Habari zote na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
RAMBIRAMBI MSIBA WA
MEJA JENERALI MAKAME RASHID
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa
masikitiko za kifo cha Mkuu wa zamani wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja
Jenerali Makame Rashid kilichotokea juzi (Aprili 14 mwaka huu) kutokana na
maradhi jijini Dar es Salaam.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema msiba huo ni mkubwa
kwa wadau wa mpira wa miguu kutokana na mchango aliotoa Meja Jenerali Makame
Rashid ikiwemo kuwa mlezi wa timu ya Ruvu Stars wakati huo akiwa Kamanda (CO) wa
Kikosi cha Ruvu JKT.
Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la
Taifa (BMT), Mdhamini (Trustee) wa TFF wakati huo ikiitwa Chama cha Mpira wa
Miguu Tanzania (FAT) na wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya katika miaka ya
themanini alikuwa sehemu ya mafanikio kwa timu ya Tukuyu Stars ya Mbeya
iliyotwaa ubingwa wa Tanzania Bara mwaka 1987 ikiwa ndiyo kwanza imepanda
kucheza Ligi Kuu wakati huo ikiitwa Ligi Daraja la Kwanza.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Meja Jenerali
Makame Rashid, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na
Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu
katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Maziko yanatarajiwa kufanyika leo (Aprili 16 mwaka huu)
nyumbani kwao mkoani Mtwara. Mungu aiweke roho ya marehemu Sembwana mahali pema
peponi. Amina
MWISHO
VPL KUTIMUA VUMBI VIWANJA VITATU
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania
Bara inaendelea kesho (Aprili 17 mwaka huu) kwenye viwanja vitatu huku vinara wa
ligi hiyo Yanga wakifukuzia ubingwa huo jijini Tanga.
Yanga inayoongoza ligi ikiwa na pointi 52 itakuwa mgeni
wa Mgambo Shooting katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Athuman Lazi kutoka
Morogoro kwenye Uwanja wa Mkwakwani. Waamuzi wasaidizi wa mechi hiyo ni Michael
Mkongwa wa Iringa na Godfrey Kihwili wa Arusha wakati Kamishna wa mechi hiyo ni
Godbless Kimaro kutoka Moshi.
Kagera Sugar na Toto Africans zitaumana kwenye Uwanja wa
Kaitaba mjini Bukoba katika mechi namba 164 itakayokuwa chini ya mwamuzi Martin
Saanya wa Morogoro.
Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro, na
wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 4,000 utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya
Mtibwa Sugar yenye pointi 33 na Oljoro JKT yenye pointi 28.
Israel Nkongo kutoka Dar es Salaam ndiye atakayechezesha
mechi hiyo akisaidiwa na Hamis Chang’walu (Dar es Salaam) na John Kanyenye
(Mbeya). Kamishna wa mechi hiyo ni Ramadhan Mahano kutoka Iringa.
MWISHO
AS FAR KUWASILI KESHO KUIKABILI AZAM
Wapinzani wa Azam katika michuano ya Kombe la
Shirikisho, AS FAR Rabat ya Morocco wanatarajiwa kutua nchini kesho (Aprili 17
mwaka huu) saa 7 mchana kwa ndege ya Emirates.
Msafara wa timu hiyo wenye watu 28 utafikia hoteli ya
Sapphire iliyoko maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam tayari kwa mechi hiyo ya
kwanza ya raundi ya pili itakayochezwa Jumamosi (Aprili 20 mwaka huu) saa 10
kamili jioni Uwanja wa Taifa.
MWISHO.
EmoticonEmoticon