Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MLINDA mlango namba moja wa Simba sc, Ivo Philip Mapunda
amepania kufanya makubwa katika msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara
unaotarajia kuanza kushika kasi Septemba 20 mwaka huu.
Simba chini ya kocha mkuu, Mzambia, Patrick Phiri
akisaidiwa na kiungo wa zamani wa klabu hiyo na timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa
Stars’, Suleiman Abdallah Matola ‘Veron’ itaanza kampeni ya kusaka ubingwa
dhidi ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union, Septemba 21 mwaka huu uwanja wa Taifa
jijini Dar es salaam.
Akizungumza na MPENJA BLOG mchana huu, Ivo amesema
kocha Patrick Phiri ameleta mabadiliko makubwa katika kikosi cha Simba na
wanatarajia kushirikiana naye ili kufikia malengo yao.
Ivo aliongeza kuwa wakati wa utawala wa Mcroatia,
Zdravko Logarusic, wachezaji walikuwa na mipaka ya kucheza mpira na hawakutumia
vipaji vyao kwa uhuru, lakini kwa kocha Phiri mambo ni tofauti kwasababu
wachezaji wanafanya kile wanachoweza na kuonesha vipaji kwa uhuru.
Kipa huyo mkongwe aliyewahi kucheza Yanga na Gor
Mahia ya Kenya alisema kwamba mchezo wa mpira wa miguu ni mchezo ambao
unatakiwa kucheza vile ambavyo unajua, halafu baadaye unaongeza vitu vingine kutoka kwa mwalimu.
“Tunachotarajia ni kufanya vizuri kwasababu
mwalimu aliyekuja nadhani kwa namna moja ama nyingine ameleta mabadiliko. Simba
ambayo iliyokuwepo msimu uliopita na ya sahizi ni tofauti, ukiangalia mechi
tulizofanya majaribo tumefanya vizuri”. Alisema Ivo.
“Timu inafanya vizuri kutokana na kwamba mwalimu
anajaribu kuwapa wachezaji uhuru wa kufanya kile kinachowezekana uwanjani.
Unajua Uwanjani unapompa uhuru mchezaji, nadhani anacheza vizuri bila wasiwasi,”.
Mlinda mlango Ivo Mapunda enzi za utawala wa kocha Zdravko Logarusic
”Alipokuwepo Mwalimu Logarusic nadhani kulikuwa na mipaka fulani ambayo lazima mchezaji ufuate na usipofuata anakuwa mkali na wachezaji walikuwa wanapoteza kujiamini”.
”Alipokuwepo Mwalimu Logarusic nadhani kulikuwa na mipaka fulani ambayo lazima mchezaji ufuate na usipofuata anakuwa mkali na wachezaji walikuwa wanapoteza kujiamini”.
“Kwahiyo nategemea kwamba tutafanya vizuri na lengo
letu ni kuleta mabadiliko ambayo lazima tushike nafasi ya kwanza katika msimu
wa ligi ambao utaanza hivi karibuni,”.
Kuhusu kusajiliwa kwa kipa bora wa msimu uliopita,
Hussein Shariff ‘Casillas’ kutoka Mtibwa Sugar, Ivo alisema ni changamoto nzuri
kwake kwasababu anaamini kuna vitu vipya atavichukua kwa kipa huyo kijana hali
kdhalika naye atajifunza kutoka kwake kutokana na uzoefu alionao.
“Changamoto
katika nafasi ya golini zipo. Unajua changamoto zinakuja pale unapofanya vibaya
na hiyo nafasi mwingine anaitolea macho. Kinachofanyika zaidi ni mazoezi ya
ziada na utulivu unapokuwa kwenye mchezo ili kupunguza makosa ambayo mwingine
hawezi kuyafanya”.
“Kitu kikubwa kinachoweza kunifanya pengine
nionekane kama nacheza vizuri ni jinsi ya
kuongea na wachezaji kadri mchezo unavyoendelea,”
“Kutokana na uzoefu wangu najua nini cha kufanya
pindi mchezo unapoendelea. Nakuwa nausoma mchezo na kujua nifanye nini ili
tuweze kukwepa madhara ambayo yakitokea watu wataangalia golikipa alikuwa ni
nani.”
“Uwepo wa golikipa mwingine Casillas nadhani
itanisaidia mimi. Unapokuwa na mtu mwingine tofauti toka timu nyingine,
unajifunza kitu kingine. Kama kipa huwezi kujua kila kitu, kwahiyo unaweza
kujifunza kutoka kwa kipa anayechipukia hata kama ni kipa mzoefu”.
“Hivyo Casillas ananisaidia mimi tunapokuwa
mazoezini au atakapokuwa anacheza mechi nitajifunza kwake na yeye anajifunza
vitu kutoka kwangu”.
Simba chini ya uongozi mpya unaoongozwa na Rais
Evans Elieza Aveva wamepania kufuta machungu ya kufanya vibaya kwa miaka mitatu
mfululizo.
Ili kuhakikishwa wanafanya vizuri, kamati ya
usajili chini ya ‘Big Boss’. Keptein wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ), Zacharia Hans Poppe, imefanya usajili makini.
Baadhi ya wachezaji waliosajiliwa na Simba ni Emmanuel Okwi, Pierre Kwizera, Pual Kiongera, Shaaban Kisiga, Abdi Banda, Joram Mgeveke na wengineo
EmoticonEmoticon