African Sports yapunguzwa kasi ya kusaka ubingwa na Small Prison

April 28, 2013
Na Oscar Assenga, Tanga.

BAO 1-0 walilofungwa timu ya African Sports “Wanakimanumanu”na Small Prison ya Tanga limewapunguzia mbio zao za kutaka kuwania ubingwa wa Ligi ya Mkoa wa Tanga kutokana na kuwa na idadi ya pointi sawa wakitofautiana mabao tu na timu hiyo.

Mchezo huo ambao ulianza kwa kasi ambapo kila timu ziliweza kuingia uwanjani hapo zikiwa na ari na nguvu ya kutaka kushinda kwa idadi kubwa ya mabao lakini hali ilikuwa ngumu kidogo kutokana na kuonekana kukamiana.

Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna timu iliyoweza kuona lango la mwenzie ambapo timu zote zilianza awamu ya pili kwa ushindani mkubwa ambapo kipindi hicho, Small Prison waliweza kufanya mabadiliko kwenye dakika ya 65 ambapo walimtoa Gerald Gasper na kuingia Said Mtupa.

Kuingia kwa mchezaji huo kuliweza kuwaongezea nguvu timu hiyo na kuanza kucheza kwa pamoja na kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa African Sports kwa dakika kadhaa na hatimaye kuweza kufanikiwa kuandika bao lao la kwanza na la ushindi kwenye dakika ya 74 kupitia Martin Mpanduzi baada ya kutokea piga ni kupige langoni mwa African Sports.

Baada ya kuingia bao hilo,African Sports waliweza kujipanga na kuanza kuliandama lango la Small Prison huku wachezaji wake wakipiga mashuti makali langoni mwa timu hiyo bila kuweza kwa mafanikio yoyote kutokana na uimara wa mlinda mlango wa timu hiyo,Frank Mutego.

Katika hatua nyengine baada ya mechi hiyo kumalizika wachezaji wa timu ya Small Prison waliweza kumbeba juu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Raphael John wakimpongeza kwa ushindi ambao waliupata.

Kwenye mechi hiyo,African Sports iliwakilishwa na Mohamed Rashid,Abasi Peter,Rashid Hassani,Yusuph Ally,Said Abdallah,Pera Ramadhani,Mohamed Issa,Thabit Mgoha,Akrusus Jacim na Ramadhani Hamid.

Small Prison walikilishwa na Frank Mutego,Lazaro Nyato,John William,Mwaita Salehe,Mohamed Muya,Msafiri  Hassani,David Mwingira,Salim Mashaka,Juma Mohamed,Martin Peter na Gerald Gasper.

Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »