Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi akikabidhi vitanda kwa ajili ya kituo hicho
Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi akikabidhi gari la kubebea wagonjwa kwa ajili ya kituo hicho
NA FREDY MGUNDA, MUFINDI
MBUNGE wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi ametoa msaada wa vitanda kumi kwa kituo cha afya cha Ihongole kilichokuwa kinakabiliwa na upungufu wa vitanda katika wodi ya wazazi.
Akizungumza wakati kukabidhi vitanda hivyo sambamba na kukabidhi gari ndogo ya kubebea wagonjwa iliyotolewa na serikali, Chumi alisema kuwa msaada huo wa vitanda utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto katika kituo hicho cha afya ambacho kinachohudumia wakazi zaidi ya 20000 wa jimbo la Mafinga mjini.
Alisema kuwa ushirikiano katika kuondoa changamoto na kuchukulia mapungufu ndio njia pekee ya kuendelea kuinyanyua Mafinga hasa katika sekta ya afya ambayo imekuwa ikikabiliana na changomoto nyingi.
Chumi alisema kuwa msaada wa vitanda vimetolewa na mmoja wa wahisani wanaolisaidia jimbo la Mafinga kuondokana na changamoto mbalimbali katika sekta ya afya ambayo imekuwa na ikikabiliwa na mapungufu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa miundo mbinu bora.
Alisema changamoto za sekta ya afya katika jimbo hilo na wilaya ya Mufindi kwa ujumla zitakashughulikiwa kupitia serikali na wadau wake mbalimbali wanaotakiwa kujitokeza kuboresha huduma zake
Akizungumzia Gari hiyo ambayo imetolewa na Serikali Chumi alisema kuwa itatumika kubeba wagonjwa ambao watalazimika kukimbizwa kwenye Hospitali ya Mafinga ambapo awali ilikuwa vigumu kwa wagonjwa pindi wakizidiwa kwenda kutibiwa.
Mbali na msaada huo, mbunge huyo ambaye mbali na ahadi mbalimbali kwa wapiga kura wake, aliahidi kuboresha huduma za afya katika jimbo hilo amekwishatoa msaada vitanda, magodoro, viti vya kubeba wagonjwa na vifaa tiba mbalimbali katika hospitali ya Mafinga.
Akipokea na kushukuru kwa msaada huo, Kaimu Mganga Mkuu wa kituo cha Ihongole, Bernad Makupa alisema msaada huo wa vitanda na gari ya kubebea wagonjwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kuwahudumia wananchi katika vijiji mbalimbali vinavyopata huduma katika kituo hicho
Kwa niaba ya halmashauri ya Mafinga Mjini, mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Charles Makoga alimshukuru Chumi kwa ushiriki wake katika kuchangia maendeleo ya wananchi wa jimbo hilo kabla na baada ya kuingia madarakani na akamuomba endelee na moyo huo.