MAWAZIRI WA NISHATI JUMUIYA YA SADC KUKUTANA NCHINI ZIMBABWE

May 30, 2025 Add Comment




📌.*Masuala ya Umeme, Gesi, Nishati Safi kujadiliwa*


Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga ameongoza jopo la Wataalam  kutoka Wizara ya Nishati katika Kikao cha awali cha Kamati Ndogo ya Nishati ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kilicholenga kujadili  maandalizi ya Mkutano wa Pamoja wa Kamati ya Mawaziri wa SADC wanaoshughulikia masuala ya Nishati utakaofanyika nchini Zimbabwe.

Kikao hicho cha awali kimefanyika tarehe 30 Mei 2025 katika Ukumbi wa Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao.

Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa SADC unatarajia kufanyika nchini Zimbabwe  Mei  30  had 04 Juni 2025 ukitanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Nishati wa SADC.

Kikao hicho cha Mawaziri  kitajadili ajenda mbalimbali ikiwemo hali ya upatikanaji wa nishati ya umeme katika Kanda; Maendeleo ya sekta ndogo ya Mafuta na Gesi, Matumizi ya Nishati Safi na kujadili nafasi na utayari wa Kanda katika kutekeleza Azimo la Dar es Salaam lililotokana na Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Misheni 300.



Washiriki wengine katika kikao hicho kilichofanyika kwa njia ya mtandao wametoka katika  nchi zote zilizopo katika Jumuiya ya SADC.

WAZIRI KOMBO AWASISITIZA MACHIFU KUSHIRIKIANA NA SERIKALI

May 30, 2025 Add Comment
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amewasisitiza Machifu wa Kanda ya Vita ya Majimaji Kusini mwa Tanzania kuendelea kushirikiana na Serikali wakati wakitekeleza majukumu yao ya kimila katika jamii.

PUMA ENERGY TANZANIA KUPITIA UPYA MPANGO MKAKATI WA BIASHARA

May 30, 2025 Add Comment

 Wawekezaji wa PUMA Energy Tanzania, ambao ni Serikali ya Tanzania na Puma Investments Limited, wamekubaliana kufanya mapitio ya mpango mkakati wa biashara wa kampuni hiyo ndani ya mwaka huu.


Mpango huu mpya wa biashara unalenga kuongeza uwekezaji, kupanua mtandao wa usambazaji, na kuongeza idadi ya bidhaa, kwa lengo la kuimarisha mchango wa wa kampuni hiyo katika uchumi wa Tanzania, na kukuza maendeleo ya sekta ya nishati.

Hayo yalibainishwa Jumatatu, Mei 26, 2025 wakati wa ziara ya viongozi wa ngazi ya juu wa PUMA Energy kwenye Ofisi ya Msajili wa Hazina iliyopo jijini Dar es Salaam, wakiongozwa na Bw. Mark Russel, Afisa Mtendaji Mkuu wa PUMA Energy Duniani.

Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema mapitio ya mpango mkakati wa biashara yanalenga kuona ukuaji wa kampuni unalingana na vipaumbele vya maendeleo ya taifa, pamoja na kufungua milango ya fursa mpya katika sekta ya nishati.

 “Uongozi wa kampuni na bodi lazima waangalie upya mpango mkakati wa biashara ndani ya mwaka huu ili kuanzia mwaka ujao tuweze kuzitumia vizuri fursa tulizonazo,” alisema Bw. Mchechu, huku akiweka wazi kuwa utekelezaji wa mpango mkakati mpya utaanza Januari mwakani.

PUMA Energy Tanzania ni kampuni inayomilikiwa kwa asilimia 50 na Serikali ya Tanzania na asilimia 50 na Puma Investments Limited.

Kampuni hii ni tawi la Puma Energy Holdings Pte Ltd, sehemu ya Trafigura PE Holding Ltd.

Bw. Mchechu alisisitiza kuwa uwekezaji wa Serikali katika PUMA ni mkakati muhimu unaolenga kuiwezesha Serikali kuwa na ushawishi mkubwa katika sekta ya nishati na mtandao wa usambazaji wa mafuta nchini.

Kwa upande wake Bw.Russel, alisema Tanzania ina fursa nyingi za kukuza biashara, ikiwemo miradi ya gesi ya asilia (LNG) na gesi ya kupikia (LPG).

“Tuna mpango wa kupanua huduma na kuongeza aina za bidhaa tunazotoa kwa jamii. Kupitia ushirikiano wetu na Serikali, tutashirikiana kufungua fursa zaidi na kukuza biashara hii,” alisema Bw. Russel.

Bw. Ben Quattara, Mkuu wa kampuni za PUMA Energy Afrika, alibainisha kuwa Tanzania ni mshirika muhimu katika biashara za PUMA barani Afrika na kampuni ina nia ya kuendeleza uwekezaji na faida zaidi hapa nchini.

Bi. Fatma Abdallah, Mkurugenzi Mtendaji wa PUMA Energy Tanzania, aliripoti ongezeko la asilimia 51 la faida mwaka 2024 na kufungua vituo vipya vya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) pamoja na upanuzi wa biashara ya gesi ya kupikia (LPG) katika mikoa kadhaa ikiwemo Dodoma, Mwanza, na Arusha.

“Tegemeeni mambo makubwa kutoka PUMA Tanzania katika miezi na miaka ijayo,” alimalizia Bi. Abdallah.

 


WAJUMBE WA MKUTANO MKUU CCM WAKIBURUDIKA KUELEKEA KUZINDUA ILANI

May 30, 2025 Add Comment

 



Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiburudika burudani ya mziki kutoka Kikundi cha Sanaa cha Tanzania One Theatre (TOT), kikiongozwa na Malkia wa Mipasho na Mziki wa Taarab, Bi. Khadija Omar Abdallah Kopa, leo Ijumaa tarehe 30 Mei 2025, jijini Dodoma.

Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa huo ukiongozwa na Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ulianza jana Alhamis, tarehe 29 Mei 2025, na leo unaendelea katika siku yake ya pili, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma, ambapo mojawapo ya agenda itakuwa ni kuzindua Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2025 - 2030.








BALOZI MATINYI AKUTANA NA WATANZANIA WANAOISHI NCHINI USWIDI

May 30, 2025 Add Comment

 


Balozi wa Tanzania katika Ufalme wa Uswidi, Mhe. Mobhare Matinyi, tarehe 29 Mei, 2025, alifanya kikao na Watanzania wanaoishi nchini humo katika viwanja vya ofisi za ubalozi jijini Stockhom.


Katika kikao hicho kilicholenga kufahamiana na kujadiliana kuhusu masuala ya Diaspora, Mhe. Balozi Matinyi alielezea tafsiri ya neno "diaspora" kwa mujibu wa Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001, toleo la mwaka 2024, iliyozinduliwa tarehe 19 Mei, 2025, jijini Dar es Salaam na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Balozi alieleza kuwa sera hii inawatambua Diaspora kuwa ni raia wa Tanzania wanaoishi nje (Citizen Diaspora) na raia wa nchi zingine wenye asili ya Tanzania (Non-Citizen Diaspora). 


Mhe. Balozi Matinyi aliwaeleza Watanzania hao waliotoka miji mbalimbali ya Uswidi, kwamba sera hiyo imetambua ushiriki wa Diaspora katika maendeleo ya nchi yetu huku akirejea wito wa Mhe. Rais Dkt. Samia wa kuwataka Diaspora wawekeze nchini ili kuchangia maendeleo ya taifa.

Akiinukuu hotuba ya bajeti bungeni ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabiti Kombo, Mhe. Balozi Matinyi aliwaambia kwamba kwa mwaka 2024 Diaspora wa Tanzania waliwekeza fedha kiasi cha shilingi bilioni 7.5 katika mfuko wa UTT-AMIS na shilingi bilioni 9.28 kwenye sekta ya milki kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na sekta binafsi.


Baada ya mazungumzo hayo Mhe. Balozi Matinyi aliwataka wajenge umoja na ushirikiano kama alama kuu za Watanzania popote walipo duniani na kupigania maslahi ya nchi yao wakati wote.