Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ally Idd akifungua mafunzo ya
Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala Mikoa nchini leo jijini Dar es salaam.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Hawa Ghasia akimpongeza Mgeni Rasmi Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ally Idd na mara baada ya
kufungua mkutano wa mafunzo ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala Mikoa
nchini leo jijini Dar es salaam.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ally Idd akitete jambo na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Hawa Ghasia wakati wa mkutano wa
mafunzo ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala Mikoa nchini leo jijini Dar
es salaam.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa mafunzo ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala Mikoa nchini leo jijini Dar es salaam.
(Picha zote na Eleuteri Mangi-Maelezo)
Eleuteri Mangi-MAELEZO
21/07/2014
Viongozi wa Wakuu wa Mikoa nchini
wameaswa kufahamiana kama viongozi ili kubadilishana uzoefu wa kujenga
mtandao wa mawasiliano na mahusiano kwa ajili ya kupashana habari na
kushauriana.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ally Idd wakati wa ufunguzi wa
mafunzo ya Wakuu wa Mikoa (RC) na Makatibu Tawala Mikoa (RAS) nchini leo
jijini Dar es salaam.
“Jengeni mshikamano wa mahusiano
katika utendaji kazi wenu mkiimarisha maelewano miongoni mwenu
mtarahisisha utendaji na kuepuka migogoro isiyo ya lazima” alisema
Balozi Seif.
Balozi Seif aliendelea kusema,
“Tumieni nafasi hii kufahamiana muweze kujenga mtandao wa mahusiano,
mawasiliano mkiimarisha mashirikiano ili kuleta maendeleo katika maeneo
yenu ya kazi kwa manufaa ya wananchi”.
Balozi Seif alisema kuwa kila kazi
inachangamoto zake, katika kutekeleza majukumu yao vizuri na kubainisha
kuwa viongozi hawa baadhi yao wamekuwa na misuguano ya hapa na pale
ambayo husababishwa na mawasiliano yasiyoridhisha.
Balozi Seif alisisitiza kuwa dawa
ya misuguano hiyo itapatikana kupitia mafunzo hayo ya siku tatu ambapo
viongozi hao watakumbushwa mengi waliyoyasahau, watapata mengi ya
kujifunza, kujikumbusha na kujinoa ili kuhuisha uhai wa utekelezaji wa
majukumu yao ambao utaleta mshikamano na umoja miogoni mwa watendaji
hao.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu Hawa Ghasia alipokuwa akimkaribisha Mgeni Rasmi alisema kuwa
mafunzo hayo yataimarisha mahusiano na mawasiliano ya viongozi hao
katika kutekeleza majukumu yao ili yapate tija iliyokusudiwa.
Waziri Ghasia amewaasa viongozi
hao kuwa wasipofanya kazi kama timu hawawezi kupata tija katika maeneo
yao ya kazi hasa katika kuwaletea maendeleo wananchi wanaowaongoza na
nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Wakuu wa Mikoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro
akimshukuru na kumhakikishia Mgeni Rasmi Balozi Seif kuwa wanamatumaini
makubwa kuimarisha mahusiano kati yao vilevile na wanasiasa wote na
kuahidi kuwa watatoa huduma bora zaidi.
Aidha, mikoa ya Lindi, Mtwara na
Ruvuma viongozi wao hawatashiriki mkutano huo kwa kuwa kwa sasa wapo
kwenye ratiba ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Jakaya Kikwete katika mikoa hiyo.
Wakuu wa mikoa hiyo waunganishwa
kupata mfunzo kama hayo na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa ya
Zanzibar ambayo itapangwa kufanyika hapo baadaye ambapo Serkali ya
Mapinduzi imeahidi kushirikiana na Tasisi ya Uongozi kutoa mafunzo hayo.
Mafunzo hayo yameandaliwa na
Taasisi ya Uongozi kwa lengo la kuwawezesha viongozi hao kufahamu kwa
kina umuhimu wa mawasiliano bora baina ya viongozi wa kisiasa na
watendaji Wakuu wa ngazi ya Mkoa ili kuimarisha utoaji bora wa huduma
kwa wananchi.
EmoticonEmoticon