TFS YAJIDHATITI KUKABILIANA NA MAJANGA YA MOTO MSITUNI

June 17, 2025 Add Comment

 

Baadhi ya vijana wakipewa mafunzo ya utimamamu wa mwili kwa ajili ya kulinda na kuzuia mtoto usiharibu miti ya mashamba ya miti Sao Hill.Baadhi ya vijana wakipewa mafunzo ya utimamamu wa mwili kwa ajili ya kulinda na kuzuia mtoto usiharibu miti ya mashamba ya miti Sao Hill.Baadhi ya vijana wakipewa mafunzo ya utimamamu wa mwili kwa ajili ya kulinda na kuzuia mtoto usiharibu miti ya mashamba ya miti Sao Hill.

Na Fredy Mgunda,Mufindi

Ikiwa ni kuelekea msimu wa kipindi cha kiangazi, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS kupitia Shamba la Miti Sao Hill umeendesha zoezi la usahili kwa watumishi wa muda watakaounda kikosi maalumu kwa  ajili ya kupambana na kudhibiti majanga ya moto katika maeneo yanayolizunguka Shamba.


Zoezi hilo limefanyika leo Juni 16, 2025 katika viwanja vya Shamba la Miti Sao Hill likishirikisha wahifadhi wa Shamba, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Jeshi la Polisi, likilenga kupata vikosi vitakavyohudumu katika Makao Makuu ya Shamba pamoja na Tarafa ya II ya Shamba Ihefu.


Akizungumza katika zoezi hilo Mhifadhi Mwandamizi anayesimamia Utumishi na Utawala Felista Bayo amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 Shamba linatarajia kuajiri watumishi wa muda 192 kwa ajili ya kukabiliana na kupambana na majanga ya moto kwa kipindi chote cha kiangazi.


Ameongeza kuwa licha ya maombi kuwa mengi kulinganisha na nafasi zilizotajwa, Shamba la Miti Sao aaHill lina shughuli nyingine zinazoendelea katika vituo vyake vyote ikiwa ni pamoja shughuli za bustani na usafi wa mashamba, hivyo wanaokosa nafasi katika vikosi hivyo wanapata fursa ya kuendelea na shuguli nyingine za Shamba.


Kwa upande wake Mhifadhi anayesimamia Kitengo cha Ulinzi wa Msitu dhidi ya moto Murya Sawa amesema kuwa baada ya kukamilisha zoezi hili ni matarajio ya TFS kupitia Shamba la Miti SaoHill kuwa watumshi hawa muda  waliopata nafasi watafanya kazi hiyo kwa weledi kwa kutanguliza uzalendo huku akihimiza ushirikiano baina ya wananchi wote wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi katika kulinda rasilimali za misitu.


Naye Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Mufindi Ashery Kitundu amesema kuwa lengo mama la jeshi la zimamoto ni kuhakikisha matukio ya moto hayatokei kwa kutoa elimu, na kuyadhibiti pindi yanapotokea hivyo ni watumishi hawa wa muda watakuwa mabalozi wazuri katika maeneo yao waliyotoka kwa kushirikiana na jeshi la zimamoto katika kutoa elimu ya kuepuka na kukabilina na majanga ya moto.


Usaihili huo unatarijiwa kuendelea hapo kesho katika Tarafa ya Kwanza ya  Shamba Irundi kisha Tarafa ya Tatu Ihalimba, na Tarafa ya Nne Mgololo.

MAADHIMISHO YA MIAKA 25 YA JUMUIYA YA TATHIMINI AFRIKA ( AfrEA ) WAFANYIKA ADDIS ABABA-ETHIOPIA

June 16, 2025 Add Comment


*Na Mwandishi Wetu – Addis Ababa, Ethiopia*


Tanzania imeshiriki Maadhimisho ya Miaka 25 ya Jumuiya ya Tathmini Afrika (AfrEA) yanayofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 16  hadi 18 Juni, 2025, katika Kituo cha Mikutano cha Umoja wa Mataifa (UNECA), jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bi. Sakina Mwinyimkuu.

 Washiriki wengine kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ni Mkurugenzi wa Mipango na Bajeti Bw. Eleuter Kihwele na Mkaguzi Mkuu wa Ndani katika Ofisi hiyo Bw. Exavery Salira.


Maadhimisho hayo ya siku tatu yameandaliwa kwa lengo la kuenzi mchango wa tathmini katika maendeleo barani Afrika, na kuimarisha uwajibikaji wa sera kwa kutumia ushahidi (Evidence Based) katika kufanya maamuzi.

Aidha Washiriki kutoka nchi mbalimbali ndani na nje ya bara la Afrika wanajadili mbinu bunifu na jumuishi za tathmini kwa maendeleo endelevu yenye muktadha wa Kiafrika.




*MWISHO*

RAIS SAMIA ATEMBELEA MRADI WA REA SIMIYU

June 16, 2025 Add Comment

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametembelea mradi wa nishati safi ya kupikia wa shule ya Sekondari ya Wasichana Simiyu iliyopo Bariadi mkoani humo na kupewa maelezo na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga wakati akifungua shule hiyo leo tarehe 16 Juni, 2025

Mradi huo unahusisha usimikaji wa mfumo wa kupikia kwa kutumia gesi yaani LPG, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, hivyo kuchangia katika utunzaji wa mazingira na kulinda afya ya wanafunzi na walimu.



Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetoa ufadhili wa kiasi cha Shilingi Shilingi Milioni 14 kwa ajili ya ujenzi na usimikaji wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika shule hiyo.

BEI YA KUJAZA GESI LPG KWA MATUMIZI YA KUPIKIA NI HIMILIVU-KAPINGA

June 16, 2025 Add Comment


*📌 Wizara ya Nishati na TAMISEMI zaendelea kushirikiana kuhakikisha  Shule mpya zinafungwa mifumo ya Nishati Safi ya Kupikia*

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema gharama ya kujaza gesi kwenye mitungi (LPG) ni himilivu ikiwa ni jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ili kuwezesha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Juni 16, 2025 katika ziara ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Simiyu  wakati wa kuzindua Shule Maalum ya Sayansi ya Wasichana ya Simiyu ambayo imefungwa miundombinu ya nishati safi ya kupikia. 



“Mheshimiwa Rais ulituelekeza Taasisi ambazo zinahudumia watu zaidi ya mia moja tuzifungie miundombinu ya nishati safi ya kupikia, Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na TAMISEMI tunatekeleza agizo hilo kwa kuzifungia mifumo ya nishati safi shule mpya ambazo zinajengwa." Amesema Kapinga

Ameeleza kuwa,  uwezo wa shule hiyo ni wanafunzi 800 na mifumo ya Nishati Safi ya Kupikia iliyofungwa ina uwezo wa kuhudumia wanafunzi 800.

Ameongeza kuwa, kwa idadi hiyo ya wanafunzi 800  mtungi wa gesi katika Shule ya Wasichana Simiyu utakuwa ukijazwa kila  baada ya miezi miwili.



WIZARA YA NISHATI NA TAASISI YASHIRIKI MAADHIMISHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA DODOMA

June 16, 2025 Add Comment


Wizara ya Nishati na taasisi zilizo chini yake inashiriki Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo yameanza Juni 16, 2025 katika viwanja vya Chinangali, Jijini Dodoma.

Maadhimisho hayo yamebebwa na kaulimbiu isemayo "Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijiti Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji", 

Watalaam wa Wizara pamoja na kueleza mafanikio yaliyofikiwa katika Sekta ya Nishati ikiwemo ukamilishaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere na usambazaji wa umeme vijijini, wanatoa elimu  kwa njia mbalimbali ikiwemo machapisho na vitendo kuhusu ajenda ya kitaifa ya  utekelezaji wa Mkakati wa Nishati Safi ya kupikia.

Taasisi za Wizara ya Nishati zinazoshiriki maadhimisho hayo ni Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli ( PURA),  Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC), Wakala wa Nishati Vijijini ( REA) na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).