KUPITIA MRADI WA FEMA AILEADERS WABUNGE WABUNIFU NA MAKUNDI MENGINE WAPIGWA MSASA AKILI MNEMBA

May 21, 2025 Add Comment





Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam


Kupitia Mradi wa FemAILeaders, Shirika la Women Political Leaders (WPL), GIZ Makao Makuu, GIZ Tanzania na Omuka imeandaa Mafunzo ya Akili Mnemba “Artificial Intelligence - AI” yaliyoanza Mei  19 hadi 20 mwaka 2025, Dar es Salaam yaliyolenga mambo mbalimbali ikiwemo ulinzi wa mtandao,ubunifu na matumizi ya AI.

 

Mafunzo haya yaliwaleta pamoja Wabunge, Wabunifu na Makundi mengine kwa lengo la kuangazia ubunifu na matumizi ya AI, ulinzi wa kimtandao, utatuzi wa changamoto za AI na uhitaji wa kisera.

Delegation ya Bunge iliongozwa na Mhe Salome Makamba na kujumisha Mhe Prof Joyce Ndalichako, Mhe Esther Matiko, Mhe Ng’wasi Kamani na Makatibu wa Kamati za Bunge, Adv Ganjatuni Kilemile na Pius Katabazi.

 

Tanzania imeendelea kuongoza barani Afrika kwa Kuimarisha Uelewa na Ushawishi wa Wabunge Wanawake ili wawe Vinara wa AI hivyo kuchangia kwa Tanzania kunufaika na fursa zinazotokana na Akili Mnemba - AI. Tanzania imechaguliwa kuwa Mfano wa Kuigwa barani Afrika katika eneo hili. 

 

Aidha, Mradi wa FemAILeaders umeweza kufanyika Tanzania kufuatia jitihada za Mhe Neema Lugangira (Mb) ambae pja ni Mwakilishi wa Afrika/Mjumbe Maalum wa Afrika wa Shirika la Women Political Leaders (WPL) hivyo ametumia nafasi hiyo kuileta fursa hii Tanzania.
 

PANGANI WAPONGEZWA KWA KUSHIRIKI VYEMA UBORESHAJI WA DAFTARI AWAMU YA PILI

May 21, 2025 Add Comment

 

 
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele leo Mei 21, 2025 ametembelea na kukagua mwenendo wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na uwekaji wazi wa Daftari la awali unaoendelea katika mikoa 16 ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar Katika Halmashauri ya Wilaya ya Pangani katika Jimbo la Uchaguzi la Pangani Mkoani Tanga. 

Zoezi la uboreshaji awamu ya pili linataraji kuanza Mei 16 hadi 22, 2025 sambamba na uwekaji wazi wa daftari la awali la Wapiga Kura na vituo vitafunguliwa kuanzia Saa 2:00 asubuhi hadi Saa 12:00 jioni.
Jaji Mwambegele aliwapongeza wananchi wa Pangani kwa namna walivyojitokeza kuboresha taarifa zao na kutazama daftari la awali lililobandikwa katika vituop mbalimbali walivyovitumia wakati wa uboreshaji wa daftari hapo awali. 



Mkazi wa Mtaa wa Kimanga uliyopo Kata ya Kimanga, Wilayani Pangani, Mtwana Juma akionesha kadi yake baada ya Kuboresha 
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akimkabidhi Kadi ya Mpiga Kura Mkazi wa Mtaa wa Kimanga uliyopo Kata ya Kimanga, Wilayani Pangani, Mtwana Juma  leo Mei 21, 2025  wakati alipotembelea na kukagua mwenendo wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na uwekaji wazi wa Daftari la awali unaoendelea katika mikoa 16 ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar Katika Halmashauri ya Wilaya ya Pangani katika Jimbo la Uchaguzi la Pangani Mkoani Tanga. 
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza na Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Pangani, Ndg. Charles Edward Fussi. 

Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akisalimiana na wananchi wa Pangani waliojitokeza kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye kituo cha Soko la Samaki Pangadeco
Jaji Mwambegele akimsikiliza Mwandikishaji Msaidizi wa Kituo cha Soko la Samaki Pangadeco Wilayani Pangani.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegelakiwa kituo cha Ofisi ya Mtendaji Kata ya Pangani 

DC SAME APIGA MARUFUKU MAJI MACHAFU YA KIWANDA KUINGIA MTONI

May 21, 2025 Add Comment

 




Na Ashrack Miraji

Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amepiga marufuku mara moja utiririshaji wa maji machafu yenye kemikali kutoka katika Kiwanda cha kuchakata mkonge kinachomilikiwa na Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MELT), kilichopo katika shamba la mkonge la Hassan Sisal Estate, Kata ya Makanya.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia wasiwasi wa uchafuzi wa mazingira na athari za kiafya kwa wakazi wa Makanya na maeneo jirani yanayopata huduma ya maji kupitia mto unaopita karibu na kiwanda hicho.

Mhe. Kasilda alitembelea baadhi ya maeneo ya mto huo na kujionea hali ya maji yaliyobadilika rangi kuwa nyeusi na kutoa harufu kali, hali iliyomsukuma kufika kiwandani kujiridhisha na chanzo cha uchafuzi huo.


“Kuanzia sasa ni marufuku kuelekeza maji machafu yenye kemikali kwenye mto ambao maji yake yanatumika kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu, hususan kilimo na mifugo. Baadhi ya wananchi wanayatumia moja kwa moja,” alisema DC Kasilda.

Alisisitiza kuwa uamuzi huo unalenga kulinda afya za wananchi na mazingira kwa ujumla.

Aidha, Mhe. Kasilda alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same kuhakikisha wataalam wa mazingira na afya wanafika kiwandani hapo kufanya uchunguzi wa kina ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.


“Serikali inathamini uwekezaji, lakini ni lazima wawekezaji wazingatie sheria na taratibu ili kulinda afya za wananchi na kukuza uchumi wa taifa kwa njia endelevu,” alisema.

Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa wilaya pia alieleza kutoridhishwa na hali ya usafi kiwandani hapo na kuwataka wasimamizi wa kiwanda kufanya usafi wa maeneo yao ya kazi ili kuepuka hatari ya magonjwa ya mlipuko kwa wafanyakazi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, kifungu cha 129 kinakataza mtu yeyote kuachilia maji taka au taka hatarishi moja kwa moja kwenye mazingira bila kibali au bila kuyatibu.

Sheria hiyo pia inataka viwanda kuwa na mitambo ya kisasa ya kutibu majitaka kabla ya kuyamwaga kwenye mazingira. Endapo ukiukwaji utabainika, Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC) itachukua hatua kali dhidi ya wahusika.




 

BENKI YA CRDB KUIWEZESHA ZANZIBAR KUJENGA SHULE 23 ZA GHOROFA

May 21, 2025 Add Comment

 

Zanzibar. Tarehe 21 Mei 2025: Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Benki ya CRDB kwa jitihada zake za kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo baada ya kusaini mkataba wa mkopo nafuu wa takriban Euro milioni 80 (shilingi bilioni 240).

Akizungumza kwenye hafla ya kutiliana saini mkopo huo kati ya Benki ya CRDB na Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Rais Dkt. Mwinyi amesema maendeleo ya taifa yanahitaji ushirikiano wa serikali na sekta binafsi na Benki ya CRDB imekuwa ikionyesha hilo kwa vitendo kwa kujitoa kwake kila inapohitajika kufanya hivyo.
“Mkopo wa Euro milioni 79.962 utatusaidia kujenga shule 23 za ghorofa mbili. Shule hizi zitajengwa Pemba na Unguja hivyo kusaidia kutatua uhaba wa vyumba vya madarasa kwa kiasi kikubwa. Lengo letu ni kuwaona vijana wetu wanasoma katika mazingira rafiki ya kukua kiumri na kielimu,” amesema Rais Dkt. Mwinyi.


Uboreshaji huu wa mazingira ya shule, Rais amesema ni muhimu ili kuwapata viongozi bora, madaktari, wahandisi, wahasibu, wanasheria na wasomi wengine mahiri hivyo ni lazima kuwekeza kwenye elimu.
“Kila mtu mwenye maono mazuri anatambua umuhimu wa elimu hivyo mkopo huu utakaoboresha miundombinu, umekuja kwa wakati sahihi sasa hivi. Nawapongeza Wizara ya Elimu kwa kulifanikisha hili kwani ilikuwa nikipita wananchi wanaomba shule ya ghorofa kila mahali mpaka kule Tumbatu. Sasa suala hilo limekamilika na fedha za ujenzi wake ndio hizi hapa,” amesema Rais Mwinyi.

Benki ya CRDB imetoa mkopo huo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikishirikiana na Benki ya Deutsche ya nchini Hispania kwa malengo ya kufanikisha ujenzi wa shule hizo zitakazokuwa na madarasa ya kisasa, vyoo bora, bustani za kuvutia, ofisi nadhifu za utawala, maabara na maktaba za kisasa pamoja na viwanja safi vya michezo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Adulmajid Nsekela amesema kwa muda mrefu wamekuwa wadau muhimu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Serikali zote yaani ile la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi mjini au vijijini.


“Kwa hatua tuliyofikia, kwa sasa pande zote yaani Benki ya CRDB, Benki ya Deutsche na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tunakamilisha masharti ya awali ya mkopo kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi kusudiwa. Ni matumaini yetu kuwa masharti haya ya awali yatakamilishwa kabla ya mwishoni mwa mwezi ujao hivyo kuwezesha kuanza haraka iwezekanavyo utekelezaji wa mradi huu,” amesema Nsekela.
Nsekela ameongeza kuwa mkopo huo unajumuisha Euro milioni 69.312 sawa na asilimia 85 utakaotolewa kwa ushirikiano wao na Benki ya Deutsche huku kiasi kilichobaki cha Euro milioni 10.65 sawa na asilimia 15 kitatolewa na Benki ya CRDB peke yake suala lililopata baraka zote za SMZ kupitia Wizara ya Fedha na Mipango.

Nsekela pia amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa juhudi zake za kuimarisha uchumi wa Zanzibar ikiwamo uuzaji na uorodheshaji wa Hatifungani ya Sukuk iliyotolewa na SMZ mapema mwaka huu na kukusanya shilini bilioni 381 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa kufuata misingi ya dini ya Kiislamu.
Benki ya CRDB imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo visiwani Zanzibar ikishiriki kufanikisha miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 130. Kwa mkopo uliosainiwa, unaifanya Benki ya CRDB kufikisha jumla ya shilingi billion 375 ya uwezeshaji wa miradi inayosimamiwa na SMZ.





RAIS WA NAMIBIA ATEMBELEA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM,ALAKIWA NA MKUU WA CHUO DKT KIKWETE

May 21, 2025 Add Comment


Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akimkaribisha Rais wa Jamhuri ya Namibia Mhe. NetumboNandi-Ndaitwah alipowasili chuoni hapo leo asubuhi ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kiserikali ya siku mbili nchini.

Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah amefurahi kualikwa kuzungumza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam leo na ameeleza kuwa atatumia fursa hiyo kuwahamasisha wanafunzi kushiriki katika fursa mbalimbali za kujenga nchi kizalendo na za uongozi.