ATLETICO YAI'BEEP' BAYERN 1-0

April 28, 2016
ATLETICO Madrid jana wamepata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Bayern Munich katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya ligi ya Mabingwa barani Ulaya kwenye uwanja wa Vicente Calderon, jijini Madrid.

Bao pekee katika mchezo huo lilifungwa katika dakika 11 na kiungo kinda wa timu ya taifa ya Hispania chini ya miaka 21 (U21), Saul Niguel baada ya kutumia uwezo binafsi na kuwapoteza walinzi wa Bayern.

Katika mchezo huo ambao Bayern walitawala kwa kiasi kikubwa huku wakifanikiwa kulifikia lango la wenyeji mara kwa mara, zilishuhudiwa kadi za njano tano ambapo Atletico walipata moja (Niguez) na Bayern wakizawadiwa nne ambazo zilienda kwa Douglas Costa, Mehdi Benatia, Manuel Neuer na Arturo Vidal.

Kocha wa Bayern, Josep Guardiola alilazimika kufanya mabadiliko matatu akijaribu kupata ushindi au sare kwa kuwatoa Kingsley Coman, Thiago Alcantara na Juan Bernat huku nafasi zao zikichukuliwa na Franck Ribery, Thomas Mueller na Benatia. Kwa upande wa Atletico alitoka Niguez na nafasi yake kuchukuliwa na Thomas.

Kwa ushindi huo, vijana wa Diego Simeone watakwenda Allianz Arena wiki ijayo wakihitaji ushindi wowote au hata sare ili wafaulu kucheza fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu barani Ulaya.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »