Afisa
Habari wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Veronica Kazimoto akizungumza na
waandishi wa habari Oktoba 7, 2015 jijini Dar es Salaam kuhusu mkutano
wa wadau wa takwimu wenye lengo la kujadili namna ya kushirikiana katika
kuhakikisha takwimu za viashiria vya Mpango wa Maendeleo Endelevu
(SDGs) zinapatikana kwa wakati unaotakiwa. Mkutano huo utafanyika kesho
katika ukumbi wa hoteli ya Habour View iliyopo Dar es Salaam.
…………………………………………………………………………………………………
Na: Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KATIBU Mkuu
Kiongozi Balozi Ombeni Sefue kesho anarajia kuwa Mgeni Rasmi katika
mkutano wa wadau wa takwimu ulioandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu
(NBS) kwa ajili ya kukubaliana jinsi ya kushirikiana katika kuhakikisha
takwimu za viashiria vya Mpango wa Maendeleo Endelevu zinapatikana kwa
wakati.
Akizungumza na wandishi wa
habari leo jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa ofisi hiyo, Veronica
Kazimoto amesema mkutano huo utafanyika katika ukumbi wa Hoteli ya
Habour View, Dar es Salaam ukiwa na lengo la kuelimishana juu ya
kukamilika kwa utekelezaji wa Malengo ya Milenia (MDGs) na kuanza kwa
Malengo mapya ya Maendeleo Endelevu – Sustainable Development Goals
(SDGs).
“Kama mnavyofahamu utekelezaji
wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia – MDGs ulikuwa ni wa miaka 15 kuanzia
mwaka 2000 hadi 2015. Mpango huu wa MDGs unakamilika mwaka huu na
kuanza kwa mpango mpya wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ambao pia
ni miaka 15 ijayo”, amesema Kazimoto.
Kazimoto amefafanua kuwa mkutano
huo utahudhuriwa na wadau wa takwimu takribani 100 kutoka Wizara,
Idara, Wakala na Taasisi za Serikali, Wadau wa Maendeleo, Wadau wa Sekta
Binafsi pamoja na Wadau wa Taasisi za Elimu ya Juu.
Aidha, Afisa Habari huyo amesema
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeandaa mkutano huo kwa kuwa ndio yenye
mamlaka nchini ya kutoa takwimu rasmi kwa ajili ya kupanga mipango ya
maendeleo na kufanya maamuzi sahihi.
Kazimoto ameongeza kuwa mwezi
Septemba mwaka huu, viongozi wa nchi mbalimbali duniani akiwemo Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, walikutana
nchini Marekani kwa ajili ya kutathmini utekelezaji wa Malengo ya
Maendeleo ya Milenia – MDGs ambapo ilionekana kwamba kuna baadhi ya
malengo yalikuwa yamefanikiwa na mengine hayakufanikiwa.
Kutokana na hali hiyo, viongozi
hao walikubaliana na kuridhia mpango mbadala wa MDG ambao unaitwa Mpango
wa Maendeleo Endelevu ambao pia ni wa miaka 15 kuanzia 2015 hadi 2030.
Mkutano huo wa viongozi
mbalimbali duniani uliidhinisha mpango huo mpya wenye malengo 17 na
viashiria 169 ambavyo kila nchi kwa uratibu wa Kitengo cha Takwimu cha
Umoja wa Mataifa inatakiwa kuvipitia na kuona kama kuna takwimu za
kutosha kukidhi upimaji wa malengo kwa kutumia viashiria hivyo.
Malengo hayo 17 yaliyoidhinishwa
na mkutano huo wa wakuu wa nchi mbalimbali duniani ni pamoja na Kuondoa
Umaskini wa aina zote, kuondoa njaa, kuhakikisha kuna maisha yenye afya
bora na kuhamasisha ustawi kwa wote, Kulinda uhai wa viumbe juu ya
ardhi, elimu Bora na usawa wa kijinsia.
Malengo mengine ni kuhakikisha
upatikanaji na matumizi endelevu ya maji na usafi wa mazingira kwa wote,
kuhakikisha kuna upatikanaji wa huduma rahisi ya nishati endelevu na ya
kisasa kwa wote, uwepo wa Ajira na ukuzaji wa uchumi, uwepo wa Viwanda
na Miundombinu, kulinda Amani na Utawala wa Sheria na kupungunza tofauti
ya kipato baina ya nchi na nchi na ndani ya nchi.
Ameyataja malelengo mengine kuwa
ni pamoja na uwepo wa Miji na Jamii endelevu, kuwajibika katika
Uzalishaji, kuchukua hatua za haraka kukabiliana na mabadiliko ya tabia
nchi na madhara yake, kutunza na kuwa na matumizi endelevu ya bahari
pamoja rasilimali za baharini kwa ajili ya maendeleo endelevu na
kushirikiana na wadau katika kufikia malengo ya SDGs.