Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kiingilio
cha shilingi elfu mbili tu (2,000) kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa
kirafiki wa kimataifa kati ya Serengeti Boys (Tanzania U17) dhidi ya The
Pharaohs (Misri U17).
Mchezo kati ya timu hizo za vijana utachezwa kesho Jumanne saa 10
kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki na Kati, katika uwanja wa Azam
Complex uliopo eneo la Chamazi jijini Dar es salaam.
Katika mchezo wa kirafiki wa awali uliochezwa Jumamosi katika uwanja
wa Taifa jijini Dar es salaam, Serengeti Boys waliibuka na ushindi wa
mabao 2 – 1 dhidi ya The Pharaos, mabao ya Serengeti yakifungwa na
kiungo Cyprian Bennedictor na Ally Hussein.
Kikosi cha Serengeti Boys kinachonolewa na makocha Bakari Shime na
Sebastian Mkomwa wakishauriwa na Kim Paulsen, baada ya mchezo wa awali
kimeendelea na mazoezi katika uwanja wa Karume kujiandaa na mchezo huo
wa kesho.
Mchezo huo wa kirafiki ni sehemu ya maaandalizi kwa timu zote
Tanzania (U17) na Misri (U17) zinazojiandaa na michezo ya kuwania kufuzu
kwa Fainali za Mataifa Afrika kwa Vijana mwaka 2017 zitakazofanyika
nchini Madagascar.
Serengeti Boys itaanza kutupa karata yake dhidi ya Shelisheli Juni
25, 2016 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam na marudiano
kuchezwa baada ya wiki moja nchini Shelisheli.
EmoticonEmoticon