Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu
(watu wenye Ulemavu) Mhe. Stella Ikupa akitoa maelezo kuhusu masuala ya
watu wenye ulemavu kwa Kamati ya Kudumu ya Katiba na Sheria ili
kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa
mwaka 2017/18 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2018/19 Kwa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Machi 28, 2018 Bungeni
Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.Jenista
Mhagama akifafanua jambo wakati kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Katiba na Sheria Machi 28, 2018 Bungeni Dodoma.
Baadhi ya Wajumbe wa kikao
wakifuatilia mada zinazowasilishwa wakati wa Taarifa ya Utekelezaji wa
Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2017/18 na Makadirio ya Mapato
na Matumizi kwa mwaka 2018/19 Kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na
Sheria Machi 28, 2018 Bungeni Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Katiba na Sheria Mhe.Najma Giga akiongoza kikao cha kamati yake wakati
wa Uwasilishaji wa Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri
Mkuu kwa mwaka 2017/18 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka
2018/19 kwa mafungu 27,62,65 na 15 ya Ofisi hiyo.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Mhe. Antony Mavunde akitoa hoja wakati wa Kikao cha Kamati hiyo.
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Kailima Ramadhan akifafanua jambo wakati wa kikao cha kamati hiyo.
Baadhi ya Wajumbe wa kikao wakifuatilia mada zinazowasilishwa wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU – DODOMA)
…………………………………………………………………………………….
Na.MWANDISHI WETU
Serikali imedhamiria kuboresha
mazingira ya watu wenye ulemavu ili kuwasaidia kujikwamua katika nyanja
zote na kuchangia katika maendeleo nchini.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu
Mhe.Stella Ikupa wakati wa Uwasilishaji wa Taarifa ya Utekelezaji wa
Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2017/2018 na Makadirio ya
Mapato na Matumizi kwa mwaka 2018/2019 kwa mafungu ya Taasisi
zinazosimamiwa na Ofisi hiyo Mjini Dodoma.
Waziri Ikupa alieleza kuwa tayari
Serikali imeanza mikakati ya kuboresha mazingira ya watu wenye Ulemavu
kwa kuvifufua vyuo na vituo vyao ili kuwapa nafasi nzuri ya kujifunza
katika mazingira yanayowapa uhuru na tija kulingana na aina za ulemavu
walionao.
“Tayari tumeanza kuboresha
mazingira ya vyuo vya ufundi ikiwemo kile cha Yombo kilichopo Mjini Dar
es Salaam na Sabasaba ili kusaidia kuwapa fursa za kujifunza katika
mazingira rafiki hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuna kuwa na vifaa
vya kutosha”.Aliongezea
Sambamba na hilo Serikali
inaendelea na hatua za kuboresha mazingira ya Watu wenye ulemavu kwa
kuwajengea uwezo, kuongeza wataalam wa kuwafundisha, kuwapa mafunzo
maalumu yenye kuleta tija pamoja na kuwashirikisha katika fursa za
maendeleo.
Aliongezea kuwa Ofisi yake
itaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja
na vyuo mbalimbali ili kupata taarifa sahihi za mahitaji halisi ya watu
wenye ulemavu yatakayosaidia kuwa na kanzidata ya kudumu yenye taarifa
hizo.
“Jitihada zilizopo ni pamoja na
kushirikisha Wizara ya Elimu ili kuweza kupata taarifa muhimu za watu
wenye ulemavu zitazosaidia kuwa na kanzi data ya uhakika
inayowatambulisha kwa idadi, aina ya ulemavu na ujuzi alionao ili kuwapa
nafasi wenye sifa za kushiriki katika programu za kukuza
ajira”.Alisisitiza Mhe.Ikupa
Kwa upande wake mmoja wa wajumbe
wa Kamati hiyo Mhe.Amina Mollel alishauri kuwe na mikakati madhubuti
yenye tija kwa watu wenye ulemavu ikiwemo kutoa semina kwa watumishi wa
serikali juu ya namna bora ya kuwahudumia watu wenye ulemavu kwa
kuzingatia mahitaji yao.
“Ifike mahali kuwe na mikakati
madhubuti ya kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum hususani kwa
kuwajengea uwezo watumishi kujua namna nzuri ya kuwahudumia watu wenye
ulemavu pamoja na kusaidia kuzikabili changamoto wanazokabiliana
nazo”.Alisema Mhe.Mollel.