HALMASHAURI YA WILAYA YA LUSHOTO YATISHIA KUWAONDOA WAPANGAJI KWENYE MAJENGO YAO WASIOLIPA KODI KWA WAKATI

August 09, 2016
Kushoto  ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Lushoto,Kazimbaya Makwega Kazimbaya akizungumza na waandishi wa habari
HALMASHAURI  ya Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga imetishia kuwaondoa watu waliopangisha katika nyumba za Serikali na vibanda vya biashara watakaoshindwa kulipa kodi za pango kwa wakati uliopangwa na kuwagaiwa wengine wenye uwezo wa kufanya hivyo ili kuongeza kasi ya ukusanyaji
wa mapato.

Hatua hiyo inatokana na baadhi yao kutokulipa kodi zao kwa muda
ulioweka na hivyo halmashauri hiyo kutoa hadi kufikia Agosti 13 mwaka huu wawe wamekwisha lipa la sivyo watashughulikiwa ikiwemo kuondolewa kwenye nyumba hizo.

Haya yalisemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya
hiyo,Kazimbaya Makwega Kazimbaya ambapo  alisema kuwa Serikali haitakuwa tayari kuona inapoteza mapato yake kwa kuwaachia watu wakikaa kwenye majengo hayo ya serikali kwa kutegemea vyeo au nafasi zao za kifedha bila ya kulipia kodi jambo ambalo katika serikali ya awamu ya tano watu wa namna hiyo hawatakuwa na nafasi.

Alisema kuwa zipo mali za serikali ikiwemo nyumba,vibanda vya biashara na vizimba katika soko kuu ambavyo vinafanyiwa kazi na wafanyabiashara bila ya kulipiwa kodi kwa muda mrefu na kupoteza pato la Halmashauri idara ya biashara itakuwa na wajibu wa upotevu wa pesa hizo.

Makwega alisema kuwa lazima Halmashauri kwa kushirikiana na idara ya biashara itumuie vizuri rasilimali zake na kuzisimamia ili kuhakikisha swala la ukusanyaji wa kodi katika vyanzo hivyo unafanyika kwa wakati na bila ya ubabaishaji.

Alisema katika suala hilo hawataangalia cheo cha mtu awe Mbunge,Diwani ama mfanyakazi yeyote serikalini na halmashauri badala yake wasiokuwa tayari wataondolewa ili kupisha watu watakao kuwa na uwezo wa kulipia kodi ya mapango kwa wakati ili kuchangia ongezeko la mapato.

Aidha alisema zipo tabia zilizojengeka kwa muda mrefu kwa baadhi ya watumishi wa Halmashauri kufanya kazi kwa kulindana na baadhi ya wateja wao kutokana na nafasi zao hali hiyo ndiyo iliyopelekea kupoteza kiasi kikubwa cha pato la Halmashauri.

Mkurugenzi huyo alisema huu si muda wa kulindana tena kila mmoja anapaswa awajibike katika nafasi yake ya kazi kiukamilifu na kuhakikisha Halmashauri inakusanya kodi ya kutosha itakayaokidhi uwezo wa kuboresha shughuli mbalimbali za maendeleo Wilayani humo.

Akitolea mfano mkurugenzi huyo alisema wanahitajika kukusanya kiasi cha shilingi 200 ushuru wa wafanya biashara sokoni na shilingi 800 gharama ya kulipia kizimba jambo kwa siku jambo ambalo halikufanyika kwa miaka mingi na kupoteza pesa nyingi na sasa wafanya biashara wanaowajibu wa kulipia kiashi hicho kama nilivyoelekeza.

Hata hivyo alisema Wilaya imekuwa na rasilimali nyingi ambazo
hazikutumiwa vizuri kwa ajili ya kuwaleta maendeleo wananchi wa maeneo husika huku wananchi wakilalama kutokuwepo kwa baadhi ya huduma na kupelekea kuichukia Serikali yao jambo ambalo  linahitaji kusimamiwa kwa nguvu zote ili rasilimali hizo ziwe na manufaa kwa wananchi wote.

Makwega alisema hatomvumila mtumishi yeyote atakae kwenda kinyume na taratibu za kazi na kutoa onyo kwa watumishi wote sharia kali zitachuliwa kwa yoyote atake bainika ni miongoni mwa wanaokwamisha jitihada za kupambana na jitihada za  kuwapunguzia kero wananchi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »