Na Mwandishi wetu Washington
Wazanzibari waishio nchi za nje wametakiwa kuwekeza nyumbani kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya taifa.
Wito huo ulitolewa jana na maofisa kutoka Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zaznzibar (ZSSF) wakati wakizungumza na Wazanzibari waishio nchini Marekani.
Akizungumza kwenye mkutano huo uliondaliwa na Jumuiya ya Wazanzibari waishio nchini Marekani (ZADIA), Meneja wa Mipango na Uwekezaji kutoka ZSSF Bwana Khalifa Muumin Hilal alisema kuwa Taasisi yake ina miradi kadhaa ya uwekezaji inayoendeshwa kwa ushirikiano na Benki ya Watu wa Zanzibar, na kwamba inawahamasisha Wazanzibari waishio Ughaibuni kuwekeza katika miradi hiyo.
Miongoni mwa miradi hiyo ni mradi wa nyumba za kisasa katika eneo la Mbweni, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar ambao ujenzi wake tayari umeanza na unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miaka mitatu.
Bwana Hilal alifafanua kuwa eneo hilo litakuwa na majengo ya nyumba za kuishi yenye urefu wa ghorofa saba, ambapo kila ghorofa itakuwa na nyumba mbili.
"Kutakuwa na nyumba za vyumba viwili, vitatu na vinne" alifafanua Meneja Hilal, na kuongeza kuwa nyumba hizo zitapatikana kwa bei nafuu.
Akijibu swali kukhusu masharti ya upatikanaji wa nyumba hizo, Bwana Hilala alifafanua utaratibu wa upatikanaji wake kwa kusema "Kwanza kabisa tunaangalia vigezo vya fedha, kwa maana ya kipato cha mtu, kuna fomu ya maombi unajaza, kisha tunakupatia fomu ya mkataba ambayo inaelezea masharti yote, na tunaendelea kutoka hapo".
Aliendelea kusema kuwa nyumba hizo zitapatikana kwa njia za mkopo au fedha taslim, ambapo ukilipa fedha taslim utapata punguzo lisilozidi asiliam tano (5%).
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tawi la Muamala wa Kiislamu katika Benki ya Watu wa Zanzibar Bwana Said Muhammed Said, alisema "Tumeweka utaratibu ili kila mtu aweze kumudu kununua nyumba hizo, na hapo ndipo inapokuja nafasi ya Benki"
Aliendelea kusema kuwa, baada ya kujaza mikataba na ZSSF, mwekezaji ambaye hana uwezo wa kulipa fedha taslim anaweza kwenda kwenye Benki yake na kupata mkopo wenye masharti nafuu.
Akijibu swali kukhusu iwapo mtu atafariki kabla ya kumaliza kuilipia nyumba hiyo, Bwana Said alitoa khofu kwa kusema "Mtu haki yake haipotei". Aliendelea kuwa mtu akifariki kuna hali mbili, ama nyumba itauzwa na haki ya marehemu kupewa warithi wake, au warithi wakiamua kuendelea kulipa basi wataendelea kubaki na nyumba yao.
Kukhusu taratibu za malipo, Bwana Hilal alisema, mtu anaweza kulipa kila mwezi, miezi mitatu au kama atakavyojaza kwenye mkataba wa mauzo.
Mbali na nyumba za kuishi, eneo hilo pia litajumuisha viwanja vya watoto, michezoya aina mbalimbali, mabwawa ya kuogelea, kituo cha Mikutano Msikiti na mengineyo.
Akijibu swali iwapo mikopo ya nyumba hizo itakuwa na riba au la, Bwana Said alisema "Unachagua, kama unataka mkopo wenye riba au mkopo kwa kupitia tawi letu la Muamala wa Kiislamu, huo utakuwa hauna riba".
Alendelea kufafanua kuwa kiwango cha riba rubuni vinategemea na hali ya soko kwa wakati ule mteja atakapochukua mkopo ikiwemo thamani ya sarafu kwa wakati ule, viwango vya riba vinavyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania na urefu wa muda wa mkopo wenyewe.
Kukhusiana na khofu ya mtu kupoteza nyumba yake iwapo atapoteza kazi, Bwana Said aliwatoa khofu Wazanzibari kwa kusema "Kutolipa mkopo kwa wakati uliokubaliwa kulaleta athari katika mfumo wa Benki.
Hata hivyo, iwapo mtu atashindwa kulipa kwa mara ya mwanzo na ya pili tunamtumia barua ya ukumbusho. Mara ya tatu ikiwezekana tunakutana naye ana kwa ana na kutafuta ufumbuzi" Ama iwapo mtu atapoteza kazi milele kwa sababu zisizoweza kuepukika kama ugonjwa na mengineyo, Mkurugenzi huyo alisema "Tutazungumza naye ili kuiuza nyumba na kumrejeshea chake".
"Tutakuwa na mkataba maalum, na yote hayo tuliyoyazungumza yatakuwemo humo", alisisitiza Bwana Said.
Mradi wa Makaazi ya Mbweni ni hatua za awali zilizopangwa kutekelezwa na ZSSF, kwani baadaye kutakuwa na mpango wa ujenzi wa nyumba moja moja (bungalow).
Hata hivyo, Mkurugenzi Said alisema kuwa mtu akiwa na kiwanja chake binafsi, basi pia PBZ inaweza kutoa huduma za kifedha kugharamia ujenzi wa nyumba binafsi. "Muhimu uwe na hati miliki ya kiwanja, uwe na mkandarasi anaye julikana, na siyo mafundi wa vichochoroni", alifafanua Bwana Said.
Akijibu hoja juu ya sheria inayowazuia raia wa kigeni kumiliki ardhi Zanzibar, Meneja Hilal alifafanua kwa kusema "Ardhi ni milki ya Serikali, lakini serikali inaruhusu ukodishaji wa ardhi kwa wawekezaji. Hata sisi ZSSF tumekodishwa tu ardhi hiyo ya Mbweni, lakini kuna sheria ya umiliki wa nyumba kwenye majengo ya ghorofa, na sheria hii haimbagui mtu yeyote"
Aliongeza kuwa kila mtu atapewa hati ya umiliki wa nyumba katika ghorofa hizo bila kujali uraia wake. "Ndiyo maana tumekuja kwenu" alisistiza Bwana Hilal.
Baadhi ya wachangiaji kwenye mkutano huo waliezea wasiwasi wao kuwa nyumba hizo huenda zikatolewa kwa upendeleo kama ilivyotokea kwenye nyumba za eneo linalojuilikana kama "Kwa Mchina". Awali nyumba hizo zilikusudiwa kuwasaidia watu wenye vipato vya chini, lakini badala yake zikatolewa kwa upendeleo na kumalizikia mikononi mwa watoto wa Wakubwa. "Je kuna uhakika gani kuwa mradi wa nyumba za Mbweni hautomalizikia kuwa kama ule wa Kwa Mchina"? aliuliza mchangiaji mmoja.
Akijibu hoja hiyo, Bwana Hilal alisema kuwa, hilo halitotokea. Zitatolewa kwa usawa kwa mtu yoyote yule mwenye uwezo, na ndiyo maana tumekuja Marekani kuunadi mradi huu, ili kila mtu mwenye uwezo akiwa Mzanzibari au laa, ndani au nje ya nchi aweze kununua nyumba hizo.
Maofisa hao wa kutoka Benki ya Watu wa Zanzibar na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar wapo nchini Marekani kuhudhuria Kongamano la Wanadiaspora wa Tanzania (DICOTA) lilloifanyika katika Jimbo la Texas.
Bwana Hilal alielezea shukurani zake kupata fursa ya kuzungumza na Wazanzibari nchini hapa, na kuelezea matmaini yake kuwa mkutano huo hautokuwa wa mwisho bali wa mwanzo kwa jili ya kuendeleza maslahi ya Zanzibar.
Kwa maelezo zaidi juu ya mradi huo tembelea http://zssf.org/en/, na fomu za maombi zitapatikana hapo katika wakati mwafaka.
EmoticonEmoticon