WAZIRI MKUU MAJALIWA : SERIKALI IMEJIPANGA KUDHIBITI MAGUGUMAJI ZIWA VICTORIA

May 19, 2025 Add Comment


_▪️Amshukuru Rais Dkt. Samia ununuzi wa mitambo ya uteketezaji wa magugumaji

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha changamoto ya uwepo wa magugumaji katika ziwa Victoria inapatiwa ufumbuzi ili kuwezesha shughuli za kijamii ziweze kuendelea katika maeneo hayo.

 



”Ninamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa fedha za ununuzi wa mitambo mikubwa ya kuteketeza magugumaji ndani ya ziwa Victoria ili kuwezesha shughuli za uvuvi, usafiri na usafirishaji kuendelea.”

 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Mei 19, 2025) wakati akizungumza na wananchi alipokagua shughuli ya udhibiti wa magugumaji katika eneo la Kigongo-Busisi akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.

 


Mheshimiwa Majaliwa amesema magugumaji hayo yamekuwa yakiathiri kwa kiwango kikubwa shughuli mbalimbali za kijami na kiuchumi katika ziwa hilo, hivyo ununuzi wa mitambo hiyo utasaidia kuteketezwa kwa magugu hayo.

 

Aidha, Waziri Mkuu amewashukuru wananchi wa maeneo hayo wakiwemo wavuvi ambao wamejitolea kushirikiana na Serikali katika zoezi la kuyaondoa magugumaji hayo.

 

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira iendelee na kazi ya kuyaondoa magugumaji hayo hadi pale yatakapomalizika ili kuhakikisha shughuli za kijami zinaendelea bila ya kikwazo chochote.

 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Cyprian Luhemeja akitoa taarifa kuhusu shughuli ya kuteketeza magugumaji hayo kwa Waziri Mkuu amesema kwa sasa wanaendelea na kazi ya kuyaondoa magugumaji ya asili ambayo yamesambaa katika eneo la ukubwa wa ekari zaidi ya 300.

 

Amesema magugumaji hayo ambayo yamegawanyika katika aina tatu (salivinia molesta ambalo ni jipya, water hyacinth na gugumaji la asili aina ya Lutende) yameathiri mfumo wa ikolojia, shughuli za usafiri na usafirishaji na shughuli za uvuvi katika baadhi ya maeneo ndani ya Ziwa Victoria

 

Katibu Mkuu huyo amesema wanatarajia kumaliza kazi ya kuyateketeza magugumaji mwezi Julai, 2025 na hivyo kuwezesha shughuli za uvuvi, usafiri na usafirishaji kuendelea katika ziwa Victoria kama ilivyokuwa awali.

BIASHARA YA MAZAO YA MISITU NA NYUKI YAPAA – MAUZO NJE YA NCHI YAONGEZEKA KWA ASILIMIA 333%

BIASHARA YA MAZAO YA MISITU NA NYUKI YAPAA – MAUZO NJE YA NCHI YAONGEZEKA KWA ASILIMIA 333%

May 19, 2025 Add Comment

 MH CHANA.jpg

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akiwasilisha akadirio ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
-----
WhatsApp Image 2025-05-19 at 10.42.45.jpeg

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Kutoka kushoto ni Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, akiwa na makamishna wengine wa uhifadhi wafuatilia kwa makini hoja mbalimbali, ikiwemo mafanikio makubwa ya TFS katika usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu na nyuki Mei 19,2025—ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kujenga uchumi shirikishi wa kijani.

Serikali imebainisha mafanikio makubwa katika biashara ya mazao ya misitu na nyuki nchini, ikiwemo ongezeko la uzalishaji, viwanda na mauzo nje ya nchi, ikiwa ni matokeo ya uwekezaji wa kimkakati unaofanywa kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Akizungumza leo Mei 19, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati wa kuwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana alisema kuwa ndani ya miaka mitano, sekta hizo mbili zimeonyesha ushahidi wa wazi wa kuimarika kwa msingi wa uchumi wa kijani nchini.

Aliongeza kuwa, katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2024/2025, uzalishaji wa mbao kutoka mashamba ya miti ya Serikali unaolimwa kibiashara umeongezeka kutoka mita za ujazo 1,108,791 hadi 1,264,535, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya 155,000 m³.

Aidha, viwanda vya kati na vikubwa vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao ya misitu vimeongezeka kutoka 636 mwaka 2020 hadi 1,671 mwaka 2025, huku viwanda vidogo vidogo kama vya useremala vikifikia zaidi ya 7,000 kote nchini.

Waziri Chana alisema kuwa thamani ya mauzo ya mazao ya misitu nje ya nchi nayo imepanda kwa kasi, kufikia Shilingi 458.47 bilioni mwaka 2024/2025, kutoka Shilingi 105.68 bilioni mwaka 2020/2021. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 333.8, jambo alilolieleza kuwa ni matokeo ya kuimarika kwa viwango vya usimamizi na ubora wa bidhaa zinazozalishwa.

Katika upande wa nyuki, Serikali imewezesha ujenzi wa viwanda nane (8) vya kati na vikubwa vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao ya nyuki, kutoka kiwanda kimoja (1) mwaka 2020. Viwanda hivyo vimejengwa katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Singida, Iringa, Katavi na Geita.

Mpaka kufikia Aprili 2025, Tanzania imeuza nje ya nchi jumla ya tani 1,321.35 za asali zenye thamani ya Shilingi 15.86 bilioni, ikilinganishwa na tani 430.61 za mwaka 2020/2021 zenye thamani ya Shilingi 5.17 bilioni — ikiwa ni ongezeko la asilimia 206.9.

Kutokana na mafanikio haya, Shirika la Wafugaji Nyuki Duniani limeiteua Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Dunia wa Wafugaji Nyuki (APIMONDIA) utakaofanyika mwaka 2027 na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 4,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani.
“Kuongezeka kwa uzalishaji na thamani ya mauzo ya mazao ya misitu na nyuki ni ushahidi wa mafanikio ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. Tunajenga msingi wa uchumi wa kijani unaozingatia uhifadhi, maendeleo ya viwanda na ajira kwa vijana wetu,” alisisitiza Waziri Chana.

Katika hatua nyingine, Waziri Chana amewakaribisha wabunge wote na wadau wengine wa sekta ya maliasili kushiriki maonesho ya Siku ya Nyuki Duniani ambayo yanaendelea jijini Dodoma, na kufikia kilele chake kesho Mei 20, 2025 katika katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma.


--

Tulizo Henry Kilaga I A Brand Communication Strategist,

Located: Dodoma I Dar es Salaam - Tanzania. 

Call/WhatsApp: +255 765 888887

www.thestrategist.co.tz

RC DKT BATILDA AFUNGUA MAADHIMISHO YA NNE YA SIKU YA KIMATAIFA YA WANAWAKE KATIKA SEKTA YA BAHARI ATOA NENO

May 19, 2025 Add Comment




Na Oscar Assenga,Tanga

kuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk Batilda Burian amesema maendeleo ya Taifa hayawezi kupimwa kwa kiwango cha uwekezaji au ujenzi wa viwanda pekee, bali kwa namna serikali na jamii zinavyoweka fursa za usawa wa kijinsia katika ajira, hususan kwa watoto wa kike na wa kiume.

Dk Burian ameyasema hayo alipokuwa akifungua maadhimisho ya nne ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake katika Sekta ya Bahari yaliyofanyika jijini Tanga  (Jumapili) Mei 18/2025.


Akimnukuu mwanafalsafa maarufu Plato, aliyewahi kusema kuwa "Kilimo cha jamii yoyote ni jinsi inavyowathamini wanawake", Dk Burian alisisitiza kuwa taifa linapaswa kujipangia malengo ya kuhakikisha usawa wa kijinsia unatekelezwa kikamilifu.

"Tusiache mwanamke abaki ufukweni bali tunataka aingie ndani ya bahari," alisema kwa msisitizo..

Alieleza kuwa licha ya juhudi zinazofanywa na serikali na wadau mbalimbali, sekta ya bahari bado inatawaliwa na wanaume, huku takwimu zikionyesha kuwa wanawake wanaofanya kazi katika sekta hiyo ni asilimia 1.2 pekee.

Katika hatua ya kutia moyo, Dk Burian alipongeza Umoja wa Wanawake Wanaofanya Kazi katika Sekta ya Bahari katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (WOMESA) kwa kuanzisha programu ya 'Wakamate Wangali Wadogo' (Catch them Young) inayolenga kuelimisha na kuwahamasisha wanafunzi wa kike kujiunga na fani zinazohusiana na bahari.

Alisisitiza kuwa wanawake ndio uti wa mgongo wa sekta hiyo, akibainisha kuwa juhudi kama hizo zinaunga mkono maono ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuwekeza kwenye elimu ya sayansi kwa watoto wa kike, ikiwemo kuanzishwa kwa shule maalum."

Hapa Tanga, kupitia uwekezaji wa Rais, tumeanzisha shule maalum ya watoto wa kike wilayani Kilindi ambayo imepewa jina la aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Beatrice Shelukindo," alisema.

Dk Burian pia alitoa wito kwa sekta binafsi inayohusika na bahari kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa katika ajira.


"Nifahari yetu Kuwaona Wanawake wa Kitanzania wakiongoza na kushiriki miradi mkubwa ya maendeleo ya bandarini,fukwe zetu wakifundisha kwenye vyuo vya Bahari kama Chuo Cha Bahari Dar es salaam(Dar es salaam Maritime INstute-DMI)kufanya kazi kwenye Meli za kitaifa na Kimataifa Kwa hakika Hawa ni vinara na fahari yetu ni lazima tuwapongeze"alisema Burian.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa WOMESA, Bi Fortunata Kikwaya, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, kwa uwekezaji mkubwa walioufanya katika sekta ya bahari."


Sherehe hizi za nne zinaashiria maono yetu kuwa wanawake si wa kushirikishwa tu, bali ni wadau wakuu katika maendeleo ya sekta hii," alisema.

Bi Kikwaya alitaja mafanikio ya WOMESA kuwa ni pamoja na ongezeko la wanachama kutoka 24 mwaka 2021 hadi kufikia 174 mwaka huu, pamoja na kudhamini mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa wanawake.


Kuhusu mpango wa 'Catch them Young', alisema tayari wametembelea shule 35 na kuanzisha vilabu tisa vya wanafunzi, vitatu kati yake vikiwa jijini Tanga.

Hata hivyo, alieleza kuwepo kwa mwamko mdogo wa wanawake kujiunga na WOMESA pamoja na uelewa mdogo kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya bahari.

Aliiomba Serikali kuanzisha utaratibu wa kutoa ufadhili wa masomo kwa watoto wa kike wanaotaka kusomea taaluma zinazohusiana na sekta ya bahari na kusaidia kuendeleza juhudi za kuwahamasisha kuingia katika sekta hiyo.



Mwisho

MADAKTARI WANAWAKE WA KIISLAM TANZANIA WAZINDUA MFUKO WA KUSAIDIA HUDUMA ZA AFYA KWA WATOTO WENYE UHITAJI

May 19, 2025 Add Comment

 

Katika kuunga mkono falsafa ya UTU NA MAENDELEO inayoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Madaktari Wanawake wa Kiislam nchini wamezindua rasmi Mfuko wa Kusaidia Huduma za Afya kwa Watoto Wenye Uhitaji, unaojulikana kama Muslimah Medical Support Fund (MMSF).

Mfuko huu ni mwendelezo wa juhudi za kujitolea ambazo madaktari hao wamekuwa wakizifanya kwa muda katika utaratibu usio rasmi, ambapo wamekuwa wakisaidia watoto kutoka familia zisizo na uwezo kupata matibabu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwenyekiti wa MMSF Dkt. Asha Omari Mahita alisema kuwa wazo hilo lilianza kupitia mawasiliano ya kawaida katika kundi la WhatsApp, baada ya madaktari kuguswa na mateso ya watoto wanaokosa huduma muhimu za afya kutokana na ukosefu wa rasilimali.

“Kwa mujibu wa maadili ya Uislamu, huduma ya afya ni haki ya msingi kwa kila binadamu. Tumeona ni wajibu wetu kusaidia kundi hili linaloathirika zaidi, kwa kuanzia na watoto, mpaka Sasa tumekwisha wakatia bima za Afya watoto 500 na malipo ya moja kwa moja hospitalini bila kujali ni dini gani” alisisitiza Dkt. Mahita.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Mstaafu, Prof. Mussa J. Assad, aliwapongeza Madaktari hawa Wanawake kwa moyo wao wa kujitolea na kuonyesha mfano bora wa uwajibikaji wa kijamii. Alisisitiza umuhimu wa kutumia uzoefu wa madaktari waliostaafu ili kupanua huduma kwa walengwa zaidi.

“Mfuko huu unaonyesha dira sahihi ya mshikamano wa kitaifa na matendo yenye kugusa maisha ya wengi. Ninafurahishwa na muundo wa MMSF ambao ni himilivu na unaolenga kupanua wigo wa huduma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,” alisema Prof. Assad.

Waanzilishi wa MMSF wamesema wanatarajia kushirikiana na hospitali, taasisi, watubinafsi na wahisani mbalimbali ili kuhakikisha kuwa watoto kutoka familia zisizo na uwezo wanapata huduma za kitabibu zenye ubora bila vikwazo vya kifedha.

Katika malengo mengine Karibu wa MMSF Dr Khadija Ibrahim alisema malengo ya mbeleni ni pamoja na kusaidia ada kwa waschana waliokwana wanotaka kuwa madaktari na pia kuweka Kambi za kitabibu (Medical camp) vijijini.












WAOMBAJI MIKOPO YA ELIMU,TAFUTENI NAMBA ZA NIDA MAPEMA

May 18, 2025 Add Comment


Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Tanga


Ni takwa la kisheria kwa waombaji wa mikopo ya elimu kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuwa na namba ya utambulisho (National Identification Number-NIN) au kitambulisho cha uraia kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili kuweza kuomba mikopo ya elimu.


Pamoja na kwamba takwa hilo la kisheria kwa miaka ya nyuma kwa mwombaji ambaye hakuwa na namba ya utambulisho au kitambulisho cha uraia aliweza kuomba na kupata mkopo, lakini kwa mwaka huu wa masomo wa 2025/2026, bila namba ya utambulisho au kitambulisho cha uraia, mwombaji atashindwa kuomba mkopo na hivyo kukosa mkopo.


Bodi ya Mikopo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa walifanya mkutano Mei 16, 2025 ambapo mkazo juu ya kila mwombaji  wa mkopo wa elimu kuhakikisha ana namba ya utambulisho au kitambulisho cha uraia uliwekwa bayana mbele ya vyombo vya habari na Watanzania kwa ujumla.

Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia alisisitiza juu ya umuhimu wa waombaji kuwa na namba ya NIN. "NIN itaiwezesha HESLB kuwa na taarifa sahihi na za kipekee za kila mwanafunzi. Kwa kutumia NIN kutatuwezesha kuboresha uwezo wetu wa kufuatilia wanufaika waliokopeshwa baada ya kuhitimu. Tumeunganisha mifumo yetu ili kuwezesha kuhakiki taarifa za waombaji mikopo kupitia NIN. Tayari wataalamu wa Tehama kutoka pande zote mbili (HESLB na NIDA) wanashirikiana kuhakikisha mifumo yetu iliyounganishwa inafanya kazi kwa ufanisi," amesema Dk. Kiwia.


Kimsingi, serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikisisitiza mifumo ya serikali kusomana ili kurahisisha utendajikazi na ufuatiliaji kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama). Kabla ya maboresho makubwa yaliyofanywa na HESLB kuhusiana na mifumo ya kidigitali, kulikuwa na changamoto ya kupata taarifa za wanufaika wahitimu ambao hawajarejesha mikopo ambayo ni fedha zilizotumika kuwasomesha elimu ya juu katika taasisi mbalimbali za elimu.


Kwahiyo, maboresho makubwa yamefanyika kwa HESLB kuungana na taasisi nyingine mbalimbali ili kuwa na mfumo wa pamoja ambao utarahisisha utendajikazi na ufuatiliaji. Sambamba na hilo, kwa kuzingatia gharama zilizopo katika elimu ya kati na ya juu yaani ada, chakula, malazi, vitabu, kudurufu matini (kutoa photocopy), mafunzo kwa vitendo; Watanzania wengi wanahitaji kuwezeshwa kifedha kupitia mikopo inayoratibiwa na HESLB.


Hivyo, niwashauri waombaji wa mikopo ambao hadi sasa hawana namba ya NIN kuomba namba hizo kupitia tovuti ya NIDA au kwenda kwenye ofisi za NIDA zilizopo katika Halmashauri na wilaya zao ili kupata namba ili kuweza kuomba mikopo pindi dirisha la maombi ya mikopo litakapofunguliwa rasmi na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kupata mikopo. 


Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, amesema NIDA wapo tayari kuwahudumia waombaji wa mikopo. "Tunafurahia wenzetu wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu wameona na kutambua jitihada zetu, pamoja na mambo mengine watatuunga mkono katika kutoa hamasa hii kwa vijana. Namba ya utambulisho wa Taifa (NIN) inapatikana ndani ya siku 5 baada ya kujisajili, na kadi ya NIDA inapatikana ndani ya siku 21 baada ya uthibitisho wa taarifa za mwombaji, hakikisha unapojisajili unapata kadi," amesema.


Dirisha la maombi ya mikopo linatarajiwa kufunguliwa mwezi Juni, 2025, ni vyema waombaji watarajiwa wasiokuwa na namba ya utambulisho au kitambulisho cha uraia wakaanza kufuatilia mapema badala ya kusubiri hadi muda wa kuomba mkopo ufike ndipo waanze kuhangaika kufuatilia. Ikumbukwe kuwa bila namba ya utambulisho, maombi ya mikopo hayataweza kukamilika. 


"Tunatarajia kufungua dirisha la maombi ya mikopo mwezi Juni, 2025, kwa mwaka wa masomo wa 2025/2026, namba ya utambulisho wa Taifa itakuwa hitaji la lazima katika kujaza fomu za maombi ya mikopo, hivyo waombaji wote wanapaswa kuwa na namba hii wakati wa kujaza maombi yao ya mkopo," alisisitiza Dk. Kiwia.


Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.


Maoni: 0620 800 462.