Na Jonas Kamaleki- MAELEZO.
Viongozi wa Dini wanajiandaa kumpa
tuzo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William
Lukuvi kwa utendaji mzuri uliojaa ubunifu na uwajibikaji.
Hayo yameelezwa katika mahojiano
maalum jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya
Maadili na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Dini zote Tanzania, Askofu
William Mwamalanga.
Askofu Mwamalanga amesema kuwa
Waziri Lukuvi amekuwa kiongozi imara katika kufuatilia masuala
yanayohusu ardhi ikiwemo utatuzi wa migogoro ambayo imedumu kwa muda
mrefu.
“Lukuvi ameing’arisha Serikali ya
Awamu ya Tano kwa kuendana na kasi ya Rais John Pombe Magufuli, hakika
amevaa viatu vya Magufuli, hivyo tumeamua kumpa tuzo maalum kwa ajili
utendaji wake”, alisema Askofu Mwamalanga.
Ameeleza kuwa Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi imefanya jambo zuri kwa kutoa elimu ya
ardhi kiasi kwamba karibu kila mtu amefahamu matumizi ya ardhi na
umuhimu wake.
Askofu Mwamalanga amesema kuwa ardhi imefanywa kuwa lulu na kufanya sura mpya ya ardhi kuonekana ambapo takriban asilimia 85 ya Watanzania wameiona kuwa ni mali.
Mhe. Lukuvi amewapa nafasi ya
kwanza wananchi kuliko Sheria jambo ambalo limewafanya Watanzania
kujisikia kuwa wanathaminiwa na Serikali yao, aliongeza Askofu
Mwamalanga.
Kiongozi huyo wa Dini amesema kuwa
Mhe. Lukuvi ni mfano wa kuigwa na mawaziri na viongozi wenzake kwa
uchapakazi wake. Amesema kuwa ni Waziri ambaye anawashirikisha watendaji
waliochini yake katika maamuzi mbali mbali, hivyo anastahili kupewa
tuzo.
“Tumepanga kumpa tuzo Waziri
Lukuvi kwa kuzingatia yafuatayo: Kuiweka ardhi mikononi mwa watanzania,
kuonyesha kuwa ardhi ni chanzo kikuu cha uchumi wa watu na utatuzi wa
migogoro ya ardhi hasa iliyodumu kwa muda mrefu”, alisema Askofu
Mwamalanga.
Migogoro hiyo ni kama vile mgogoro
wa kijiji cha Mabwegere, Mkoani Morogoro, mgogoro wa Chasimba, jijini
Dar es Salaam na migogoro mingine mingi katika mikoa ya Arusha, Mbeya,
Kigoma, Tanga na Mwanza.
Askofu Mwamalanga amesema Kamati
yake imewasiliana na Taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi ili watoe
mapendekezo ya tuzo ambayo anastahili kupewa Mhe. Lukuvi kwa utendaji
kazi wake mzuri.
Amezitaja baadhi ya Taasisi hizo
kuwa ni Vyuo Vikuu vya Umma na Binafsi, Marais wastaafu na mawaziri
wakuu wastaafu, Vyama vyote vya siasa ambavyo kwa ujumla wake
vimeonyesha kutambua mchango wa waziri Lukuvi.
Baada ya kupokea mapendekezo na
kuyafanyia kazi ndipo itatangazwa siku ya kutoa tuzo hiyo kwa Mhe.
Lukuvi, alisema Askofu Mwamalanga.
Tangu Waziri Lukuvi aiongoze Wizara ya ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mwisho mwa uongozi wa awamu ya Nne hadi sasa,
mabadiliko yenye tija katika
wizara hiyo yameonekana. Migogoro mingi ya ardhi imetatuliwa, utoaji wa
hati za viwanja umerahisishwa na huduma kwa wateja imeboreshwa.
EmoticonEmoticon