Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesikitishwa na
taarifa zilizosambaa katika mitandao kuanzia jana zikiwahusisha viongozi
wa timu moja ya daraja la kwanza na baadhi ya watumishi wa TFF.
Pamoja na kwamba taarifa hizo zilizosambazwa hazihusiani na kesi ya
kupanga matokeo iliyoamuliwa siku ya tarehe 03/04/2016, TFF inachunguza
kubaini uhalisia (authenticity) wa taarifa hizo na itachukua hatua kali
sana kwa watumishi wa shirikisho na viongozi wa timu husika
watakaobainika kushiriki vitendo vilivyo kinyume na maadili ya mpira wa
miguu.
TFF imekwishaweka bayana nia ya kupambana na yeyote atakayehusika
katika upangaji matokeo na uhalifu mwingine unaoharibu ustaarabu wa
mpira kwa njia yoyote ile.
Pia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa onyo kwa
baadhi ya viongozi, watumishi wa TFF na wadau wa mpira wa miguu kwa
ujumla wanaotumia majina ya viongozi wa juu wa TFF katika kufanikisha
mipango yao kwa manufaa binafsi.
TFF inawaomba wapenda mpira wa miguu kuwa watulivu na waangalifu wakati suala hili linashughulikiwa.
Aidha, kuhusu hukumu ya Kamati ya Nidhamu ya TFF ni muhimu ikaeleweka
wazi kwamba zipo taratibu za kukata rufaa kwa mujibu wa kanuni ili
upande usioridhika na maamuzi yanayotolewa uweze kuhoji maamuzi husika.
Ni vema tukaacha kamati huru zifanye kazi zake kwa mujibu wa
taratibu. Kutoa hukumu mtaani au kwenye vyombo vya habari kunaweza
kuwanyima haki wanaostahili na kutengeneza kichaka cha kujificha watenda
maovu.
EmoticonEmoticon