NIMEPIGA KURA NIMETIMIZA HAKI YANGU YA KIKATIBA-MHE KAPINGA
siasa📌 *Aungana na Wananchi kuchagua Viongozi Kitongoji cha Mheza*
📌 *Ahimiza Watanzania kuendelea kujitokeza kupiga kura*
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga leo ameshiriki zoezi la kupiga
kura katika Kitongoji cha Mheza kijiji cha Mkumbi Halmashauri ya Mbinga Vijijini ili kuchagua viongozi wa eneo husika.
Kapinga ameeleza kuwa, kwa kufanya hivyo ametimiza haki yake ya kikatiba na kutoa wito kwa Watanzania wote kuitumia haki hiyo kikamilifu.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni miongoni mwa mihimili muhimu ya Demokrasia inayowezesha ushiriki wa wananchi katika uongozi wa maeneo yao.
![]() |
NLD YAHIMITISHA KAMPENI KWA KISHINDO HANDENI YAWAOMBA WANANCHI KUWAPA RIDHAA WAGOMBEA WAO ILI WAWAPE MAENDELEO
siasaCHAMA cha The National League For Democracy (NLD) kimehitimisha kampeni kwa wagombea ambao wanawania nafasi za uongozi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu huku wakiwawataka wananchi kuwapa ridhaa ili waweze kuwapa maendeleo.
Akizungumza wakati wa mkutano wa kampeni wa kuhitimisha kampeni hizo katika viwanja vya soko la Misima wilayani Handeni,Katibu Mkuu wa NLD Doyo Hassani Doyo alisema kwamba chama hicho kimejipanga kuhakikisha wanatatua kero za wananchi zinazowakabili kwa muda mrefu.
Alisema kwamba wagombea ambao wamewasimamisha kwenye maeneo yote wanauwezo mkubwa wa kuweza kuwatumikia wananchi na kuwasaidia kutatua changamoto ambazo zinawakabili kutokana na kwamba wanatosha na uwezo wa kuwaongoza.
“Sisi katika uchaguzi huu tumewasimamisha wagombea wasiokuwa na njaa lakini pia wenye uwezo wa kutoa ajira kwa wengine kupitia fursa tulizonazo na wengi wametoa ajira kwenye jamii zinazowazunguka”Alisema
Awali akizungumza Mwenyekiti wa NLD wilaya ya Handeni Rajabu Doyo aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kufanya uchunguzi haraka iwezekanavyo kwa baadhi ya wagombea wa vyama vya siasa kuandika barua za kujitoa kwenye uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa.
“Haiwezekani mgombea anachukua fomu ya kugombea anaijaza halafu akairudisha alafu leo unaambiwa kajitoa hii ni rushwa ya wazi wazi kabisa kwa hiyo tunaiomba Takukuru iingilie kati haraka iwezekanavyo “Alisema
Mwisho.
HATUNA HURUMA TUNABEBA VYOTE -DKT.BITEKO
siasa📌 *Tunataka Tuoneshe Afrika na Dunia Tanzania ni Nchi ya Demokrasia*
📌 *Asema CCM Imejipanga Kushinda na Kuleta Maendeleo*
📌 *Asema CCM Inataka Ushindi wa Heshima*
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa CCM chini ya uongozi wa Rais Samia imejipanga kuifanya Geita kuwa na maendeleo zaidi na katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaofanyika Novemba 27, 2024 wananchi waichague CCM na kuipa ushindi wa heshima.
Ametolea mfano wa jitihada za kuiletea maendeleo zilizofanywa na CCM kuwa ni pamoja na juhudi za Rais Samia za kuhakikisha Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) unawanufaisha zaidi wananchi kwa Geita.
Dkt. Biteko amesema hayo Novemba 24, 2024 wakati akihutubia katika Kampeni zinazoendelea za
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Wilaya ya Geita zilizofanyika katika Viwanja vya Nyankumbu mkoani Geita.
“ Sasa tunaona miradi mbalimbali ikitekelezwa, Geita maendeleo yapo kila kona tunataka mchague viongozi watakaoshirikiana na viongozi wengine ili kutuletea maendeleo, CCM tunataka ushindi wa heshima,” amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza “ Kwetu sisi hivi ni vyama rafiki na Mhe. Rais anaeleza kuhusu falsafa ya 4R, tunataka tuiambie Afrika na dunia kuwa Tanzania ni nchi ya demokrasia na tunafuata misingi ya waasisi wetu na sisi Geita hatuta wabagua vyama vingine lakini jambo moja hatuna huruma nalo ni kura na hatuwapi kura hata moja,”
Ameongeza “ CCM tunabeba vyote, tunabeba vijiji, vitongiji na mitaa yote hatuwaachi hata kimoja na tunafanya hivyo kwa sababu wananchi wameridhishwa na kazi kubwa ya miradi ambayo CCM imetekeleza hapa na inaendelea kutekeleza.”
Aidha, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imefanya jitihada kubwa za kuhakikisha Tanzania inaendelea kuimarika kiuchumi kwa kuanzisha miradi ya umeme ambayo imeongeza utoshelevu wa umeme nchini pamoja na uwepo wa treni ya umeme ambayo imeanza safari zake kutoka Dar es salaam hadi Dodoma na inatarajiwa kufika Burundi hapo baadae.
Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Mhe. Constantine Kanyasu amesema kuwa Wilaya ya Geita imejipanga kushinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuwa wananchi wameona miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo.
Vilevile, Kanyasu ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya afya, elimu na barabara ambayo inaendelea vizuri.
Mbunge wa Jimbo la Busanda, Mhe. Tumaini Magesa amewahimiza wananchi wa Geita kuwapigia kura wagombea wa CCM kwa kuwa Serikali ya Rais Samia ina nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Geita, Muhoja Mapande amesema kuwa wilaya yake ina vijiji 158, mitaa 65 ambapo vyama vingine vimeweka wagombea 50 na nane kati yao hawataendelea kugombea, katika vitongoji 640 vyama vingine vimeweka wagombea 115 ambapo 92 kati yao wameandika barua ya kutoaendelea na vyama hivyo.
Ameendelea kusema wagombea wa vyama hivyo wamefikia uamuzi huo baada ya kuona jitihada za CCM za kuleta maendeleo katika wilaya hiyo.
MWISHO
TWENDE NA KASI YA DUNIA UBUNIFU NA UJASIRIAMALI-BALOZI NCHIMBI
siasa
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amewataka wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe kuendelea kuwa viongozi wa mabadiliko katika soko la ajira la Tanzania, wakienda sambamba na kasi ya dunia katika maeneo ya ujasiriamali na ubunifu.
Akizungumza katika Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu ya Morogoro, B hialozi Nchimbi amesema ni muhimu kwa vyuo vya elimu ya juu na wahitimu wake kuzingatia kasi ya mabadiliko ya dunia katika maeneo ya ubunifu, ujasiriamali, na uongozi ili kuleta mapinduzi makubwa katika kutengeneza fursa za ajira nchini.
Kupitia mkutano wa baraza hilo uliofanyika leo tarehe 23 Novemba 2024, ukiwa na kauli mbiu isemayo “Kuwawezesha wanafunzi kufanya mapinduzi katika soko la ajira na kuchochea upeo mpya wa fursa za kazi,” Balozi Nchimbi amesisitiza kuwa mapinduzi hayo, mbali ya kusaidia kutengeneza fursa za ajira, kujiajiri na kuajiriwa, pia yatakuwa sehemu ya misingi ya kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi nchini.
“Maendeleo ya teknolojia, masuala ya akili bandia, na uchumi wa kijani vimekuwa vichocheo vikubwa vya mabadiliko duniani. Sisi Watanzania, kipekee wahitimu wetu, wanapaswa kuwa sehemu ya mabadiliko hayo kwa ufanisi. Ninatoa wito kuhusu umuhimu wa kutambua umuhimu wa ubunifu katika kutatua changamoto, kwa kuzingatia maslahi ya taifa,” amesema Balozi Nchimbi.
Alisema kuwa dunia inabadilika haraka, hivyo ni muhimu kwa wahitimu kuchukua fursa hizo ili kuleta maendeleo endelevu, huku akiwasisitiza kutumia elimu waliyoipata chuoni hapo, kuwa sehemu ya kutafuta njia za kuboresha masoko ya ajira kupitia matumizi ya teknolojia na ubunifu, na kushiriki kwa dhati katika mchakato wa maendeleo.
Katika hotuba yake, Balozi Nchimbi alisisitiza kuwa Serikali ya CCM, chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kutengeneza fursa za ajira na maendeleo ya vijana, kwa sababu kundi hilo ni nguzo muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.
Aidha, alisisitiza kuwa sekta ya ujasiriamali, ni mojawapo ya sekta zitakazosaidia kufungua fursa za ajira na kukuza viwanda na biashara mpya nchini. Aliwahimiza wahitimu kuwa na mtazamo wa kimataifa na kuona changamoto kama fursa za ubunifu na maendeleo.
Balozi Nchimbi pia alizungumza kuhusu umuhimu wa usawa wa kijinsia katika maendeleo ya taifa. Alisema kuwa serikali inajitahidi kuhakikisha kuwa wanawake na wanaume wanapata fursa sawa katika sekta zote, na aliwahimiza wahitimu wa kike na wa kiume kujitahidi kutimiza malengo yao kwa usawa na kushirikiana kwa pamoja katika kuleta maendeleo.
Balozi Nchimbi pia alitoa wito kuhusu umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa wahitimu, wakijifunza kwa watangulizi wao, hasa katika kuunda mitandao ya kijamii itakayosaidia kubadilishana uzoefu na kuendelea kujifunza masuala mapya, ikiwemo mbinu za kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
#Ends