Shime maarufu kama Mchawi Mweusi, amezungumza hayo wakati anaendelea
kufanya maandalizi ya mwisho ya mchezo dhidi ya Jamhuri ya Congo
utakaofanyika Jumapili Oktoba 2, kwenye Uwanja wa Alphonse
Massamba-Débat ulioko kwenye Makutano ya Barabara za Nkolo na Boko, hapa
jijini Brazzaville.
Katika mazungumzo yake, Shime anasema: “Timu iko vizuri. Tumejiandaa
vizuri kwa yale ya msingi yote tumekamilisha. Kwa hivyo, kila kitu kiko
sawa, kama tulivyokusudia. Tupo hapa Congo kwa sasa kumalizia au
kukumbushia mambo mawili au matatu hivi...
“Lakini pia tupo hapa Congo kuzoea hali ya hewa. Kwa bahati nzuri si
tofuati na ya nyumbani Tanzania,” anasema Shime kwa kujiamini kabisa leo
mchana Septemba 29, 2016 huku akijiandaa kwenye mazoezi.
Shime anasema kwamba mfumo atakaoutumia ni wa 4-4-2 katika mchezo huo
wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa
vijana. Fainali hizo zitafanyika jijini Antananarivo, Madagascar mwezi
Aprili, mwakani.
Anasema kwamba mfumo huo ni rafiki kwa Serengeti Boys kwani katika
michezo takribani 15 ya kimataifa hajapoteza hata mmoja, “Kwa hivyo
siwezi kubadili mfumo huu. Ni mfumo wa kushambulia na kulinda
tusifungwe. Vijana wanauelewa zaidi na ndio mfumo wetu.”
Shime aliyekuwa mchezaji zamani kabla ya ndoto zake za kusonga mbele
kufutwa kwa majeruhi, anasema kwamba benchi nzima la ufundi linafahamu
kuwa mchezo wa Jumapili dhidi ya Congo ni mgumu kwa sababu ya umuhimu
wake.
Na akiwaelezea Congo - wapinzani wake, Kocha Shime anasema: “Ni timu
ya kawaida kwa maana wanafungika. Kwenye mchezo huu ukiangalia kwa
makini sisi ndio tunahitaji zaidi ushindi kuliko Congo. Lakini nataka
uwaambie Watanzania kwamba pamoja na hayo, nawaheshimu Congo, najua wako
nyumbani lakini mwisho wa siku ni wachezaji 11 kila upande ndio
watakaoingia uwanjani.”
Amesema kwamba amekiandaa kikosi chake vema kabisa katika eneo la
mbinu, ufundi na saikolojia. “Akili za vijana wangu wooooote ni
kuhakikisha tunafanya vema kwenye mchzo wa Jumapili.”
Naye Kocha wa Makipa, Muharami
Mohammed au Shilton, alisema: “Silaha zangu ziko tayari kwa vita, makipa
wangu wangu wote akiwamo Kelvin Kayego, Ramadhani Kabwili na Brazio
wote wako fiti. Ye yote kati yao anaweza kucheza.”
EmoticonEmoticon