao;
  5.  tozo zisizokuwa za lazima; 
  6. upungufu wa Wataalamu wa Ugani;
  7. upungufu wa maghala, mabwawa, malambo, majosho;
  8. vifaa duni vya wavuvi;
  9. upotevu wa mazao ya uvuvi;
  10. Uvuvi haramu;
  11. uzalishaji duni  wa vifaranga bora vya samaki na uzalishaji mdogo wa chakula bora cha samaki; na
  12. uwekezaji mdogo hususani viwanda vya mazao ya uvuvi, na hasa katika ukanda wetu wa baharí.
 
Kwa kiasi Serikali imeweza kukabiliana au kuondoa kabisa changamoto hizi  kutokana na jitihada za maksudi zinazochukuliwa ili kuhakikisha kuwa maghala ya kisasa yanaendelea kujengwa nchi nzima.
 
Kwa upande wa changamoto ya kupata masoko na kupata bei nzuri ya bidhaa, Serikali inaendelea na maandalizi ya kuanzisha soko la bidhaa pamoja na kuhawamasisha wazalishaji kujiunga kwenye  Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) ili kuweza kunufaika na fursa zinazoweza kupatikana kutoka kwenye vyama hivyo.  Tutaendelea kuboresha na kuendeleza misingi hii ili kuongeza kasi ya kuleta mapinduzi makubwa katika kilimo, mifugo na uvuvi.
 
Ndugu Wananchi;
Mbali na mikakati niliyoitaja hapo awali ambayo mengi imelenga katika sekta ya kilimo cha mazao; Serikali vilevile imekuwa na dhamira ya kudumu  ya kuhakikisha kuwa inaleta mageuzi katika Sekta ndogo ya Mifugo kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Mifugo. Tayari  tumeshachukua hatua za kuainisha changamoto zinazoikabili sekta hii na kuzitengenezea mkakati. Mtakumbuka ya kwamba katika matukio tofauti Serikali imeahidi kutoa kipaumbele kwenye kuendeleza sio tu Sekta ya Kilimo bali pia sekta ya Mifugo na Uvuvi ambayo nayo pia ikiwekewa mkazo inaweza kuwa  na mchango mkubwa zaidi kwenye pato la taifa.
 
Nimepata tarifa kuwa safari yetu ya kuanza kuondoka kwenye uchungaji kwenda kwenye ufugaji imeanza.  Nimeambiwa kuwa, baadhi ya vijiji sasa vinaandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi na hivyo vinatenga maeneo ya kilimo na ya ufugaji. Natoa rai kuwa tuendelee kuhimiza vijiji vyetu kutekeleza mipango hiyo ili wafugaji wapate maeneo ya malisho mbali na mazao ya wakulima. Vilevile tuwahimize kuhusu umuhimu wa matumizi ya  teknolojia ya uhimilishaji kama mlango wa kuingilia kwenye kuboresha kosaafu za mifugo yetu.
 
Ndugu Wananchi;
Natumai mmeshuhudia juhudi za Serikali  za kuongeza idadi ya wagani wa mifugo  kwa kuongeza idadi ya wanachuo wanaodahiliwa kupitia Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kutoka 2,451 mwaka 2014/2015 hadi 2,500 kwa mwaka wa fedha 2015/2016;  kati ya hao 1,034 ni wa Stashahada na 1,466 ni wa Astashahada. Mpaka kufikia mwezi Juni 2016, wanachuo 1,471 wamekwisha hitimu mafunzo yao. Hii imesaidia Serikali kuongeza  idadi ya Wagani wa Mifugo kutoka 8,541 mwaka 2014/2015 hadi 8,600 mwaka 2015/2016 kati ya 17,325 wanaohitajika, hata hvyo kuna upungufu ya Wagani 8,725.
 
Ndugu Wananchi;
Hatua zilizochukuliwa katika kupambana na changamoto katika Sekta ya Kilimo na Uvuvi; ni pamoja na:
 
Mosi, Mhe. Rais aliunda Wizara mpya kwa kuiunganisha iliyokuwa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika pamoja na Wizara ya  Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kuwa Wizara moja ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi akiwa na lengo la kurahisisha ufanyaji kazi na kuongeza tija.
 
Pili, Serikali ilifuta baadhi ya kodi ambazo hazikuwa na tija na manufaa kwa Wavuvi mfano, tumefuta kodi ya zana za uvuvi ili kuwawezesha wavuvi kupata zana bora na za kisasa kwa bei nafuu zaidi.
 
Tatu, tumeimarisha vyuo vya uvuvi kwa kuanzisha wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA).
 
Nne, tumeongeza juhudi za kupambana na uvuvi haramu ili kutunza mazingira, mazalia ya samaki na kuzuia kuvuliwa kwa samaki wadogo.
 
Tano, tumeimarisha maabara ya Taifa ya Samaki iliyopo Nyegezi Mwanza kwa kuweka vifaa vya kisasa na wataalam ili iende na wakati.
 
Sita, tumeongeza msukumo wa kuhimiza ufugaji wa samaki na kuwezesha mabwawa  ya samaki kuongezeka kutoka 21,300 mwaka 2014/2015 hadi 22,545 mwaka 2015/2016.
 
Ili kuhakikisha jitihada hizi zinaleta matokeo chanya, Serikali imeendelea  kuratibu na kusimamia uvunaji na matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi nchini. Japokuwa bado matukio ya Uvuvi haramu yanaenedelea kujitokeza, lakini mikakati hii imesaidia kuongezeka kwa maduhuli  kutoka  sekta ya uvuvi kwa kiwango cha kuridhisha kutoka shilingi bilioni 9.67  mwaka 2005/2006 hadi shilingi bilioni 17 mwaka 2015/2016. Hivyo basi nawaagiza  mkaze kamba kwa kuwa bado tuna kazi kubwa ya kufanya katika sekta hii ili kuongeza tija na mapato ya wavuvi na pato la taifa kwa ujumla. Ili kufanikisha hili naielekeza Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya sensa za uvuvi na kufuatilia ukusanyaji na uchakataji wa takwimu za uvuvi katika maeneo ya maji makubwa na madogo ili tuweze kufahamu mchango halisi wa sekta hii katika pato la Taifa.
 
Katika hatua nyengine nimefarijika kuona kuna hatua zimeanza kuchukuliwa zenye lengo la kuboresha usimamizi wa uvuvi wa bahari kuu. Nina hakika kuwa uvuvi katika bahari kuu ukisimamiwa vizuri utaongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la Taifa.
 
Ndugu Wananchi;
Napenda kumalizia kwa kuwashukuru washiriki wote mliotumia muda wenu na rasilimali kuwepo hapa na kushiriki katika kutoa elimu ya kuongeza uzalishaji, tija na kipato kupitia kilimo, ufugaji, uvuvi na ushirika. Nimeona jinsi Wizara, Taasisi, Wakala za Serikali, Halmashauri za Wilaya na vikundi vya wajasiriamali mlivyojipanga kikamilifu katika kufanikisha sherehe hizi na hata mimi nimeridhika na jitihada zenu wakati nikitembelea katika baadhi ya mabanda yenu. Uwepo wenu ulikuwa muhimu sana katika kukamilisha shughuli za maadhimisho haya.
 
Nawashukuru tena viongozi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kazi kubwa mliyofanya katika kufanikisha sherehe hizi kwa ngazi ya Kitaifa. Nimeambiwa kuwa Sherehe hizo zitaendelea kufanyika hapa kwa miaka mingine miwili hivyo, ni matumaini yangu kuwa maonesho haya yataendelea kuboreshwa kila mwaka ili yaweze kufikia kiwango cha kimataifa.
 
Katika kipindi hicho, ni wajibu wetu kama Serikali kuona kuwa kiwanja hiki kinaendelea kutumika kama darasa la wakulima, wafugaji na wavuvi hata baada ya maonesho haya kuhitimishwa. Napenda kutoa wito kwa uongozi wa Mikoa hii kwa kushirikiana na Wizara za Sekta ya Kilimo, Mifugo na uvuvi kuhakikisha azma ya kukifanya kiwanja hiki kuwa kituo cha mafunzo ya wakulima, wafugaji na wavuvi inatimia. 
 
Nimalizie kwa kuwashukuru wananchi ambao ndio hasa walengwa wa Maadhimisho haya kwa kushiriki kikamilifu na kufanikisha shughuli hii, na ni matumaini ya Serikali kwamba mtazidisha mchango wenu katika uchumi, uhakika wa chakula na katika kuondoa umaskini wa kipato.
 
Nawasihi mtumie fursa hii kikamilifu ili kubadili kilimo, ufugaji na uvuvi kuwa wa kisasa na hatimae tuboreshe maisha yetu na maendeleo ya Taifa letu. Kumbukeni kuwa kila mmoja akitimiza wajibu wake ipasavyo, maendeleo ya viwanda yanawezekana, ajira zitapatikana, uhakika wa chakula na lishe bora utakuwepo, sote kwa pamoja tutasonga mbele, uchumi wetu utaimarika, na Taifa litastawi na kunawirika.
 
Baada ya kusema hayo sasa natangaza rasmi kuwa  Maadhimisho ya 23 ya Sikukuu ya Wakulima - Nane Nane kwa Mwaka 2016, yamefungwa rasmi.
 
Nawashukuruni sana kwa kunisikiliza.  
 

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »