Serikali yatoa Ufafanuzi juu ya uzushi wa kifo cha Rais wa Awamu ya Tatu

November 04, 2015



 Na Georgina Misama-MAELEZO

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene amekanusha taarifa za uzushi zinazosambazwa kwenye baadhi ya
vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa.


Akiongea katika mkutano na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Bw. Mwambene amesema kuwa Mhe. Rais Mkapa ni mzima na mwenye afya nzuri   anaendelea na shughuli zake kila
siku kama kawaida.


“Mhe. Rais Benjamin William Mkapa ni mzima hajafariki, wala haumwi na si jambo jema kumzushia tukio hilo kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na nawasihi msiendelee kusambaza
ujumbe huo” alisisitiza Mwambene.


Aidha, katika mkutano huo Mwambene aliwashukuru wahariri, waandishi wa vyombo vyote vya habari na mitandao ya kijamii kwa ujumla kwa kuonyesha moyo wa uzalendo katika kipindi
chote ambacho Taifa limekuwa katika mchakato wa uchaguzi na mpaka sasa ambapo serikali inaendelea na maandalizi ya sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Awamu ya Tano, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.


Mwambene amesema mpaka sasa maandalizi ya sherehe hizo yanaendelea vizuri, zaidi ya Marais 15 kutoka nchi mbalimbali wamealikwa baadhi wameshawasili nchini na wengine wanaendelea kuwasili.

Sherehe za kuapishwa Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya Tano zitafanyika kesho tarehe Novemba, 5 mwaka huu katika uwanja wa Uhuru.

chanzo:michuziblog

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »