Mraghbishi
Kootu Tome (wa pili kushoto) akiwa na mtendaji wa kijiji Rabie Lebuna (mwenye
shati la njano) na Mwenyekiti wa Kijiji, Kerry Dukonya (wa pili toka kulia).
|
Na Kisuma Mapunda,Loliondo
Sasa
ni dhahiri waraghbishi wanatambua majukumu na haki zao ndani ya jamii. Uelewa
wao umewapa fursa ya kuchukua hatua na kusimamia kile wanachoamini kwa manufaa
ya wanajamii wanaowatumikia.
Watu
hawa wamekuwa mhimili muhimu wa kuleta mabadiliko katika maeneo wanayoishi.
Lakini inapendeza zaidi kuona waraghbishi hao wakijawa na dhamira ya dhati ya
kuwatumikia wananchi wao kwa kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi
kama ilivyo kwenye Kijiji cha Ololosokwani, kilichopo katika tarafa ya
Loliondo, wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha.
Kijiji
hiki kina jumla ya kaya 1,520
zinazoundwa na vitongoji vinne vya kijiji, ambavyo ni Sero, Ololosokwani,
Mairowa A na B. Baadhi ya wanaounda kaya hizo ni pamoja na waraghbishi
wanaofanya kazi na mradi wa Chukua Hatua, akiwamo Kootu Tomu, mama wa watoto
sita kutoka kitongoji cha Mairowa.
Tomu
ni mmoja wa waraghbishi wa kwanza kuanza kufanya kazi na mradi wa Chukua Hatua wakiwa na
jukumu la kufuatilia ahadi za wagombea
wakati wa uchaguzi wa mwaka 2010. Ni
katika uraghbishi huu wa kufuatilia ahadi zilizokuwa zinatolewa na wagombea,
ndipo alipojifunza taratibu na kanuni za kuwa kiongozi bora.
Miaka
mitano baadaye, alijitokeza katika kinyang’anyiro cha kuomba kuchaguliwa na
wanachama wenzake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kura ya ndani ya maoni.
Na baada ya hapo alipata fursa ya kupeperusha bendera ya chama chake na
kuchaguliwa katika uchaguzi uliofanyika mwezi Disemba mwaka 2014.
Akielezea jinsi ilivyokuwa Kootu Tomu anasema:
“Nilifahamu
jukumu lililokuwa mbele yangu katika kusimamia haki kwenye migogoro ya ardhi
katika eneo letu. Hivyo, katika uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa niliomba
ridhaa ya kuchaguliwa kuwa mjumbe wa kijiji kupitia CCM na nilichaguliwa. Sasa
naweza kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa akinamama kupitia fursa hii ya
uongozi niliyopata,”
Ndani
ya halmashauri ya serikali ya kijiji cha Ololosokwani, mraghbishi huyu
amechaguliwa kuwa mmoja kati ya wajumbe 9 wanaounda kamati ya elimu. Akiwa kama
mjumbe wa kamati hiyo, anafafanua majukumu yake:
“Moja
ya jukumu la kamati yetu ni kusimamia upatikanaji wa ada kwa wanafunzi. Kijiji
chetu kinapata fedha kutoka idara ya wanyama pori, ambazo ndiyo hutumika
kulipia ada za watoto kwenye kijiji chetu.”
Katika
kijiji cha Ololosokwani, kila mtoto anapata fursa ya kupata elimu kwa kulipiwa
gharama stahiki kuanzia ngazi ya shule ya msingi hadi kiwango cha shahada ya
uzamili.
Serikali
ya kijiji hiki imejiwekea utaratibu wa kuhakikisha walengwa wanapata huduma
husika na kuhakikisha wanatoa taarifa za kweli.
Akifafanua
utaratibu huo, mwenyekiti wa kijiji cha Ololosokwani, Kerry Dukonya anasema:
“Jambo
la kwanza ni mwanafunzi kutafuta shule na baada ya kupata atatakiwa kuleta fomu
na barua ya kukubaliwa kujiunga na shule husika kama kielelezo. Barua hiyo ndio
inayotoa maelezo ya ada na mahitaji mengine ya shule. Ndipo hapo kamati inafuatilia na kuhakiki
taarifa, kabla ya kupitishwa na halmashauri ya serikali ya kijiji.”
Waraghbishi wamekuwa msaada mkubwa
katika kutimiza majukumu ya serikali kwa kuwa mstari wa mbele katika harakati
za kuhimiza wananchi kutambua haki na majukumu yao katika kijiji. Na viongozi
wa kijiji wanakiri kwamba waraghbishi wamekuwa wakishawishi wananchi kuchukua
hatua mbalimbali, ikiwamo kuwawajibisha viongozi wazembe.
Akifafanua
hali hiyo na jinsi viongozi wanavyojisikia iwapo uraghbishi utagusia masilahi
yao hasa linapokuja suala la kuwawajibisha, mwenyekiti wa kijiji anasema:
“Sisi
kama viongozi, tunamruhusu Kootu kwenda popote na akinamama hawa wamekuwa
mstari wa mbele kutukosoa na kutukumbusha majukumu yetu. Hii ni njia mojawapo
ya kuruhusu haki itendeke. Hivyo ni haki ya wananchi kujua mapato na matumizi
ya serikali yao ambayo sisi kama viongozi
tunayasimamia.”
Kama
mwanamke ndani ya halmashauri ya serikali ya kijiji, amepatiwa jukumu maalumu
la kuhakikisha wanawake na wasichana wanashiriki katika shughuli za
maendeleo. Akifafanua jambo hilo,
mwenyekiti wa Ololosokwani, Kerry alisema:
“Tungependa
kuona anakuwa kielelezo cha mwanaharakati mwanamke kutokana na nafasi yake kama
mjumbe wa halmashauri ya serikali ya kijiji. Lakini pia wanawake wamekuwa ni
kundi la pembezoni, ikiwamo walemavu. Mraghbishi huyu atakuwa mstari wa mbele
kuwahamasisha wenzake kutambua umuhimu wa elimu.”
Mraghbishi
Kootu Tome (kushoto) akigawa nakala za Riwaya za Chukua Hatua kwa baadhi wa
wananchi wa kijiji cha Ololosokwani ikiwa kama sehemu yake ya uraghbishi.
(Picha na Kisuma Mapunda)
|
Mraghbishi
Tome, kwa kutumia mbinu za kiuraghbishi, anahakikisha watoto wa kike wanakwenda
shule. Katika hili, anaeleza anaeleza mikakati yake:
“Kama
mraghbishi, nimepata fursa ya kukutana na akinamama na kuhakikisha watoto wa
kike wanapata nafasi za kusoma. Lakini siku zote nimekuwa nikiwataka
kuwasiliana na walimu ili watambue changamoto zinazowakabili watoto wao wa
kike, hasa kwa wale ambao wapo mashuleni tayari,”
Kwa
upande wake, mtendaji wa kijiji Rabia Legula anasema:
“Ninapozungumzia
mraghbishi, namaanisha wale wanaohamasisha wananchi kudai haki zao za msingi,
ikiwamo kuwawajibisha viongozi. Si hivyo tu, waraghbishi wamekuwa mstari wa
mbele kunisaidia masuala yanayohusu wanawake. Kupitia ujuzi wao na kama
wanawake waraghbishi tunatoa kipaumbele kwa wanawake.”
Katika
jamii ya kimasai ambayo bado wanawake hawajapata nafasi ya kutosha, uwepo wa
waraghbishi wanawake umekuwa chachu nzuri ya kuwawezesha wenzao kuongea katika
mikutano ya hadhara.
“Tunapenda
waraghbishi waendelee kuhamasisha akinamama kuongelea masuala yao katika
mikutano ya vijiji. Kwa kutumia nafasi yangu ya utendaji, nitahakikisha natoa
fursa kwa waraghbishi hawa kuzungumza kwa uwazi mambo ya wanawake.”
Kama
mjumbe wa halmashauri ya serikali ya kijiji, mraghbishi amekuwa na jukumu la
kuhakikisha wananchi wanahudhuria
mikutano ya kijiji.
“Huwa
nawahamasisha akinamama wenzangu kuhudhuria mikutano ya kijiji kila
tunapokutana kwenye vikundi vyetu vya ushirikiano,” anasema.
Mkurugenzi Mtendaji wa PALISEP, Roberth Kamakia,akielezea jambo katika mkutano uliokutanisha waraghabishi toka mikoa ya Arusha ,Simiyu na Shinyanga uliofanyika hivi karibuni |
Awamu
ya pili ya mradi wa Chukua Hatua, unalenga kuwawezesha waraghbishi wa zamani
kufundisha waraghbishi wapya waliochaguliwa na serikali za kijiji, kama
anavyoelezea Mkurugenzi Mtendaji wa PALISEP, Roberth Kamakia,
“Tuliwaandikia
barua serikali za vijiji tukiwaomba watuchagulie watu wanaofaa kuwa waraghbishi.
Tuliwapa sifa za watu hao na mwongozo wa jinsi ya kuwachagua.
Baada
ya waraghbishi hao kuchaguliwa, waliandaliwa kwa ajili ya mafunzo ya pamoja
ikijumuisha wale wa zamani na wapya. Na baada ya hapo waraghbishi wa zamani
walikuwa na jukumu la kuwafundisha wenzao jinsi ya kufanya uraghbishi.
Katika
mafunzo hayo, walikumbushwa maana ya uraghbishi na sifa za uraghbishi. Ndipo
wale waraghbishi wa zamani, akiwamo Kootu walipopewa jukumu la kufundisha
wenzao kwa kutumia uzoefu waliopata wa uraghbishi.
Akielezea
jinsi wao waraghbishi wa zamani wanalivyofundisha waraghibishi wapya wanaotoka
vitongoji vya Ololosokwani na Njoroi, Kootu anasema:
“Tulikaa
pamoja PALISEP na kuwafundisha waraghbishi wapya. Kwa upande wangu,
nilifundisha maana ya uraghbishi na kutoa maana ya mtu anayeitwa mraghbishi
Kazi yake ni kuwahamasisha wananchi. Mraghbishi anatakiwa awe na sikio kubwa la
kusikiliza, mdomo mdogo wa kuongelea na macho makubwa ya kuangalia,”
anasema.
Kootu
si mraghbishi pekee aliye kwenye halmashauri ya serikali ya Kijiji cha
Ololosokwani, mraghbishi mwingine ni Noorkishili Naing’isa ni mjumbe wa
halmashauri na kamati ya fedha. Ni
dhahiri waraghbishi wanawake wameendelea kuwa chachu ya maendeleo kutokana na
utendaji wao mzuri kwenye serikali za kijiji. Hivyo ni jukumu letu sote
kuhakikisha harakati hizi za uraghbishi ndani ya halmashauri za vijiji vyetu
zinaungwa mkono.
CHANZO ; MWANAHARAKATI MZALENDO BLOG
EmoticonEmoticon