WATOTO 13,266 MKOANI TANGA WANUFAIKA NA HUDUMA ZA AFYA ZITOLEWAZO NA UHIC

July 07, 2016
Lee Kwiwoon akuzungumza na washiriki wa mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo vijana(Keepers) katika vijana waliofundishwa kuhudumia watoto katika masuala ya Afya na Lishe
   
Washiriki wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kumalizika mafunzo hayo

JUMLA ya watoto 13,266 wenye umri chini ya miaka 10 wamenufaika mkoani hapa na huduma za afya  zitolewazo na taasisi ya Kikorea ijulikanayo kama UHIC (United Help for International Children) .
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo kanda ya Tanzania,  Lee Kwiwoon alitoa taarifa hiyo hapa mwishoni mwa juma lililopita katika mkutano uliojumuisha madaktari, manesi na wahudumu wa afya kutoka wilaya tatu za mkoa huu, ambazo zimelengwa katika mradi wa taasisi hiyo.

Mkurugenzi huyo alisema lengo la kuanzisha taasisi hiyo ni kutoa huduma kwa watoto wenye matatizo mbalimbali ya kiafya yanayowapata wenye umri chini ya miaka 10.

Aliwaeleza wanasemina hao kwamba watoto wengi walio katika umri chini ya miaka 10 hukumbwa na magonjwa mengi, hasa malaria, upungufu wa damu na utapiamlo. Magonjwa mengine ni pamoja na kifua, kuzaliwa njiti na kuharisha. 

Lee aliwaambia maofisa na manesi pamoja na wahudumu wa afya kwamba jukumu kubwa la taasisi yake ni kuzuia magonjwa yanayowanyemelea zaidi watoto wadogo pamoja na kuhakikisha watoto hao wanakua katika afya bora.

Alifahamisha kwamba taasisi hiyo ya UHIC imeanzisha mradi ujulikanao Keepers' ambao unawafundisha na kuwapatia mafunzo vijana wanaotoa huduma ya kuokoa maisha ya watoto kutoka janga la njaa, maradhi na kuwasaidia waishi katika mazingira mazuri ya kiafya.

"Afya na uzuiaji wa magonjwa yawapatayo watoto wengi mkoani Tanga ni suala linalozungumzika na hivyo kuwafanya wadau kuamua kujitolea kuanzisha taasisi zitakazosaidia kuondoa adha hiyo kwa watoto wetu", alisema Lee.

Mkurugenzi huyo alibanisha kuwa taasisi ya UHIC ni ya kimataifa iliyoanzishwa kwa lengo la kutoa huduma endelevu za afya kwa watoto waishio maeneo ya vijijini (pembezoni) mkoani hapa.

Alisema wamechagua wilaya tatu ambazo ni Pangani, Muheza na Tanga kuwa za mfano katika kuanza na mradi huo ambapo jumla ya vijiji 27 vitahusika. Alisema taasisi yake ina jukumu la kugawa dawa na kwamba wahudumu 24 tayari wamekwishapatiwa mafunzo ya kuhudumia watoto hao katika vijiji husika.

Akizungumza katika mkutano huo, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Rehema Maggid alisema mkoa umepoteza maisha ya watoto wapatao 653 kutokana na magonjwa mbalimbali, yakiwemo malaria, kikohozi, upungufu wa damu na kuharisha.

Pamoja na kupongeza msaada huo wa Korea akisema kuwa umefika wakati ukihitajika sana, lakini akataka wataalamu wanaopelekwa kwenye vijiji hivyo wapewe ushirikiano unaofaa.

Mapema, akifungua semina hiyo, Kaimu Mkuu wa Mkoa waTanga, Mayassa Hashim alisikitishwa na vifo hivyo ambapo alisema vingeweza kuzuilika kwa kutoa elimu ya kutosha kwa wazazi . 

Hata hivyo, Mayassa ambaye pia ni OfisaElimu wa Mkoa, alieleza matumaini kwamba ujio wa taasisi hiyo pamoja na madawa na wataalamu wao itasaidia kuondoa vifo visivyotarajiwa vya watoto wadogo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »