Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela (wa pili kushoto) pamoja na viongozi wa Benki ya NMB wakifungua rasmi tawi jipya la Benki ya NMB Pamba wilayani Nyamagana mkoani Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela akizungumza kwenye afla ya uzinduzi wa tawi jipya la Benki ya NMB Pamba wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.
BENKI ya NMB imetoa msaada wa vitanda 11 vikiwa na magodoro na mashuka yake katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana (Butimba) wenye thamani ya Sh Milioni 10 kwa ajili ya akinamama wajawazito na hivyo kupunguza adha ya kukosa malazi.
Msaada huo ulitolewa na uongozi wa benki hiyo mara baada ya kukamilika kwa hafla ya uzinduzi wa tawi jipya la NMB Pamba katika wilaya ya Nyamagana jijini hapa. Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa NMB kanda ya ziwa- Abraham Augustino, alisema msaada huo ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja.
“Ni utaratibu wa kawaida kwa benki yetu kutoa sehemu ya faida yake kwa ajili ya kuwasaidia wananchi ili nao waweze kunufaika, na kuona umuhimu wa kuwepo kwa NMB katika maeneo yao,” alisema.
Naye Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongela aliishukuru benki hiyo kwa kuhakikisha kuwa inatoa sehemu ya faida yake katika kuisaidia jamii, hususani kwa kutoa msaada wa vitanda hivyo katika hosipitali ya wilaya ya Nyamagana ( Butimba)
Aliipongeza benki hiyo kwa kusogeza huduma za kibenki karibu kwa wananchi, kwa kufungua matawi 32 kwa mikoa ya Kanda ya ziwa na kufanya sasa kuwa na jumla ya matawi 211 kwa nchi nzima.
Alisema serikali inaipongeza benki hiyo kwa hatua hiyo nzuri waliyofikia kwa kusogeza huduma za kibenki karibu na wananchi na kunapunguza umbali na imeongeza idadi ya Watanzania wanaopata huduma hizo ambao kwa sasa hawafiki asilimia 20 kwa nchi nzima. Aliwataka wakazi wa mkoa wa Mwanza kujiunga na kuitumia benki hiyo ili waweze kuwa na mfumo mzuri wa kuhifadhi fedha utakaowawezesha kupata mikopo kwa ajili ya ustawi wa maisha yao.
“Sasa muache tabia ya kuweka fedha nyumbani huduma imekwishaletwa karibu, wekeni fedha zenu benki na hii itasaidia kupunguza kesi za kuvamiwa na kuporwa fedha” alisema.
Alisema kuwa, serikali ya awamu ya tano imeweka mikakati mizuri ya kupunguza umaskini kwa wananchi wake kwa kutumia fursa zilizopo, na kuwa ndiyo maana imekuwa ikiunga mkono jitihada zinazofanywa na wadau mbalimbali wa maendeleo, zikiwamo taasisi za fedha ikiwemo benki hiyo.
Aliipongeza benki hiyo kwa kuendelea kubuni huduma mpya na kufungua matawi mapya kwa lengo la kuhakikisha huduma zinakuwa karibu na wananchi, ili kuwaondolea adha ya kufuata huduma hizo mbali na makazi yao.
“Napenda kuwapa changamoto kwa ajili ya kusaidia kuendeleza na kukuza uchumi na ajira kwa wananchi, kwa kuendelea kutoa mikopo kwa wakazi wa vitongoji vyote vya mkoa wa Mwanza” alisema.
Alisema kuwa, kuwapo kwa huduma za kibenki ni kichocheo madhubuti cha maendeleo ya uchumi, maana sekta ya fedha ndiyo inawezesha shughuli zote za uchumi kama kuwekeza, malipo ya kibiashara na ya binafsi, kuweka amana na mikopo binafsi na ya biashara.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Mikopo wa Benki hiyo, Tom Borghols alisema kuwa jiji la Mwanza ni jiji linaloendelea kukua kiuchumi, hivyo linahitaji upanuzi wa huduma za kifedha, na ndiyo maana wamekubali maombi ya wananchi ya kuongezewa tawi jingine la benki.
“Kufunguliwa kwa tawi hili la NMB Pamba litasaidia kuokoa muda ambao wananchi wamekuwa wakiupoteza kwa kukaa benki kwa muda mrefu kusubiria huduma” alisema.
Aidha, alisema kuwa, mbali na kufungua matawi katika maeneo mbalimbali, NMB inazidi kuanzisha huduma mbadala ikiwamo kuweka mawakala, ili kuwezesha kuwa karibu zaidi na wateja, na kwa sasa ina jumla ya mawakala 3,800 nchi nzima.
“Tulikuwa na matawi 210 tukiongeza na hili yametimia 211, mawakala wameongezeka sasa ni zaidi ya 3,800, lakini pia tuna mashine za kutolea fedha (ATM) zaidi ya 700 nchi nzima, na tutaendelea kuboresha huduma zaidi kwa ajili ya wateja wetu” alifafanua.
Afisa Mkuu wa Mikopo wa Benki ya NMB, Tom Borghols (aliyesimama) akizungumza katika uzinduzi wa tawi jipya la NMB Pamba katika wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.
Burudani za ngoma zikiendelea kwenye uzinduzi wa tawi jipya la Benki ya NMB Pamba wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.
Sehemu ya wananchi wakishughudia uzinduzi huo wa tawi jipya la Benki ya NMB Pamba wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.
___________________________________________________________________________________
Joachim Mushi, Mwenyekiti wa Tanzania Bloggers Network (TBN) na Mhariri Mkuu wa Thehabari.com.
Mail address:- mushi@thehabari.com/ jomushi79@yahoo.com/ info@thehabari.com
Mobile:- 0717 030066 / 0756 469470
Web:- www.thehabari.com
EmoticonEmoticon