Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Mwenge wa Uhuru kiongozi wa vijana sita watakaokimbiza Mwenge huo,Charles Kabeho wakati alipozindua mbio za Mwenge wa Uhuru kwenye uwanja wa Magogo mjini Geita, Aprili 2, 2018. Wapili kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwansha Mwenge wa Uhuru kuzindua mbio zake kwenye uwanja wa Magogo mjini Geita, Aprili 2, 2018 Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Kiongozi wa wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Charles Kabeho wakati alipozindua mbio za Mwenge wa Uhuru kwenye uwanja wa Magogo mjini Geita Aprili 2, 2018
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua mbio za Mwenge wa Uhuru kwenye uwanja wa Magogo mjini Geita, Aprili 2, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama akizungumza katika sherehe za kuzindua mbio za Mwenge wa Uhuru kwenye uwanja wa Magogo mjini Geita, Aprili 2, 2018. Mgeni rasmi katika sherehe hizo alikuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Zanzibar, Balozi Ali Karume akizungumza katika sherehe za kuzindua mbio za Mwenge wa Uhuru kwenye uwanja wa Magogo mjini Geita, Aprili 2, 2018. Mgeni rasmi katika sherehe hizo alikuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (wapili kulia) wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel wakati alipotoa salamu za mkoa huo katika sherehe za kuzindua mbio za Mwenge wa Uhuru kwenye uwanja wa Magogo mjini Geita Aprili 2, 2018.
Watoto wakionyesha halaiki katika sherehe za kuzindua mbio za Mwenge wa Uhuru zilizoongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye uwanja wa Magogo mjini Geita, Aprili 2, 2018.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
………………
*Ataja mikoa saba inayoongoza kwa utoro wa wanafunzi shuleni
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa mikoa ya Tabora, Geita, Mtwara na Shinyanga ambayo inaongoza kwa utoro wa wanafunzi kwa shule za sekondari wahamasishe umuhimu wa elimu na mahudhurio endelevu shuleni.
“Kwa ujumla utoro wa wanafunzi wa Sekondari ni mkubwa zaidi kwa Mikoa husika kuliko shule za msingi. Nitumie nafasi hii kuikumbusha Mikoa niliyoitaja kuhamasisha wananchi wakiwemo wazazi, walezi na wanafunzi wenyewe kuhusu umuhimu wa elimu na mahudhurio shuleni.”
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Aprili 02, 2018) wakati akizindua mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2018 katika uwanja wa Magogo mkoani Geita. Kaulimbiu ya mbio za mwenge kwa mwaka huu ni ‘Elimu ni ufunguo wa maisha, wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu.’
Waziri Mkuu amesema dhamira ya Serikali kupitia kaulimbiu hiyo ni kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kuwekeza katika elimu na kuzalisha rasilimali watu yenye ujuzi na stadi zitakazowezesha kuchochea mapinduzi ya viwanda ili nchi iwe ya uchumi wa kati ifikapo 2025.
Akizungumzia kuhusu utoro kwa shule za sekondari nchini, Waziri Mkuu amesema mkoa wa Tabora ndio unaongoza kwa utoro kwa kuwa na silimia 9.7,
Geita asilimia 8.1, Mtwara asilimia 6.4 na Shinyanga asilimia 6.3.
Kuhusu utoro wa wanafunzi wa shule za Msingi nchini, Waziri Mkuu amesema mkoa unaoongoza ni wa Rukwa kwa asilimia 3.2, Geita asilimia 3.1, Tabora asilimia 2.9, Simiyu asilimia 2.0 na Singida asilimia1.9.
Amesema mikoa yenye kiwango kikubwa cha utoro wa wanafunzi na kuacha shule ihakikishe mahudhurio yanadhibitiwa shuleni ili kuhakikisha wanafunzi wote wanaoandikishwa wanahudhuria, wanasoma na kuhitimu ngazi husika.
“Ukitaka kuleta maendeleo ya uchumi ulio imara, ukitaka kujenga jamii inayo heshimu na kufuata misingi ya uwajibikaji na ubunifu, ukitaka kujenga Taifa lenye amani na utulivu, lazima uwekeze zaidi katika elimu”.
“Kwa hiyo, uwekezaji katika elimu haumaanishi tu kuhakikisha watoto wetu na Watanzania kwa jumla wanapata haki yao ya msingi bali ni kuweka misingi imara itakayo liwezesha Taifa na mtu binafsi kufikia hatua bora ya maisha”.
Waziri Mkuu amesema ili kuhakikisha Taifa linafikia viwango bora vya elimu, Serikali ya awamu ya tano inyoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, imedhamilia kuboresha elimu katika ngazi zote nchini, kuanzia Elimu ya Awali hadi Elimu ya Juu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zitaendelea kuhimiza mapambano dhidi ya rushwa kwa sababu bado ipo na inaendelea kuwa ni adui wa haki na kudhoofisha jitihada za Serikali za kuimarisha uchumi, kuimarisha huduma za jamii na Utawala bora.
Amesema athari zinazotokana na vitendo vya rushwa huwaathiri watu wa kawaida zaidi na kuendelea kubaki wanyonge katika jamii, hivyo Serikali itaendelea kupambana na vitendo vya rushwa bila kuchoka mpaka jamii itakapoachana na vitendo hivyo vya kidhalimu.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bibi Jenista Mhagama alisema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa umbali wa takribani kilomita 103,440.7 kwa siku 195 katika mikoa yote 31 nchini na halmashauri za wilaya 195.
Alisema kazi hiyo itafanywa na vijana sita kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ambao wameandaliwa kikamilifu ili kuhakikisha wanaendelea kuwakumbusha Watanzania historia ya falsafa ya Mwenge wa Uhuru, kufikisha kwa ufasaha ujumbe wa mwaka huu na kukagua na kuzindua miradi yamaendeleo kwa umakini.
Bibi Jenista alisema mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 zinaongozwa na Bw. Charles Kabeho kutoka mkoa wa Dar es Salaam akishirikiana na Bw. Issa Abasi Mohamed (Kusini Pemba), Bi. gusta Safari (Geita), Bw. Ipyana Mlilo (Tanga), Bw. Dominick Njunwa (Kigoma) na Bi. Riziki Hassan Ali (Kusini Unguja).
Naye, Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi Ali Abeid Karume alisema atahakikisha ujumbe wa Mwenge wa Uhuru unawafikia wananchi wote pamoja na kupita katika miradi yote ya maendeleo iliyopangwa.
Balozi Karume ametumia fursa hiyo kuwapongeza Rais Dkt. Magufuli pamoja na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein kwa jitihada zao za kudumisha amani, utulivu, kuwaletea wananchi maendeleo bila ya ubaguzi pamoja na kupambana na maadui wanaotaka kudhoofisha maendeleo nchini.