CUF YA MAALIM SEIF YAZINDUA OFISI MAGOMENI JIJINI DAR ES SALAAM

June 04, 2017
Suleiman Msuya

IKIWA ni takribani miezi 10 sasa kwa Chama cha Wananchi (CUF), upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad kuvamiwa katika Ofisi Kuu za Bugurunina kundi la Profesa Ibrahim Lipumba chama hicho kimezindua ofisi mpya za chama hicho katika eneo la Mtaa wa Idrisa, Kata ya Mzimuni, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Aidha, Seif amesisitiza kuwa hatarajii kukutana na  Profesa Lipumba kwa kile alichodai kuwa hatambuliki katika chama na hana  sifa hizo kwa sasa.

Akizindua ofisi hiyo ambayo lengo kubwa ni kwa ajili ya wabunge 40 wa CUF, Seif alisema  uamuzi wa wabunge hao kumpatia ofisi ya kufanyia kazi hapo ni cha kiungwana na kinahitajika kuungwa mkono na wanachama wote.

Alisema kwa muda wa miezi 10 sasa wamekuwa wakishindwa kufanya kazi hasa upande wa Tanzania Bara jambo ambalo limewaathiri sana hivyo kupatiwa ofisi kutamsaidia kutimiza majukumu yake vilivyo bila hofu yoyote.

Maalim Seif alisema kukosa ofisi kumewaathiri sana katika baadhi ya mambo hivyo anaamini kwa sasa akifikia Dar es Salaam anamahali pa kukutana na wakurugenzi wake.

“Nimekuwa ni kija hapa nakosa sehemu ya kukutana na wakurugenzi, viongozi mbalimbali wanachama ila hiki ambacho wabunge wamefanya ni cha kuungwa mkono sijawahi kufanya kazi na wabunge wanao kipenda chama kama kipindi hiki,” alisema.

Katibu huyo alisema atahakikisha kuwa anaanza kazi haraka iwezekanavyo kwa kukutana na wakurugenzi wake ili waweze kutekeleza majukumu ya chama.

“Hakuna shaka kuwa hu u unaoitwa mgogoro umeturudisha nyuma sana hivyo naamini wakati wa kufanyakazi umerejea na hawa wabaya wetu hawata ambulia kitu kwani CUF ni  chama imara hakitikisiki,” alisema.

Maalim Seif alisema jitihada zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukimaliza chama ni kubwa lakini hawataweza kufikia lengo hilo kutokana na misingi ya chama hicho.

Alisema kwa sasaa atafanya kazi katika ofisi hiyo ambayo amepewa na wabunge hadi hapo muafaka wa ofisi kuu Buguruni utakapopatikana huku akisisitiza kuwa haki haipotei ila inachelewa.

Katibu huyo alisema anaimani na   mahakama kuwa ita wapatia haki stahiki hivyo kuwataka wanachama kuendelea kuwa na subira.

Aidha, alisema kupitia mgogoro huo hadi sasa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini inashikilia zaidi ya sh. bilioni 1.2 ambazo ni ruzuku ya chamahicho.

Maalim Seif alisema fedha hizo ni pamoja na zile ambazo ofisi ya msajili ilimpatia Lipumba hivyo waamini mgogoro ukiisha wata pata haki yao.

Kwa upande mwingine Katibu huyo alisema hana mpango wa kukutana naLipumba kuhusu mgogoro unaondelea ndani ya chama hicho kwa kile alichodai kuwa si kiongozi wala mwanachama wa chama hicho.

Alisema CUF haimtambui Lipumba kwa sifa yoyote tofauti na kumfukuza uanachama hivyo yeye hawezi kukukutana na mtu  kamahuyo.

Maalim Seif alisema pamoja na kuwa hawamtambui Lipumba kama kiongozi au mwanachama ila akiomba msamaha wapo tayari kumsamehe.

Akizungumza baada ya kuzinduliwa ofisi hizo Mbunge wa Viti Maalum na Kiongozi wa Wabunge wa CUF bungeni, Riziki Ngwali alisema wamelazimika kufungua ofisi nyingine ili wapate mahali pa kukutana wakiwa nje ya Bunge.

Ngwali alisema kupitia ofisi hiyo wataweza kujadiliana mambo mbalimbali yanayo wahusu wabunge na wananchi na kuja na ufumbuzi.

Kwa upande wake Mbunge wa Temeke CUF, Abdallah Mtolea alisema katika ofisi hiyo wanatarajia kuajiri wataalam mbalimbali ambao watasaidia kufanya tafiti na kupitia tarifa mbalimbali za Bunge ili kuwarahisishia katika uchangiaji bungeni.


Alisema katika ofisi hizo wameingia mkataba wa kulipa sh. milioni 18 kwa mwaka ambazo zitatolewa na wabunge wenyewe kwa maslahi ya chama chao.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »