NCAA YATOA MAFUNZO KWA WADAU WA UTALII KUHUSU MATUMIZI YA MFUMO MPYA WA SAFARI PORTAL V2

May 29, 2025 Add Comment


Na Kassim Nyaki, NCAA.


Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imetoa mafunzo ya siku mbili kuanzia tarehe 29 hadi 30 Mei, 2025 kwa wadau wa Utalii kuhusiana na matumizi ya mfumo mpya wa *Safari Portal V2* ulioboreshwa kutoka mfumo wa zamani wa Safari Portal.


Akifungua Mafunzo hayo Kaimu Meneja wa Huduma za Utalii na masoko NCAA, Afisa Uhifadhi Mkuu Peter Makutian ameeleza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wadau wote wa Utalii kuhusu matumizi ya mfumo mpya wa makusanyo ya mapato yatokanayo na shughuli za Utalii ambao umeboreshwa ili kurahisisha utoaji huduma kwa wadau wote wanaofanya kazi na NCAA.

"Tumeboresha mfumo wetu wa makusanyo ya mapato ya Utalii na utaaanza kutumika kuanzia tarehe  31/05/2025, kwa hiyo ni muhimu wadau wetu wanaopata huduma kupitia mfumo huu wawe na uelewa ya maboresho yaliyofanyika na kuwasaidia namna ya kuhamisha taarifa zao kwenye mfumo mpya kabla ya tarehe ya kuanza mfumo huo" alilisitiza Makuatian.


Makutian ameongeza kuwa sababu zilizopelekea kuboresha mfumo huo ni kuendana na mabadiliko ya kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano sambamba na kuzingatia mapendekezo ya Wadau wa utalii ambao ndio watumiaji wakuu wa mfumo huo.

Mafunzo hayo yameshirikisha makundi mbalimbali katika mnyororo wa sekta ya utalii ikiwemo Waongoza watalii, wamiliki wa kampuni za utalii, madereva wa utalii, wamiliki wa hoteli na wadau wengine wanaohusika na sekta ya Utalii.

Wadau wa utalii walioshiriki mafunzo hayo wametoa pongezi kwa uongozi wa NCAA kwa maboresho ya mfumo huo ambao umerahisisha taratibu za malipo bila kutumia mda mrefu wanapokuwa na shughuli za utalii na wageni ndani ya hifadhi ya Ngorongoro



DKT.BITEKO ATAJA MAENEO SITA YA VIPAUMBELE UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM 2020/2025

May 29, 2025 Add Comment


📌 CCM yajivunia kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwa jamii


📌 Rais Samia asema CCM kuzindua Ilani yake kesho


📌 CCM yazalisha ajira 800,000 kwa vijana 2020/2025


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita aliyowasilisha ni ya mwisho katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020. 


Amesema hayo Mei 29, 2025 wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Mkutano Mkuu Maalum wa  CCM Taifa - 2025 jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa. 


Ametaja maeneo sita muhimu ya vipaumbele  katika utekelezaji wa Ilani hiyo ya CCM kuwa ni pamoja na kulinda  na kuimarisha misingi ya utu, usawa, haki na uongozi bora ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa.

Dkt. Biteko ameendelea kwa kusema kuwa eneo lingine ni kukuza  uchumi wa kisasa, fungamanishi, jumuishi na shindani  uliojengwa katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi.


Aidha, kipaumbele kingine “ Kuleta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula na kujitegemea kwa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, maji, umeme na makazi vijijini na mijini na kutengeneza ajira zisizopongua milioni nane katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya vijana,”  ameongeza Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa kumekuwepo na mafanikio makubwa ikiwemo nchi kuendelea kuwa na amani, umoja na mshikamano pamoja na kuendelea kuenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na kudumisha Muungano wa Tanzania.


“ Vilevile, Serikali imeendelea kuimarisha demokrasia, utawala bora na haki za binadamu kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuondoa zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na hivyo kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari ili kuwezesha wananchi kupata habari kwa wakati,” amesema Dkt. Biteko.

Ameendelea kusema  kuwa mafanikio hayo  yamechagizwa na falsafa aliyoianzisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya 4R ambayo ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga Upya.


Amesisitiza “ Falsafa  hiyo imekuwa dira na nguzo muhimu ya kisera katika kuijenga upya Tanzania yenye mshikamano, haki na maendeleo endelevu kwa misingi ya demokrasia na ushirikishwaji wa wananchi katika masuala ya msingi ya Taifa.”



Kupitia mkutano huo Dkt. Biteko alielezea mafanikio ya Rais Samia kitaifa na kimataifa hususan katika sekta ya nishati kwa kuwa kinara wa nishati safi ya kupikia barani Afrika.


Akihutubia katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Mkutano Mkuu huo ni sehemu muhimu ya maandalizi ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.


“ Kesho  tutafanya uzinduzi wa Ilani tutakayoinadi kwa wananchi ili kutupa nafasi nyingine ya kuongoza kwa miaka mitano,” amesema Dkt. Samia.


Amebainisha  kuwa Ilani hiyo imehusisha vipaumbele  vya Chama na kuwa kabla ya kuiwasilisha  kwa wajumbe wameona ni muhimu kupitia utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2020 hadi 2025.


Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa CCM, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema  lengo la  mkutano huo ni kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa mwaka  2020 hadi 2025, kuzindua Ilani mpya 2025 hadi 2030 na kupitia maboresho machache ya Katiba ya CCM.


Aidha, Mkutano huo ulioongozwa  na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan umehudhuriwa na viongozi wa vyama vya siasa nchini, mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania pamoja wawakilishi wa vyama rafiki kutoka nchi mbalimbali za Afrika, China na Korea ya Kaskazini na Urusi.

 

MWISHO

DCEA YAIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA KUPITIA MAFUNZO KWA VIONGOZI WA MITAA SAME

May 29, 2025 Add Comment

 



Na Ashrack Miraji Tanga Raha

Katika harakati za kitaifa za kuikomboa jamii dhidi ya janga la dawa za kulevya, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini imeendesha mafunzo maalum kwa viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya wilaya hadi vitongoji, katika Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro.

Mafunzo hayo yaliyofanyika leo, Mei 29, 2025, katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, yamelenga kuwawezesha viongozi hao kutambua, kuzuia na kushughulikia changamoto zinazotokana na matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya. Viongozi hao pia wamehimizwa kuzingatia maadili, uwajibikaji na ushirikiano wa kijamii katika mapambano hayo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mheshimiwa Kasilda Mgeni, alisema kuwa dawa za kulevya si tu kwamba zina madhara ya kiafya kwa binadamu, bali pia zinachangia kudhoofisha uchumi, kuvuruga familia, kuporomosha maadili, kupunguza nguvu kazi ya taifa na kuongeza matukio ya uhalifu.


Alisema: “Hili ni janga linalohitaji nguvu ya pamoja kuanzia kwa viongozi, wazazi, walimu na vijana wenyewe ambao ndio waathirika wakuu wa dawa za kulevya. Hivyo nawahimiza kupitia mafunzo haya mkawe mabalozi na waelimishaji; muhamasishe na msimamie utekelezaji wa mikakati ya kupambana na dawa za kulevya katika maeneo yenu.”

Aidha, aliwataka viongozi wa serikali kuhakikisha kuwa wanakuwa wawajibikaji, waadilifu na kutojihusisha au kufumbia macho biashara haramu ya dawa za kulevya katika maeneo yao. Alibainisha kuwa serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo.


Kwa upande wake, Afisa Elimu kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Kanda ya Kaskazini, Ndg. Shaban Miraji, alisema kuwa sababu kuu zinazochangia matumizi ya dawa za kulevya ni pamoja na malezi duni, ukosefu wa elimu sahihi kuhusu madhara ya dawa hizo, pamoja na hali ngumu ya kiuchumi.

Kwa upande wake Katibu tawala wa wilaya ya Same.  Bi. Upendo Wela akifunga Mafunzo hayo amesema kuwa ni wajibu wa kila mmoja aliyepata mafunzo hayo kuhakikisha wanapambana na kilimo cha mirungi na bangi ili kiweze kumalizika kabisa ndani ya wilaya ya Same kwa kushirikiana kwa pamoja

Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015, mtu yeyote atakayekutwa akilima bangi au mirungi, kufanya biashara, kusafirisha au kumiliki kiasi cha bangi au mirungi kisichozidi kilo 100, atahukumiwa kifungo kisichopungua miaka 30. Iwapo kiasi hicho kitazidi kilo 100, adhabu ni kifungo cha maisha.

Mafunzo hayo yaliambatana na mada mbalimbali, ambapo mada kuu ilikuwa kuhusu dawa za kulevya, huku nyingine zikihusu maadili kwa watumishi wa umma, mapambano dhidi ya rushwa, pamoja na kuhamasisha kilimo mbadala kama njia ya kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.




 

Mradi wa Miaka 13 wa Amend Wazidi Kutoa Matunda Tanzania

May 29, 2025 Add Comment

WADAU wa usalama wa barabarani wametoa wito wa kuanzishwa kwa mjadala wa kitaifa kuhusu namna ya kudhibiti ajali za barabarani, wakisisitiza kuwa vifo na majeruhi vinavyotokana na ajali hizo hususani kwa Watoto, haviwezi kuvumilika tena katika jamii ya Watanzania.

PROF. MUSHI: TUONDOE VIKWAZO VYA USAJILI KWA WANAFUNZI WA KIKE

May 29, 2025 Add Comment
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, ametoa wito kwa wadau wa elimu nchini kuunga mkono juhudi za serikali kwa kufadhili masomo ya elimu ya juu kwa wasichana hasa wanaoishi kwenye mazingira magumu.