DR.Mndolwa: Wazazi tutainua kiwango cha Elimu ndani ya Miaka miwili.

April 22, 2013
Na Oscar Assenga, Tanga.

MWENYEKITI wa Jumuiya wa Wazazi Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Dr, Edmund Mndolwa amesema jumuiya hiyo imejiwekea mikakati ya kuinua kiwango cha elimu ndani ya miaka miwili katika shule wazazi mkoani hapa.

Akizungumza jana,Dr. Mndolwa alisema mikakati hiyo ni pamoja na kuhakikisha wanafunzi waliopo kwenye shule hizo kuwa na nidhamu ya hali ya juu kwa walimu wao pindi wawapo shuleni na nje ya shule ikiwemo kuweka wastani ambao endapo mwanafunzi atashindwa kufanya vizuri atarudia mwaka.

Alisema walikwisha kuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha shule hizo haziingiliani na masuala ya kisiasa hivyo kuwataka wanafunzi wanaopata nafasi ya kusoma wasome kwa bidii ili waweze kuwa na misingi mizuri katika jamii zao zinazowazunguka.

Akizungumzia suala la utoro, Dr.Mndolwa alisema wanafunzi ambao watabainika wametoroka shuleni watapewa adhabu kali ikiwemo kuchapwa viboko ili kuweza kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Alisema hawatawafumbia macho walimu ambao watabainika wamewapa ujauzito wanafunzi wao watawachukulia hatua stahiki ikiwemo kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria na kuwafukuza kazi kwani watakuwa hawana msaada katika shule hizo.

  “Suala la upewaji mimba wanafunzi sio nzuri linapaswa kukemewa ipasavyo na mwalimu ambaye atabainika amefanya kitendo hicho hatutamvumilia tutamfukuza pamoja na kumchukulia hatua stahiki dhidi yake “Alisema Dr.Mndolwa.

Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »