Mkurugenzi Msaidizi Masuala
Mtambuka kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Venance Manori
akiwa katika picha ya pamoja na waandaaji wa warsha ya kuwawezesha
Maafisa Waandamizi wa Serikali kutoka nchi sita za Afrika katika
kutengeneza mipango inayozingatia usawa wa kijinsia katika elimu kutoka
shirika la Plan International- Tanzania, Global Partnership for
Education (GPE), Dubai Cares pamoja na United Nations Girls’ Education
Initiative (UNGEI) mara baada ya ufunguzi wa warsha hiyo uliofanyika
jana jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Plan
International- Tanzania, Jorgen Haldorsen akitoa neno fupi kwa ajili ya
kuwakaribisha Maafisa Waandamizi wa Serikali kutoka nchi sita za Afrika
katika ufunguzi wa warsha ya kuwawezesha kutengeneza mipango
inayozingatia usawa wa kijinsia katika elimu. Ufunguzi wa warsha hiyo
ulifanyika jana jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Maafisa Waandamizi wa
Serikali wanaohusika na elimu kutoka nchi sita za Afrika wakisikiliza
hotuba ya Mkurugenzi Msaidizi Masuala Mtambuka kutoka Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia (hayupo pichani), Venance Manori wakati wa
ufunguzi wa warsha ya kuwawezesha maafisa hao katika kutengeneza mipango
inayozingatia usawa wa kijinsia katika elimu.Warsha hiyo ya siku tatu
imefunguliwa jana jijini Dar es Salaam.
…………………
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Serikali imejipanga kutengeneza
mwongozo wa kuwarudisha shuleni wanafunzi waliopata mimba wakiwa
masomoni ili kuhakikisha wanapata elimu hadi kufikia ngazi za juu.
Hayo yamesemwa jana Jijini Dar es
Salaam na Mkurugenzi Msaidizi Masuala Mtambuka kutoka Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Venance Manori alipokuwa akifungua warsha ya
kuwawezesha Maafisa Waandamizi wa Serikali kutoka nchi sita za Afrika
katika kutengeneza mipango inayozingatia jinsia katika elimu kwa niaba
ya Waziri wa Wizara hiyo Prof. Joyce Ndalichako.
Manori amesema Serikali ya
Tanzania inajitahidi kuzingatia jinsia katika utoaji wa elimu ambapo
takwimu zinaonyesha kuwa elimu ya Msingi na Sekondari uwiano wake ni
moja kwa moja japo kuwa idadi ya wasichana hupungua kutokana na
changamoto mbalimbali zinazowakumba hivyo lengo la warsha hiyo ni
kuwasaidia wadau kuweka mipango ya elimu inayozingatia usawa wa
kijinsia.
“Serikali yetu imejipanga
kuhakikisha wasichana wanapata elimu hadi ngazi za juu lakini mpango huo
unakumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za mimba na ndoa za utotoni
hivyo ili kuhakikisha mtoto wa kike anafikia ngazi za juu za elimu tuko
kwenye mchakato wa kuandaa mwongozo kwa ajili ya wanafunzi waliopata
mimba wakiwa bado wanasoma kupata nafasi ya kuendelea na masomo,”alisema
Manori.
Mkurugenzi Msaidizi amezitaja
changamoto zingine zinazowapelekea wanafunzi wa kike kuacha shule
zikiwemo za umaskini, mazingira rafiki ya kusomea, mila na desturi
zinazomkataza msichana kupata nafasi ya kusoma pamoja na kukosa muda wa
kujisomea kwa sababu ya kufanya kazi nyingi wanaporudi majumbani.
Manori ametoa rai kwa Watanzania
kuelewa kuwa kila mtoto ana haki na wajibu wa kupata elimu bila kujali
jinsia pia ameiasa jamii kuacha kuwaozesha wasichana wenye umri chini ya
miaka 18 ili waweze kufikia malengo yao waliyojipangia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
shirika la Plan International- Tanzania, Jorgen Haldorsen ameahidi
kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha mipango ya elimu
nchini inaangalia usawa wa kijinsia kwa kuwa ni njia moja wapo
itakayochochea maendeleo ya elimu kwa watoto wa kike.
“Warsha hii imeandaliwa kwa ajili
ya wadau wote kutoa mawazo yao juu ya changamoto za usawa wa kijinsia
zinazoikumba sekta ya elimu pamoja na kuwapa fursa wadau hao kushauriana
kuhusu mikakati mbalimbali ya kutatua changamoto hizo ili kuinua sekta
ya elimu sio tu kwa Tanzania bali kwa Afrika nzima,”alisema Haldorsen.
Haldorsen ameongeza kuwa mfumo wa
elimu umetambua uhusiano uliopo kati ya elimu na usawa wa kijinsia ndio
maana wadau wa masuala ya elimu wa Serikali kutoka katika baadhi ya nchi
za Afrika wameamua kuungana kwa pamoja kujadili juu ya tathmini,
mpangilio na ufuatiliaji wa elimu unayozingatia jinsia.
Tanzania imekua nchi ya kwanza
kuendesha warsha hiyo ya siku tatu iliyoshirikisha maafisa waandamizi wa
Serikali wanaoshughulikia mipango ya elimu kutoka nchi za Mozambique,
Zambia, Malawi, Uganda, Zanzibar na Tanzania Bara.
Imeandaliwa kwa ushirikiano wa
shirika la Plan International- Tanzania, Global Partnership for
Education (GPE), Dubai Cares pamoja na United Nations Girls’ Education
Initiative (UNGEI).
EmoticonEmoticon