Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira Mh. January Makamba akizungumza na Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi
ya Ngorongoro mara baada ya kutembelea eneo hilo kujionea
changamoto za kimazingira.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira Mh. January Makamba akiongea na Baraza la wafugaji (hawapo
pichani) katika Wilaya ya Ngorongoro. Wafugaji hao walimweleza Waziri
kilio cha muda mrefu cha mradi wa Josho Wilayani hapo, Waziri Makamba
ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Ngorongoro na Baraza la Taifa la Hifadhi
na Usimamizi wa Mazingira kuleta ufumbuzi mapema.
Na Lulu Mussa
Ngorongoro
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais mwenye dhamana
ya usimamizi wa Mazingira nchini Mhe. January Makamba amesema kuwa ni
lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kudhibiti mimea inayohatarisha
uoto wa asili katika Mamlaka ya Ngorongoro.
Katika kutatua changamoto hii, Waziri Makamba ameagiza
kuundwa kwa jopo la wataalamu kutoka Tume ya Sayansi na Tecknolojia,
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Hifadhi za Taifa
za Tanzania, Wizara ya Kilimo na Mifugo na Mamlaka ya Ngorongoro ndani
ya miezi sita kufanyika kwa utafiti wa kina wa kisayansi wa kubaini
mbinu mpya ya kupambana na mimea hiyo vamizi inayotawala mimea inayotumiwa
na wanyama.
Akizungumza katika kikao kilichojumisha Wahifadhi
wa Mamlaka ya Ngorongoro na Wajumbe wa Baraza la wafugaji, Waziri Makamba
amesikitishwa na kitendo cha Uongozi wa Mamlaka ya Ngorongoro kushindwa
kuandaa mpango kabambe wa usimamizi wa hifadhi baada ya ule wa awali
kuisha muda wake. Waziri Makamba ameuagiza uongozi wa Ngorongoro kuandaa
mpango huo mapema na kuwa shirikishi. " Mpango mtakoandaa hakikisheni
kuwa unakuwa shirikishi kwa jamii inayozunguka na wadau na Taasisi muhimu
likiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Waziri Makamba pia ameagiza kufanyika kwa ukaguzi
wa kimkakati wa Mazingira utakaojumuisha Wilaya nzima ya Ngorongoro
na kuitaka Mamlaka ya Ngorongoro kushirikiana na Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC kutekeleza wajibu huo mapema.
Ukaguzi huo wa kimkakati wa kimazingira kwa Wilaya hiyo unatazamiwa
kutoa mtazamo wa hali ya mazingira kwa miaka hamsini ijayo.
Aidha, Waziri Makamba ameagiza kufanyika kwa Tathmini
ya Athari kwa Mazingira ama Ukaguzi wa Mazingira katika Hotel
zote zilizopo eneo la hilo na kulitaka Baraza la Taifa la Hofadhi na
Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupita siku ya Alhamisi tarehe 30/03/2016
kuwaandikia adhabu na kuwatoza faini wahusika wote ambao hawana vyeti
hivyo. "Haiwezekani toka mwaka 2004 Sheria ipo na mpaka leo watu
wanaendea na mchakato, hii haikubaliki!" Alisisitiza Makamba.
Katika hatua nyingine Waziri Makamba ametoa miezi
sita kwa wamiliki wa Hotel zilizopo katika Mamlaka ya Ngorongoro kuwekeza
katika mfumo mpya wa kuvuta maji kutoka Mto Lukusale na kusitisha mfumo
wa sasa wa kutoa maji kwenye creator. Pia Makamba ameutaka
ungozi wa Mamlaka ya Ngorongoro ndani ya miezi sita kuandaa ramani itakayoonyesha
mito na vijito vyote vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo.
Waziri Makamba ametoa maagizo hayo leo juu ya
namna bora ya kutumia rasilimali ya "creater" kwa
ajili ya utalii na Uhifadhi wa Mazingira, ikiwa ni pamoja na utekelezaji
wa zuio la mifugo ndani ya crater. Ziara maalumu na mahsusi ya
kukagua utekelezaji na uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira inayofanywa
na Waziri Makamba hii leo imefika Wilayani Ngorongoro.
EmoticonEmoticon