HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA
MIZENGO PETER PINDA (MB),
KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MATUMIZI
YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2014/2015
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja
kwamba, kutokana na Taarifa zilizowasilishwa katika Bunge lako Tukufu na
Wenyeviti wa Kamati za Katiba, Sheria na Utawala; Kamati ya Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa; Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara na Kamati ya Masuala
ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee
na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka
2013/2014 na Mwelekeo kwa Mwaka 2014/2015. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu
likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu,
Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Taasisi zilizo
chini yake pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2014/2015.
2.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote na
kwa masikitiko makubwa naomba nichukue fursa
hii kutoa salamu za pole
kwako na kwa Bunge lako Tukufu kwa kuondokewa na wabunge wawili, Mheshimiwa William
Augustao Mgimwa, aliyekuwa Mbunge wa Kalenga, aliyefariki tarehe 01 Januari,
2014 na Mheshimiwa Saidi Ramadhani Bwanamdogo, aliyekuwa Mbunge wa Chalinze,
ambaye alifariki tarehe 22 Januari 2014. Aidha, niwape pole Wananchi wa Mkoa wa
Mara kwa kifo cha Mheshimiwa John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo,
kilichotokea tarehe 25 Machi 2014, na kwa Wananchi wa Wilaya ya Urambo kwa kifo
cha Mheshimiwa Anna Magowa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, kilichotokea tarehe
24 Septemba 2013. Vilevile, natoa pole kwa Wananchi wa Wilaya ya Kalambo kwa
kifo cha Mheshimiwa Moshi Mussa Chang’a aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo,
aliyefariki tarehe 21 Aprili 2014. Naomba pia niwape pole Waheshimiwa Wabunge
na Wananchi wote
waliofiwa na ndugu na jamaa zao
kutokana na majanga na matukio mbalimbali tangu
nilipowasilisha Bajeti yangu
ya mwaka 2013/2014.
Tunamwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu wote mahali pema
Peponi. Amina! Nichukue fursa hii pia kuwapa pole Wahanga wote wa majanga
mbalimbali yakiwemo mafuriko na ajali za barabarani, na niwashukuru kwa dhati
wote waliotoa misaada ya hali na mali wakati wa ajali na maafa hayo.
3.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha
2013/2014, Bunge lako Tukufu limepata Wabunge wapya watatu ambao ni Mheshimiwa
Yusuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani; Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa,
Mbunge wa Kalenga; na Mheshimiwa Ridhiwan Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze.
Nawapongeza kwa kuchaguliwa kuwawakilisha Wananchi katika Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Nawaomba watumie fursa waliyoipata kwa manufaa ya
Wananchi na Taifa kwa ujumla.
MAANDALIZI YA BAJETI
4.
Mheshimiwa Spika, huu ni mwaka wa
pili tangu tuanze utaratibu wa Mzunguko mpya wa Bajeti ambao unatuwezesha
kukamilisha Mjadala wa Bajeti ya Serikali ifikapo tarehe 30 Juni ya kila
mwaka. Taarifa za awali zinabaini kwamba
utaratibu huu umeanza kuonesha mafanikio ya haraka katika utekelezaji wa kazi zilizopangwa. Bajeti hii imeendelea kutayarishwa
kwa kuzingatia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi
ya mwaka 2010; Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza
Uchumi na Kuondoa Umaskini Tanzania (MKUKUTA II); Mpango wa Kwanza wa Maendeleo
wa Miaka Mitano wa Mwaka 2011/12 hadi 2015/16; Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015;
na Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa (Big Results Now – BRN). Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea
kutekeleza miradi ya kipaumbele
iliyoainishwa kwenye mipango
hiyo ya Kitaifa ili kuleta maendeleo endelevu na ya
haraka yatakayowanufaisha Wananchi wa Tanzania.
5.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru Wajumbe
wa Kamati zote za Kudumu za Bunge lako Tukufu kwa mchango wao mkubwa wakati wa
uchambuzi wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za
Serikali Zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kazi waliyoifanya ni
kubwa na ambayo imetuwezesha kukamilisha maandalizi ya Bajeti ninayoiwasilisha
leo. Maoni na Ushauri wao utazingatiwa wakati wa kukamilisha mjadala wa Bajeti
ya Serikali na utekelezaji wake.
HALI YA SIASA
6.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla hali ya
siasa Nchini ni tulivu na Vyama vya Siasa vinaendelea kutekeleza majukumu yao. Nchi
yetu inapitia kwenye kipindi cha mpito ambapo tunaandika Katiba Mpya
itakayoweka mustakabali wa mwelekeo wa
Taifa letu kwa miaka mingi ijayo. Nawasihi Wanasiasa na Wananchi wote kwa
ujumla kutoa ushirikiano mkubwa wakati wa maandalizi ya Katiba hiyo ambayo
baadaye wananchi wote wataipigia kura ya maoni.
Nawaomba tushindane kwa nguvu ya hoja na si hoja ya nguvu katika kuandaa
Katiba hii ambayo itatuongoza sasa na vizazi vijavyo.
7.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za
kukuza na kuimarisha demokrasia ya vyama vingi Nchini, Ofisi ya Msajili wa
Vyama vya Siasa imeratibu shughuli za Vyama vya Siasa kwa kuhakikisha
kunakuwepo na fursa sawa katika shughuli za siasa Nchini. Hadi Aprili 2014,
idadi ya Vyama vya Siasa vyenye Usajili wa kudumu imefikia 21 baada ya Chama
cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kupata usajili wa kudumu mwezi Juni, 2013.
Aidha, Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-TANZANIA), Chama cha
Wananchi na Demokrasia (CHAWADE) na Chama cha Maridhiano na Uwiano (CMU) vimepata
usajili wa muda. Nirejee wito wangu kwa Viongozi na Wanachama wa vyama vyote
vya siasa kuendeleza utamaduni wa kuvumiliana na kutohamasisha siasa za chuki
na vurugu ambazo zinaweza kutugawa na kuhatarisha amani, utulivu na umoja wa
Taifa letu tulioujenga kwa miaka mingi.
ULINZI NA USALAMA
Usalama wa Raia
8.
Mheshimiwa Spika, Nchi yetu
imeendelea kudumisha amani na utulivu kama tunu ya Taifa iliyojengwa na
kuimarishwa tangu tulipopata uhuru. Katika mwaka 2013/2014, Jeshi la Polisi
limeendelea kutekeleza Programu ya Maboresho ya Jeshi na Mkakati wa Kupunguza
Uhalifu ambavyo vimeongeza ushirikiano na wananchi. Jeshi hilo limeongeza
Vikundi 1,778 vya Ulinzi Shirikishi na kufikia vikundi 6,798 kwa mwaka 2013 kwa
Nchi nzima. Vikundi hivyo vimechangia kupunguza vitendo vya uhalifu Nchini
kutoka Asilimia 4.3 mwaka 2012 hadi Asilimia 2.8 mwaka 2013 na hivyo kuchangia
kupungua kwa makosa makubwa na madogo ya jinai kutoka makosa 566,702 mwaka 2012
hadi makosa 560,451 mwaka 2013.
Mauaji ya Wanawake
9.
Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi
zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Wananchi katika kuimarisha ulinzi
na usalama wa raia, hivi karibuni kumetokea wimbi la mauaji ya kikatili dhidi
ya wanawake. Katika kipindi cha Januari hadi Aprili 2014, wanawake wanane (8)
wameuawa kikatili katika Kata za Mugango, Etaro, Nyakatende na Nyegina Wilayani
Butiama. Uchunguzi uliofanyika umebaini kwamba, mauaji hayo yamefanyika mchana
na kwa mtindo unaofanana wa kunyongwa na kanga au kamba na miili yao kufukiwa
kwenye mashimo mafupi au kufichwa vichakani. Mara zote walengwa ni wanawake
wanapokuwa kwenye shughuli zao za kilimo.
10.
Mheshimiwa Spika, Serikali inalaani
vitendo hivyo visivyokubalika katika jamii na itawachukulia hatua kali za
kisheria wale wote watakaobainika kuhusika kwa namna yoyote. Serikali imechukua
hatua kadhaa za kudhibiti vitendo hivyo vya mauaji ikiwa ni pamoja na
kuwakamata watuhumiwa 26 na kati yao 13 wamefikishwa mahakamani. Vilevile, Jeshi la Polisi limeunda kikosi
kazi kwa ajili ya kudhibiti hali hiyo na kufanya mikutano ya kuhamasisha jamii
kuhusu kuanzisha na kuimarisha vikundi vya Polisi Jamii. Nitoe wito kwa
wananchi wema, wenye upendo na Nchi yetu kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu
kwenye vyombo vya usalama ili Sheria ichukue mkondo wake.
Ajali za Barabarani
11.
Mheshimiwa Spika, ajali za barabarani
zimeendelea kuwa tishio kwa maisha ya watu na mali zao. Takwimu za Jeshi la
Polisi zinaonesha kuwa katika mwaka 2013, kulitokea ajali za barabarani 24,480
zilizosababisha vifo vya watu 4,091 na majeruhi 21,536 ikilinganishwa na ajali 23,604 zilizosababisha vifo vya watu
4,062 na majeruhi 20,037 mwaka 2012. Kwa upande wa pikipiki pekee, mwaka 2012 zilitokea jumla ya ajali 5,763
na kusababisha vifo 930 na majeruhi 5,532.
Mwaka 2013, zilitokea ajali 6,831 na kusababisha vifo 1,098 na majeruhi
6,578. Aidha, katika kipindi cha Januari hadi Machi, 2014 zimetokea ajali 1,449
na kusababisha vifo 218 na majeruhi 1,304. Ajali hizi ni nyingi na zinasababisha vifo
vingi na majeruhi ambao wengi wao ni nguvukazi ya Taifa. Ni vyema ikumbukwe
kwamba, Serikali iliruhusu matumizi ya pikipiki kwa nia njema ya kupunguza
matatizo ya usafiri hususan maeneo ya Vijijini. Hata hivyo, fursa hiyo
imeambatana na changamoto ya ajali nyingi barabarani. Hivyo ni wajibu wa
madereva wote kuzingatia sheria za barabarani na kukidhi vigezo vyote vya kuwa
na vibali halali vya kufanya biashara hizo pamoja na leseni za udereva.
SUMATRA, Jeshi la Polisi, Mamlaka za Serikali za Mitaa, na Mamlaka nyingine
zinazohusika zinatakiwa kukaa pamoja ili kuweka mkakati wa kukabiliana na ajali
hizo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba Kanuni za Leseni za Usafirishaji wa
Pikipiki na Bajaji za mwaka 2010 zinatekelezwa
ipasavyo.
Hali ya Mipaka ya Nchi
12.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea
kuliwezesha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kutimiza majukumu yake ya kulinda
mipaka ya nchi yetu na raia wake. Katika mwaka 2013/2014, Serikali imewezesha
Wanajeshi wetu kupata mafunzo mbalimbali katika vyuo vya ndani na nje ya Nchi
pamoja na kushiriki katika mazoezi ya ushirikiano kikanda. Aidha, Jeshi
limeshiriki katika operesheni mbalimbali za kulinda amani zinazoongozwa na
Umoja wa Mataifa huko Darfur (Sudan), Lebanon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
na Sudan Kusini. Nafurahi kulieleza Bunge lako Tukufu kuwa Jeshi limefanya kazi
kubwa, nzuri na kwa weledi mkubwa, nidhamu na kujituma hivyo kuendelea kuipatia
heshima kubwa Nchi yetu. Katika jitihada za kuwapatia Askari mazingira mazuri
ya kuishi, Serikali imeanza kutekeleza Awamu ya Kwanza ya mradi wa ujenzi wa
nyumba za Askari ambapo ujenzi wa majengo 191 kati ya 6,064 unaendelea katika
vikosi mbalimbali vya Jeshi Nchini.
Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa
13.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2013/2014 ni
wa tatu tangu Serikali iliporejesha utaratibu wa kuwachukua Vijana wanaohitimu
kidato cha sita kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa Mujibu
wa Sheria. Hadi kufikia mwezi Desemba 2013, jumla ya Vijana 15,167 wamehitimu
mafunzo ya JKT wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wa Bunge hili Tukufu.
Mafunzo hayo yamewapatia vijana hao fursa ya kujifunza juu ya Ulinzi, Usalama
na Ukakamavu, Uzalishaji mali, Uzalendo na Umoja wa Kitaifa. Katika mwaka
2014/2015, Serikali itachukua vijana zaidi kujiunga na JKT kwa Mujibu wa
Sheria.
SHUGHULI ZA UCHAGUZI, BUNGE, MUUNGANO, MABADILIKO YA KATIBA NA VITAMBULISHO VYA TAIFA
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
14.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2013/2014, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilisimamia na kuendesha chaguzi ndogo za
Wabunge katika Majimbo matatu na Udiwani katika Kata 53 nchini. Chaguzi hizo
zimefanyika kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo vifo na baadhi ya
Waheshimiwa Madiwani kukosa sifa za kuendelea na nyadhifa hizo. Katika Uchaguzi
wa Ubunge uliofanyika katika Jimbo la Chambani - Zanzibar, CUF ilishinda kwa
kupata Asilimia 84 ya kura zote. CCM ilipata kura Asilimia 12.4, ADC ilipata
kura Asilimia 3.5 na CHADEMA ilipata Asilimia 0.4 ya kura zote. Katika Jimbo la
Kalenga – Iringa, CCM ilishinda kwa kupata Asilimia 79.3 ya kura, CHADEMA
ilipata kura Asilimia 20.2 na CHAUSTA ilipata kura Asilimia 0.5. Katika Jimbo
la Chalinze – Pwani, CCM ilishinda kwa kupata Asilimia 86.61, CHADEMA ilipata
kura Asilimia 10.58, CUF ilipata kura Asilimia 1.98, AFP ilipata kura Asilimia
0.59 na NRA ilipata Asilimia 0.25 ya kura zote. Aidha, katika Chaguzi za
Madiwani zilizofanyika katika Kata 53, CCM ilishinda viti 40, CHADEMA viti 12
na NCCR – Mageuzi kiti kimoja (1).
15.
Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na maandalizi ya
kupata vifaa vya kisasa kwa ajili ya zoezi la kuboresha Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura. Katika awamu hii ya uboreshaji wa Daftari, Mfumo wa Biometric
Voter Registration utatumika tofauti na Mfumo wa awali wa Optical Mark Recognition
ambao ulikabiliwa na changamoto nyingi za utendaji. Mfumo huu wa kisasa
unawezesha uandikishaji na uchukuaji wa alama za vidole kwa haraka zaidi na
hatimaye mwananchi kupatiwa kitambulisho cha kupiga kura kwa muda mfupi. Hii
itasaidia sana kuokoa muda na kupata takwimu sahihi za wapiga kura
watakaoshiriki kwenye chaguzi.
16.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii
kuwaomba Viongozi wa Vyama vya Siasa kuhamasisha Wanachama na Watanzania wote
wenye sifa kujiandikisha kwenye Daftari hilo na kupata kitambulisho halali cha
mpiga kura pale zoezi hilo litakapoanza rasmi.
Aidha, ninatoa wito kwa Wananchi wote wenye sifa kujitokeza
kujiandikisha. Ni imani yangu kwamba tukitumia fursa hii kikamilifu tutaondoa
malalamiko ya majina ya baadhi ya wapiga kura kutokuwepo kwenye orodha wakati
wa chaguzi. Ni muhimu tukumbuke kwamba
ni wananchi wenye sifa tu ndiyo watakaoandikishwa. Katika mwaka 2014/2015, Tume
itakamilisha zoezi la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kusimamia
Kura ya maoni kwa ajili ya Katiba Mpya, na kuendelea kutoa elimu ya Mpiga Kura
kwa Wananchi.
Bunge
17.
Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi Julai,
2013 hadi Aprili 2014, Ofisi ya Bunge imeendesha Mikutano Mitatu ya Bunge na
Mikutano mitatu ya Kamati za Bunge. Maswali ya Msingi 410 pamoja na maswali 73
ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa. Aidha, Miswada minane (8) ya Sheria
ilipitishwa na Bunge. Pia, Bunge limekamilisha ukarabati wa Ukumbi wa Bunge na
Miundombinu yake kuwezesha Mkutano wa Bunge la Katiba kufanyika na ujenzi wa
Ofisi za Wabunge Majimboni umeendelea kufanyika. Vilevile, Ofisi ya Bunge
imewajengea uwezo Wabunge na Watumishi wake kupitia semina mbalimbali katika
masuala ya Utawala Bora. Katika mwaka 2014/2015, Ofisi ya Bunge itaendelea
kuratibu Mikutano ya Bunge, Vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge pamoja na
kuimarisha miundombinu na majengo ya Bunge.
Muungano
18.
Mheshimiwa Spika, tarehe 26 Aprili 2014,
tumeadhimisha Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Miaka 50 kwa lugha yoyote ile siyo kipindi
kifupi. Tumeweza kufika hapa tulipo
kutokana na misingi imara ya Muungano iliyowekwa na Waasisi wetu na kuendelezwa
na Viongozi walioongoza Taifa letu katika awamu zilizofuatia. Tunajivunia
kwamba Muungano wa Tanzania umejengeka kwenye historia ya muda mrefu ya
ushirikiano wa watu wa pande hizi mbili. Jamii hizi zina uhusiano wa damu,
kifikra na mapambano ya pamoja dhidi ya wakoloni waliotawala kwa vipindi
tofauti. Walichofanya waasisi wetu mwaka 1964 ni kurasimisha ushirikiano wetu
wa muda mrefu. Nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza Watanzania wote
kwa kuadhimisha Miaka 50 ya Muungano. Aidha, ninawashukuru kwa dhati Viongozi
wote walioongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar tangu kuasisiwa
kwa Muungano. Kwa namna ya pekee namshukuru Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali
Mohammed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa
Uongozi wao ambao umezifanya pande mbili za Muungano kuwa karibu zaidi.
19.
Mheshimiwa Spika, tumeadhimisha Miaka 50
ya Muungano tukiwa na takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012. Takwimu hizo zinaweka jambo moja wazi kwa
Muungano wetu; kwamba zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wote wamezaliwa baada ya Muungano. Hivyo, tuliozaliwa kabla ya Muungano ni chini
ya asilimia kumi. Kwa mujibu wa takwimu
hizo, Tanzania nzima ina watu 44,926,923.
Kati yao, watu 40,640,425, sawa na Asilimia 90.6 ni wa umri wa siku moja
hadi miaka 50. Kwa upande wa Tanzania
Bara, idadi ya watu
ilikuwa 43,625,354, kati ya hao, watu 39,456,065 sawa na asilimia
90.5 wamezaliwa baada ya Muungano. Kwa
upande wa Zanzibar kulikuwa na watu 1,303,569, ambapo watu 1,184,360 sawa na
asilimia 90.9 wamezaliwa baada ya Muungano.
Takwimu hizo zina maana kwamba, asilimia 90.6 ya watu wote wamezaliwa
ndani ya Muungano na nchi wanayoifahamu ni Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Sote tunawajibika kuwatendea
haki watu hawa kwa kuulinda, kuuimarisha na kuudumisha Muungano wetu.
20.
Mheshimiwa Spika, tuna kila sababu ya
kuadhimisha Miaka hii 50 ya Muungano kwa furaha. Katika maadhimisho ya mwaka huu, tuliandaa
maonesho maalum, makongamano na shughuli nyingine ambazo zilisaidia wananchi
kuelimishwa kuhusu masuala ya Muungano. Aidha, kimeandaliwa kitabu maalum
kinachoelezea historia, utekelezaji wa mambo ya Muungano, mafanikio, changamoto,
fursa na matarajio ya Muungano kwa miaka ijayo.
Kitabu hicho kitatumika kama rejea kwa kizazi chetu na vizazi vijavyo.
21.
Mheshimiwa Spika, tutaendelea kuulinda Muungano wetu kwa nguvu zote tukiwa na uelewa
kwamba, katika kipindi cha miaka 50 iliyopita Watanzania wameishi kwa amani na
kufanya kazi zao za kujiletea maendeleo wakiwa upande wowote wa Muungano.
Tunatambua changamoto zilizopo na tumeweka utaratibu mzuri wa vikao ili
kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo. Vikao hivyo vitaendelea kufanyika katika ngazi
ya wataalam, Watendaji Wakuu na Viongozi wa Kitaifa. Ni imani yangu kwamba,
Muungano huu utaendelea kudumu na watu watapata maendeleo makubwa kwani Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ina fursa nyingi zinazoweza kutumika kwa manufaa ya
wote. Sote tukumbuke kuwa, UTANZANIA WETU NI MUUNGANO WETU, TUULINDE, TUUIMARISHE NA KUUDUMISHA!
Mabadiliko ya Katiba
22.
Mheshimiwa Spika, tarehe 30 Desemba
2013, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikamilisha Rasimu ya Pili ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuikabidhi kwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt.
Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Napenda kuishukuru Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba
kwa kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rasimu
hiyo imeliwezesha Bunge Maalum la Katiba kuanza mjadala.
Nitumie fursa hii kuwashukuru Watanzania wote kwa kutoa maoni yaliyowezesha
Tume kuandaa Rasimu hiyo ya Katiba.
23.
Mheshimiwa Spika, Bunge Maalum la
Katiba linaundwa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Wabunge wa Baraza la Wawakilishi na Wajumbe 201 walioteuliwa kwa mujibu wa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011. Naomba nitumie fursa hii
kuwapongeza Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kwa kupata fursa hii ya
kuwawakilisha Watanzania katika kuandaa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Ni dhahiri kuwa dhamana hii ni
kubwa sana!
24.
Mheshimiwa Spika, Bunge Maalum la
Katiba lilianza kazi rasmi tarehe 18 Februari, 2014 kwa kumchagua Mheshimiwa
Pandu Ameir Kificho kuwa Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo. Nichukue fursa hii
kumpongeza Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho kwa kazi nzuri aliyoifanya ya
kulisimamia Bunge Maalum hadi kuwezesha kupatikana kwa Kanuni za kuliongoza
Bunge hilo. Aidha, niwapongeze Mheshimiwa Samwel John Sitta kwa kuchaguliwa
kuwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu Mwenyekiti wa
Bunge Maalum la Katiba. Nampongeza Katibu wa Bunge la Katiba Bwana Yahaya
Hamadi Khamis na Naibu wake Dkt. Thomas Kashililah pamoja na Wajumbe wote
waliochaguliwa kuwa Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati 12 za Bunge Maalum.
Baada ya kukutana kwa muda wa siku 67, Bunge Maalum limeahirisha Mkutano wake
tarehe 25 Aprili, 2014 ili kupisha majadiliano ya Mpango na Bajeti ya Serikali
kwa mwaka 2014/2015. Ni matumaini yangu kwamba, Bunge Maalum la Katiba
litakaporejea litakamilisha kazi hiyo kwa umakini na kupata Rasimu ambayo hatimaye
itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kura ya maoni.
Vitambulisho vya Taifa
25.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya Bajeti ya mwaka 2013/2014 nilielezea dhamira ya
Serikali ya kutoa Vitambulisho vya Taifa kwa Wananchi wake. Napenda kuliarifu
Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali imekamilisha usajili na utambuzi wa watu kwa
upande wa Zanzibar, Watumishi wa Umma na vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na
wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam. Serikali pia, imekamilisha ujenzi wa vituo vya
kuingiza na kuhakiki taarifa, kituo cha kutengeneza Vitambulisho na kuhifadhi
kumbukumbu pamoja na kituo cha uokozi na majanga ya taarifa na takwimu. Katika
mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea na
zoezi la Utambuzi na Usajili wa Watanzania katika Mikoa mingine ili kwa pamoja
tuweze kunufaika na Vitambulisho vya Taifa katika nyanja za kijamii, kiuchumi
na kiusalama.
Sensa ya Watu na Makazi
26.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2013/2014, Serikali imeendelea kutoa machapisho mbalimbali ya matokeo ya Sensa
ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Machapisho hayo yanajumuisha Taarifa ya
Mgawanyo wa Watu kwa Maeneo ya Utawala; Mgawanyo wa Watu kwa Umri na Jinsia na
Taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi. Taarifa hizo zimebaini
kuwa, katika miaka kumi iliyopita kumetokea mabadiliko makubwa ya kiuchumi na
kijamii katika nchi yetu. Kiwango cha watu wanaojua kusoma na kuandika
kimeongezeka kutoka asilimia 69 mwaka 2002 hadi asilimia 78 mwaka 2012. Aidha,
uandikishaji halisi katika shule za msingi umeongezeka kutoka asilimia 69 mwaka 2002 hadi 77 mwaka 2012.
Idadi ya watu wanaoishi kwenye nyumba zenye kuta imara ni asilimia 74 na
asilimia 65.4 wanaishi kwenye nyumba zilizoezekwa kwa bati. Hata hivyo, pamoja
na mafanikio hayo,
hali ya utegemezi
nchini ni kubwa kutokana na ukweli kuwa kati ya Watanzania Milioni 44.9,
Asilimia 50.1 ni watoto wenye umri chini ya miaka 18. Aidha, takwimu
zimebainisha kuwa Asilimia 7.7 ya Watanzania ni watoto yatima. Kutokana na hali
hiyo, ni jukumu letu kama Taifa kuweka mipango madhubuti ya kukabiliana na
changamoto hizo katika sekta za huduma za jamii ili hatimaye kila mwenye uwezo
wa kufanya kazi achangie ipasavyo katika kukuza uchumi na maendeleo ya nchi
yetu.
MASUALA YA UCHUMI
Hali ya Uchumi
27.
Mheshimiwa Spika, Pato la Taifa
katika mwaka 2013 lilikua kwa Asilimia 7.0 ikilinganishwa na ukuaji wa Asilimia
6.9 mwaka 2012. Ongezeko hilo limetokana na ukuaji mzuri wa shughuli za huduma
za mawasiliano, viwanda, ujenzi na huduma za fedha. Kutokana na ongezeko hilo,
wastani wa Pato la Mtanzania limeongezeka kutoka Shilingi 1,025,038 mwaka 2012
hadi Shilingi 1,186,424 mwaka 2013, sawa na ongezeko la Asilimia 15.7. Mfumuko
wa Bei umepungua kutoka Asilimia 9.8 Machi 2013 hadi Asilimia 6.1 Machi 2014.
Kupungua kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kupungua kwa kasi ya kupanda bei za
bidhaa na vyakula hasa mahindi, mchele na aina nyingine ya nafaka.
28.
Mheshimiwa Spika, pamoja na uchumi wetu kukua kwa kasi ya
asilimia 7.0 kwa mwaka 2013 na Pato la Mtanzania kuongezeka, kiwango hicho siyo
kikubwa sana kuwezesha umaskini wa wananchi kupungua kwa kasi. Utafiti wa kitaalam unaonesha kwamba, ili
umaskini upungue kwa kasi kubwa, uchumi unatakiwa kukua kwa zaidi ya Asilimia 8
kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo.
Ukuaji huo pia unatakiwa kulenga Sekta ambazo zinagusa maisha ya watu
wengi, hususan kilimo, mifugo na uvuvi. Mwelekeo wa Serikali ni kuweka
mazingira wezeshi kwa Sekta za kipaumbele kukua kwa kushirikisha Sekta Binafsi.
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
29.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/2012 – 2015/2016 ambao unatekelezwa
katika kipindi cha mwaka mmoja mmoja. Katika mwaka 2013/2014, Serikali
ilitekeleza Mpango huo kupitia Kauli mbiu ya Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa.
Msingi wa kauli mbiu hii ni kuainisha maeneo machache
ya kimkakati na
kuyatengea rasilimali za kutosha,
kusimamia na kufuatilia utekelezaji kwa karibu zaidi. Chombo maalum cha
Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi
ya kimkakati chini
ya Ofisi ya Rais kinachojulikana
kama President’s Delivery Bureau –
(PDB) kimeanzishwa na Watendaji Wakuu wameteuliwa. Ninapenda kuliarifu Bunge
lako Tukufu kwamba, matunda ya utekelezaji wa Mfumo huo yameanza kuonekana
katika maeneo makuu sita ya kipaumbele kitaifa ambayo ni Nishati ya Umeme,
Uchukuzi, Kilimo, Elimu, Maji na Ukusanyaji wa Mapato. Utekelezaji wa miradi hiyo na mafanikio
yaliyoanza kupatikana yatatolewa maelezo na Mawaziri katika Sekta husika.
Maendeleo ya Sekta Binafsi na Uwekezaji
30.
Mheshimiwa Spika, njia ya uhakika ya
kuliwezesha Taifa kuwa na uchumi imara na wa kisasa utakaohimili ushindani
katika masoko ya Kikanda na Kimataifa ni kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji.
Katika kufikia azma hiyo, tarehe 31 Januari, 2014 nilizindua rasmi Taarifa ya
Tathmini ya Sera, Sheria na Kanuni mbalimbali zinazosimamia Uwekezaji Tanzania.
Mapendekezo ya Taarifa hiyo yatatumika kuihuisha Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya
mwaka 1996 pamoja na Sheria ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka 1997. Aidha, ili
kuwawezesha Wawekezaji na Wafanyabiashara kupata huduma na taarifa zote muhimu kama vile Sheria,
Kanuni na Taratibu mbalimbali kuhusu biashara na uwekezaji kwa njia ya mtandao,
Serikali imezindua upya Tovuti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania. Kupitia Tovuti hii, Wawekezaji popote duniani
wanaweza kupata taarifa kuhusu usajili wa Kampuni
na viwango vya
kodi kwa njia
ya mtandao.
Dhamira ya Serikali
ni kuboresha mazingira ya uwekezaji na kupunguza gharama za kufanya biashara
nchini ili kukabiliana na ushindani mkubwa kutoka nchi nyingine zilizotekeleza
maboresho ya mifumo yao ya udhibiti wa biashara.
31.
Mheshimiwa Spika, Sekta Binafsi
inaendelea kupewa nafasi kubwa katika kukuza uchumi Nchini. Takwimu zinaonesha
kwamba, Miradi iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania imeongezeka kutoka
869 yenye thamani ya Shilingi Bilioni
31.5 mwaka 2012 hadi miradi 885
yenye thamani ya
Shilingi Bilioni 141.2 mwaka
2013.
Napenda pia kuliarifu
Bunge lako Tukufu kwamba Nchi nyingi duniani zinaendelea kuiamini Tanzania kama
Kituo maarufu cha uwekezaji Duniani. Mwezi Novemba, 2011 nilizindua Mpango wa
Ushirikiano kati ya Tanzania na Uingereza unaojulikana kama Partnership in
Prosperity. Mpango huo umelenga kuongeza uwekezaji kutoka Sekta Binafsi ya
Uingereza kwenye mafuta na gesi, kilimo na Nishati jadidifu. Lengo ni kuongeza
uwekezaji kutoka Nchi hiyo kwa zaidi ya maradufu ya kiwango cha sasa. Aidha,
tumekubaliana kushirikiana kuimarisha mazingira ya biashara ili kurahisisha
uwekezaji katika sekta hizo.
32.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya Kampuni za
Uingereza tayari zimeanza kutekeleza makubaliano hayo kwenye Sekta ya
kilimo. Kampuni ya Unilever kwa mfano,
itawekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 275 kwenye kilimo cha chai kwa kushirikiana
na wakulima wadogo. Tayari Kampuni hiyo imeanza kupanua Kiwanda cha Chai
Kibwele, Mufindi na kufungua zaidi ya Hekta 300 za mashamba ya chai katika
Wilaya ya Mufindi. Aidha, Kampuni hiyo imeingiza nchini vipando 250,000 vya
miche bora ya chai. Pia, Kampuni inaandaa zaidi ya miche milioni 2 kwa ajili ya
kuwagawia wakulima wadogo Wilayani Njombe ili waongeze uzalishaji wa chai
Nchini.
33.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2013/2014, Kituo cha Uwekezaji
kimeshirikiana na Uongozi wa Mikoa mbalimbali Nchini kuratibu maandalizi ya
Makongamano ya Uwekezaji yenye lengo la kuhamasisha, kukuza na kutangaza fursa
mbalimbali za uwekezaji zilizopo kwenye Mikoa hiyo. Jumla ya Mikoa 11
imeshiriki kikamilifu kuandaa na
kufanikisha Makongamano ya Uwekezaji katika maeneo yao. Mikoa
hiyo ni
Mwanza, Mara, Kagera, Geita,
Simiyu, Shinyanga, Tabora, Manyara, Tanga, Kilimanjaro na Arusha. Makongamano
hayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuzitangaza fursa za uwekezaji zilizopo
kwenye Mikoa hiyo, pamoja na kuihamasisha Mikoa na Halmashauri za Wilaya ndani
ya Mikoa hiyo kuainisha na kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji. Aidha,
Wawekezaji wengi walioshiriki kwenye Makongamano hayo wameonesha nia na utayari
wa kuwekeza kwenye Mikoa husika. Jitihada hizi zitaendelezwa katika kipindi
kijacho.
Majadiliano na Sekta Binafsi
34.
Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba yangu
ya Bajeti mwaka 2013/2014, nilieleza kuhusu Mkutano wa Kimataifa wa Majadiliano
ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote. Mkutano huo ulifanyika kuanzia tarehe 28
Juni hadi tarehe 1 Julai 2013, Jijini Dar es Salaam chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkutano
huo ulitoa fursa ya kipekee kwa Viongozi wa Serikali kujadiliana na kupata
maoni ya makundi mbalimbali ya Wananchi kuhusu mbinu za kuongeza kasi ya
maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Serikali imedhamiria kufanya Majadiliano ya
Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote kila mwaka kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi
Taifa kwa kuzingatia fursa kubwa za maendeleo shirikishi zilizopo kwenye maeneo
husika.
35.
Mheshimiwa Spika, Baraza la Taifa la
Biashara lilifanya Mkutano wake wa Saba tarehe 16 Desemba 2013 chini ya Kauli
Mbiu ya “Ukuaji Shirikishi wa Uchumi”. Maazimio ya Mkutano huo ni pamoja na
kuunda Kamati Tatu ambazo zitashughulikia Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi,
Mazingira Wezeshi ya Biashara na Matumizi Endelevu ya Maliasili za nchi. Kamati
ya Mazingira Wezeshi ya Biashara imeanza kuishauri Serikali kuhusu mikakati ya
kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania. Kazi hiyo imefanyika
kwa utaratibu wa Maabara chini ya Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa.
Utaratibu huo ulianzisha maeneo sita muhimu ambayo yakishughulikiwa yataboresha
mazingira ya biashara nchini. Maeneo hayo ni kuboresha Kanuni na Taasisi
zinazosimamia biashara; upatikanaji wa ardhi na haki za umiliki wake na
kuimarisha ukusanyaji wa kodi na kupunguza
wingi wa kodi na tozo mbalimbali. Maeneo
mengine ni kuzuia na kupambana na rushwa; kuboresha Sheria za Kazi na
kuimarisha mafunzo na stadi za kazi pamoja na kusimamia utekelezaji wa mikataba
na utawala wa sheria. Katika mwaka
2014/2015, Baraza la Taifa la Biashara
litaendelea kuratibu utekelezaji wa maazimio hayo ya Mkutano wa Saba
sanjari na kusimamia mikutano ya Mabaraza ya Wilaya na Mikoa.
UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
36.
Mheshimiwa Spika, dhamira
ya Serikali ya kubuni na kutekeleza Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya
mwaka 2004 ni kuhakikisha kwamba Watanzania wananufaika na rasilimali za nchi yao badala ya kubaki kuwa watazamaji. Kwa kutambua umuhimu wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi,
katika Mwaka 2013/2014 Serikali imeanzisha Taasisi
ya Ujasiriamali na Ushindani wa
Kibiashara (Tanzania Entrepreneurship Competitiveness Centre).
Taasisi hiyo itatekeleza jukumu la kutoa miongozo ya uandaaji wa mitaala ya
ujasiriamali katika ngazi tofauti na kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa bora
zitakazohimili ushindani. Aidha, Serikali imeendelea kusimamia Mifuko ya
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na kuongeza ufanisi wake. Hadi kufikia mwezi
Februari 2013, Mfuko wa Uwezeshaji wa Mwananchi ulikuwa umepokea Shilingi
Bilioni 2.1 zilizotumika kudhamini mikopo ya wajasiriamali kupitia Benki ya
CRDB kwa makubaliano ya kukopesha mara tatu ya dhamana ya Serikali. Kutokana na
makubaliano hayo, hadi kufikia mwezi Desemba 2013, mikopo yenye thamani ya
zaidi ya Shillingi Bilioni 9.5
ilikuwa imetolewa kwa Wajasiriamali 9,790 waliojiunga kwenye Vikundi 283 na Vyama vya Akiba na Mikopo
(SACCOS) 51 katika Mikoa 12 na Wilaya 27.
37.
Mheshimiwa
Spika, Kwa upande wa Mfuko wa Kuendeleza
Wajasiriamali Wadogo na wa Kati, hadi kufikia Desemba 2013, ulikuwa
umetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi
Bilioni 36.39 kwa
Wajasiriamali 62,720. Aidha,
Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ulikuwa
umetoa mikopo kwa Vijana yenye
thamani ya Shilingi
Bilioni 1.22 kupitia SACCOS 244;
na Mfuko wa Maendeleo ya
Wanawake ulikuwa umetoa
mikopo yenye thamani
ya Shilingi Bilioni
5.44 kwa Wanawake
500,000 Nchini. Vilevile, Mradi
wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo (SELF) ulikuwa umetoa mikopo yenye thamani
ya Shilingi Bilioni 57.1 kupitia Asasi 375 za Kifedha ambapo Wajasiriamali
95,034 walinufaika.
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF
38.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Awamu
ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III) inatekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini zilizo katika
Mazingira Hatarishi Tanzania Bara na Zanzibar.
Katika kutekeleza Mpango huo, utaratibu wa uhawilishaji
fedha kwa kaya maskini ulifanyika katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 22 ambapo
kaya 138,032 katika Vijiji na Shehia 1,179 zilitambuliwa na kuandikishwa katika
Mfumo wa Masijala wenye walengwa 464,552. Hadi sasa, Shilingi Bilioni 5.5
zimehawilishwa katika kaya hizo. Lengo ni kuziwezesha kaya hizo kupata chakula na kujiongezea fursa ya kipato.
39.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imejenga uwezo kwa Viongozi na Wataalam
kutoka maeneo ya utekelezaji wa Mpango huo. Uwezo umejengwa kwa kutoa mafunzo
katika masuala ya utambuzi, uandikishaji na ukusanyaji taarifa za kaya maskini.
Aidha, mafunzo ya usanifu wa miradi ya ujenzi yalitolewa kwa wataalam kutoka
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Pia, Wajumbe 17 wa Baraza la Wawakilishi na Wakuu
wa Mikoa na Wilaya kutoka Zanzibar walitembelea Vijiji vya Pongwe-Kiona na
Malivundo (Bagamoyo) na Gwata (Kibaha) ili kujifunza kuhusu utekelezaji bora wa
Mpango huo. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kufanya utambuzi na
uandikishaji wa kaya maskini kufikia maeneo yote 161 ya utekelezaji wa Mpango
Tanzania Bara na Zanzibar. Lengo ni kutambua na kuandikisha Kaya 920,000 kutoka
Vijiji, Mitaa na Shehia 9,000.
UZALISHAJI MALI
Uzalishaji wa Mazao
40.
Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji
wa chakula ni ya kuridhisha katika maeneo mengi nchini kufuatia mavuno mazuri
ya msimu wa 2012/2013. Uzalishaji wa mazao ya chakula kwa
msimu huo ulikuwa Tani Milioni 14.38 ikilinganishwa na mahitaji ya chakula ya
Tani 12.15 kwa mwaka 2013/2014 ikiwa ni ziada ya Tani Milioni 2.3 za chakula.
Ongezeko hilo limefanya Taifa kujitosheleza kwa
chakula kwa Asilimia 118 na hivyo, kufanya wastani wa bei za mazao ya chakula katika masoko Nchini kuwa za chini
katika kipindi chote cha mwaka 2013/2014.
Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo
41.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea
na juhudi za kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara
kulingana na Mipango inayotekelezwa chini ya Kaulimbiu ya KILIMO KWANZA, na
Mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa. Katika mwaka 2013/2014, Serikali
imesambaza jumla ya vocha za ruzuku 2,796,300 zenye thamani ya Shilingi Bilioni
83 kwa ajili ya mbolea na mbegu bora za mpunga na mahindi kwa Kaya 932,100.
Pia, Serikali ilitoa ruzuku ya dawa za korosho kiasi cha lita 158,845 na Tani
620 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.5. Vilevile, ruzuku ilitolewa kwa ajili
ya uzalishaji wa mbegu bora za pamba Tani 4,000 zenye thamani ya Shilingi
Bilioni 4.8, miche ya kahawa 350,000 yenye thamani ya Shilingi Milioni 100 na
miche ya chai 1,850,000 yenye thamani ya Shilingi Milioni 300.
42.
Mheshimiwa Spika, ongezeko la tija
katika uzalishaji wa mazao unategemea sana huduma bora za ugani kwa wakulima.
Serikali katika mwaka 2013/2014, ilitoa kibali cha kuajiri Maafisa Ugani 1,452
ili kufanikisha
kufikiwa kwa malengo ya kuwa na Afisa Ugani wa Kilimo mmoja kwa kila kijiji.
Vilevile, Serikali
imeongeza Mashamba Darasa kutoka 16,330 yenye wakulima 344,986
mwaka 2012/13 hadi 16,543
yenye wakulima 345,106 mwaka 2013/2014
ili kuimarisha utoaji wa mafunzo kwa wakulima.
43.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea
kushirikisha Washirika wa Maendeleo kuchangia Programu ya
Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT). Miongoni mwa
malengo ya Programu hiyo ni kuwaunganisha
wakulima wadogo na mnyororo wa thamani wa kibiashara wa Makampuni makubwa ya
ndani na nje ya nchi. Ili kufikia lengo hilo, Serikali imeanzisha Mfuko
Chochezi wa Uendelezaji wa Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT
Catalytic Trust Fund). Mfuko
huo utatoa mitaji itakayogharamia hatua za awali za miradi inayotoa tija ya
haraka ambayo imebainishwa kwenye Mpango Mkakati wa Uwekezaji. Vilevile, Mfuko
huo utahamasisha biashara inayolenga kumuinua Mkulima mdogo kwa kumuunganisha
na mnyororo wa thamani na kampuni kubwa kupitia madirisha makuu mawili. Dirisha
la kwanza ni Matching Grant Fund
linalolenga kuwezesha kampuni kubwa zilizoanzisha biashara ya Kilimo
Nchini, kuimarisha minyororo ya thamani inayowahusisha wakulima wadogo zaidi au
kuanzisha kilimo cha Mkataba kati ya wakulima wakubwa na wakulima wadogo.
Dirisha la pili ni Social Venture Capital Fund, linalolenga kuziwezesha
biashara changa na za kati kwenye Sekta ya Kilimo au kuwezesha Kilimo cha
mkataba kati ya wakulima wakubwa na wakulima wadogo. Tayari Bodi ya Mfuko
imeteuliwa na Mtendaji Mkuu wa Mfuko ameajiriwa.
44.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali kupitia Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo
Makubwa, inategemea kuvutia uwekezaji na kuanzisha Kilimo cha mashamba makubwa
25 ya Kilimo cha kibiashara kwa mazao ya mpunga na miwa kwa utaratibu wa
kuwaunganisha wakulima wakubwa na wadogo wanaozunguka mashamba hayo. Aidha,
itaanzisha, itaboresha na kuendesha kitaalamu maghala 275 ya kuhifadhi mahindi
kwa kuwaunganisha wakulima katika umoja wa kibiashara kwa ajili ya kupata
masoko ya pamoja.
Umwagiliaji
45.
Mheshimiwa Spika, katika juhudi za
kuendeleza Kilimo cha umwagiliaji Nchini, Sheria ya Umwagiliaji Namba 5 ya
mwaka 2013 imeanza kutumika Mwezi Januari, 2014. Sheria hiyo itaiwezesha
Serikali kuanzisha Tume ya Umwagiliaji ambayo ni chombo cha kitaifa chenye
dhamana ya kusimamia, kuendeleza na kudhibiti shughuli za Umwagiliaji Nchini.
Sheria hiyo pia itaanzisha Mfuko wa Taifa wa Umwagiliaji utakaosaidia
kutekeleza mipango ya umwagiliaji kwa kulipia gharama za umwagiliaji
zinazofanywa na mkulima mmoja mmoja na wawekezaji kupitia mikopo na dhamana.
Serikali pia iliendelea na ujenzi na ukabarati wa skimu 24 za umwagiliaji
zilizopo katika wilaya 15 Nchini. Katika mwaka 2014/2015,
Serikali itaendeleza
Skimu za Umwagiliaji 39 kwa ajili ya Kilimo cha mpunga.
Miundombinu ya Masoko ya Mazao
46.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2013/2014, Serikali kupitia Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji
Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini imekarabati kilometa
352 za barabara za vijijini kwa kiwango cha changarawe katika Halmashauri za
Iringa Vijijini, Njombe Vijijini, Singida Vijijini, Mbarali, Lushoto, Same,
Mbulu, Msalala na Mpanda. Halmashauri nyingine ni Maswa, Songea Vijijini,
Rufiji, Karatu na Kwimba. Vilevile, imejenga maghala matano yenye uwezo wa
kuhifadhi tani 1,000 za mazao kila moja katika halmashauri za Iringa Vijijini,
Njombe Vijijini, Same, Songea na Mbarali na kukarabati maghala matatu katika
Halmashauri za Sumbawanga, Mbulu na Kahama. Aidha, Programu hiyo imezijengea
uwezo benki tisa za wananchi/ushirika ili kuimarisha mfumo wa kifedha Vijijini.
47.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2014/2015, Serikali kupitia Programu hiyo imepanga kukarabati kilometa 434 za
barabara kwa kiwango cha changarawe, kujenga maghala 14 na masoko saba katika Halmashauri 64 za Tanzania Bara na Wilaya 10 za Zanzibar. Aidha, wazalishaji wadogo kutoka Mikoa 24 ya Tanzania Bara na Mikoa mitano ya Zanzibar watajengewa uwezo wa kuhifadhi mazao
na mbinu za kufikia masoko ambapo zaidi ya wananchi 100,000 watanufaika na
mafunzo hayo.
Maendeleo ya Ushirika
48.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ushirika
Namba 6 ya mwaka 2013 imetungwa na imeanza kutumika Mwezi Januari, 2014. Sheria
hiyo itawezesha kuanzishwa kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika ambayo itakuwa na majukumu ya kusimamia
moja kwa moja Vyama vyote vya Ushirika. Aidha,
kupitia Sheria hiyo, Serikali imetoa Waraka Namba 1 wa mwaka 2014
unaotoa ufafanuzi kuhusu Chaguzi katika Vyama vya Ushirika. Ili kuondoa
migogoro ya kimaslahi, Waraka huo umewaondoa Viongozi wa Siasa na Serikali katika uongozi wa Vyama vya Ushirika katika ngazi zote. Katika
mwaka 2014/2015, Serikali itaimarisha uratibu wa Vyama vya Ushirika kulingana na mahitaji ya Wananchi na kuunganisha Vyama
vya Ushirika na Taasisi za fedha ili kuboresha utoaji wa huduma za kifedha kwa
Vyama vya Ushirika.
Maendeleo ya Sekta ya Mifugo
49.
Mheshimiwa Spika, kupitia Mpango wa
Ruzuku ya dawa ya kuogeshea mifugo, Serikali ilitoa jumla ya lita 11,020 zenye
thamani ya Shilingi Milioni 181.8 na kusambazwa nchini. Vilevile, ilitoa chanjo
kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mifugo ambapo dozi 150,000 za chanjo ya Ugonjwa
wa Homa ya Bonde la Ufa zenye thamani ya Shilingi milioni 119 ilitolewa katika
Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga na Dodoma. Vilevile, Serikali
imeimarisha Kituo cha Uhamilishaji kilichopo katika eneo la Usa River, Arusha
pamoja na Vituo vingine vitano vya Kanda kwa kusimika mitambo ya kuzalisha
kimiminika cha naitrojeni na kujenga Vituo vitano vya madume bora. Vilevile,
ng’ombe walionenepeshwa wameongezeka kutoka 132,246 mwaka 2011/2012 hadi
kufikia 175,000 mwaka 2013/2014. Ili kuboresha upatikanaji wa maziwa Nchini,
Serikali imeongeza uzalishaji mitamba katika mashamba yake kutoka mitamba 943
kwa mwaka 2012/2013 hadi mitamba 1,046 mwaka 2013/2014 na kusambaza Mbuzi wa
maziwa 9,530 kupitia Mpango wa Kopa Mbuzi lipa Mbuzi. Jitihada hizi, zimesaidia
wafugaji kuongeza tija na hivyo kuchangia ongezeko la uzalishaji wa maziwa
kutoka lita Bilioni 1.9 mwaka 2012/2013 hadi lita Bilioni 2 mwaka 2013/2014.
50.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2014/2015, Serikali itatoa ruzuku ya dawa za kuogesha mifugo na kununua dozi
milioni moja kwa ajili ya chanjo ya ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa kwa Mikoa
ya Arusha, Tanga, Tabora na baadhi ya mikoa katika Kanda ya Ziwa. Vilevile,
Serikali itaimarisha Vituo vya uhamilishaji, mashamba ya kuzalisha mifugo bora
na yale yanayozalisha mbegu bora za mifugo pamoja na kununua mifugo wazazi.
Maendeleo ya Sekta ya Uvuvi
51.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2013/2014, Serikali kwa kushirikiana na wadau ilihuisha Sera ya Taifa ya Uvuvi
ya mwaka 1997 na Sheria ya Uvuvi Namba 22 ya mwaka 2003 ili ziendane na
mabadiliko ya kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia. Katika kuimarisha ufugaji wa
samaki, wakulima 2,604 walipewa mafunzo ya ufugaji bora wa samaki na mabwawa 64
yalichimbwa. Hatua hiyo imeongeza idadi ya mabwawa ya Samaki kufikia 20,198
yenye uwezo wa kuzalisha Tani 3,029.7 za samaki ikilinganishwa na mabwawa
20,134 yaliyokuwepo mwaka 2012/2013.
Vituo vya kuzalisha vifaranga wa samaki kwa wingi kwa kutumia teknolojia
ya ndani viliongezeka kutoka kituo
kimoja mwaka 2012/2013 hadi kufikia vituo
vitano mwaka 2013/2014 vyenye uwezo wa kuzalisha vifaranga bora vya samaki
Milioni 10 kwa mwaka. Serikali pia, ilijenga matanki sita yenye lita za ujazo
8,000 kila kimoja kwa ajili ya kuzalisha vifaranga vya samaki.
52.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015,
Serikali itaanzisha Vituo vya kuzalishia vifaranga vya samaki katika maeneo ya
Bacho Dareda - Manyara, Hombolo – Dodoma, na Kigoma. Vilevile, itajenga bwawa
la kufuga samaki katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo cha Kilimanjaro – KATC; na
kutoa ruzuku kwa ajili ya kuchimba mabwawa na kuzalisha vifaranga wa samaki.
Ufugaji Nyuki
53.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya ufugaji
nyuki imeendelea kuimarika na kuchangia kuongeza ajira na kupunguza umaskini.
Mwaka 2013, thamani ya mauzo ya asali
nje yalifikia Shilingi Milioni 287.3 ikilinganishwa na mauzo ya Shilingi
Milioni 262 mwaka 2012. Katika kipindi hicho, jumla ya
Tani 384 za nta zenye thamani ya Shilingi Milioni 4,660 ziliuzwa nje
ikilinganishwa na Tani 277 zenye thamani ya Shilingi Milioni 2,583 zilizouzwa
mwaka 2012. Nchi zilizoongoza katika ununuzi wa Asali na Nta ya Tanzania ni
Ujerumani, Oman, China, Japan, Yemen, India, Ubelgiji, Botswana, Kenya na
Marekani. Kutokana na maendeleo haya mazuri
katika mwaka 2013/2014, Serikali imetenga maeneo 20 yenye ukubwa wa
Hekta 58,445 sehemu mbalimbali Nchini kwa ajili ya hifadhi za nyuki. Aidha, imetoa mafunzo kwa wafugaji nyuki 924 na vikundi 49 kutoka Wilaya 12 pamoja na kutoa elimu ya
miongozo na sheria za ubora wa mazao ya nyuki kwa wafanyabiashara wa mazao ya nyuki.
54.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Tanzania ilishiriki kwenye Kongamano la Ufugaji nyuki lililofanyika Kiev, Ukraine. Katika Kongamano hilo, mazao
ya nyuki kutoka Tanzania yalikuwa kivutio kikubwa na yaliwezesha kupata medali
ya Banda Bora la Asali kutokana na asali yake kuwa na viwango vya ubora
na usalama vinavyokubalika Kimataifa. Aidha, kampuni
mbalimbali zilionesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya ufugaji nyuki Nchini. Kama ambavyo nimesisitiza mara kwa mara, sekta ya nyuki ina fursa kubwa ya kibiashara hapa nchini na nje ya nchi. Ni sekta inayoweza kuleta mapinduzi makubwa
katika maeneo mengi kwani yanahitajika mafunzo kidogo na vifaa vichache ambavyo
vinaweza kutumika kikamilifu
kupata
asali na mazao yake.
Niendelee kusisitiza kwamba, tuwahimize wananchi katika Majimbo yetu watumie fursa za ufugaji nyuki zinazopatikana
katika maeneo yao ili kujiongezea kipato.
Maendeleo ya Viwanda
55.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Viwanda
Vidogo na Biashara Ndogo imeendelea kutoa mchango muhimu katika upatikanaji wa
ajira, ongezeko la kipato na ukuaji wa uchumi. Katika mwaka 2013/2014, Serikali
imefungua Vituo vya Teknolojia Mikoani kwa ajili kuhudumia Wajasiriamali
wanaotengeneza mashine za kusindika mazao na kutengeneza bidhaa mbalimbali za
uzalishaji mali. Vituo hivyo vimewezesha kuanzishwa kwa miradi mipya 4,127 ya
uzalishaji mali kwenye mikoa ya Lindi, Mbeya, Iringa, Arusha, Kigoma na
Kilimanjaro. Aidha, Wajasiriamali 23,546 walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali na
ujuzi maalum wa ufundi na utumiaji wa mashine za uzalishaji mali. Vilevile,
huduma za ushauri na ugani zilitolewa kwa Wajasiriamali 20,769 kwenye Vikundi
na Vyama vyao vya Biashara kwa kuviimarisha na kuviwezesha kujenga misingi ya
kujitegemea.
56.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza
Mkakati wa “Wilaya Moja, Bidhaa Moja” kwa kujenga uwezo wa kuzalisha bidhaa kutokana
na malighafi zilizopo kwenye Wilaya husika. Kupitia Mkakati huo, Serikali
imejenga uwezo wa kuongeza thamani ya mazao na bidhaa mbalimbali, kuzalisha
mitambo na vipuri pamoja na zana za kilimo ambapo viwanda vidogo 198
vilianzishwa na kuwezesha upatikaji wa ajira 1,809. Aidha, Serikali inatekeleza
Mradi wa Kuendeleza Ujasiriamali Vijijini (MUVI) kwa kutumia dhana ya
kuimarisha mlolongo wa thamani kimikoa kwa mazao mbalimbali. Mradi umewezesha
uanzishwaji wa miradi midogo 15,580 Vijijini; urasimishaji wa Vikundi 65,308
vya uzalishaji na upatikanaji wa ajira 39,574.
57.
Mheshimiwa
Spika, Serikali pia iliendelea na juhudi za kuhamasisha uwekezaji
kwenye miradi mipya katika Maeneo Maalum ya Uzalishaji (Export Processing
Zones) na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (Special Economic Zones). Hadi kufikia
mwezi Desemba 2013, kampuni 32 zilikuwa zimesajiliwa na Mamlaka ya EPZ kwa
ajili ya kuanzisha viwanda vipya kwenye maeneo hayo. Aidha, Serikali
imekamilisha utafiti kwenye Mradi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma na kuthibitisha
uwepo wa tani Milioni 370 za makaa ya mawe katika eneo la kilomita za mraba 30
kati ya kilomita za mraba 140 zilizotengwa kwa ajili ya Mradi huo. Aidha,
utafiti huo ulithibitisha uwepo wa tani Milioni 219 za madini ya chuma katika eneo la kilomita za mraba 10
kati ya kilomita za mraba 166 zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo. Ujenzi wa
mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma na madini
ya chuma Liganga unatarajiwa kuanza mwaka 2014 na
kukamilika mwaka 2018. Katika mwaka 2014/2015,
Serikali itajielekeza
katika kuendeleza viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za kilimo.
Aidha, itaendelea kujenga Mradi wa Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na Ngaka na Mradi
wa Chuma Liganga.
Sekta ya Utalii
58.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutangaza fursa za utalii zilizopo nchini kwa kutumia mbinu
mbalimbali kama vile vipeperushi, majarida, matangazo ya Televisheni na kutumia
Balozi za Tanzania zilizoko nje ya nchi. Mbinu nyingine zilizotumika ni kutumia
maonesho ya Kimataifa na kuweka matangazo kwenye
viwanja sita vya Ligi Kuu ya Mpira wa Miguu ya Uingereza. Pamoja na matangazo
hayo, huduma
za kitalii hususan hoteli, miundombinu ya barabara na mawasiliano zimeimarishwa
na hivyo kuwashawishi watalii wengi kutembelea nchini. Kutokana na hatua hizo, idadi ya watalii
walioingia nchini imeongezeka kutoka Watalii 1,077,058 mwaka 2012 hadi
1,135,884 mwaka 2013, sawa na ongezeko la Asilimia 5.46. Watalii hao
wameliingizia Taifa Dola za Marekani Bilioni 1.8 ikilinganishwa na Dola za
Marekani Bilioni 1.7 zilizopatikana mwaka 2012. Vilevile, Serikali imeanzisha
utalii wa usiku katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara; utalii wa kuangalia
wadudu katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo na Hifadhi ya Amani; utalii wa makasia
katika Hifadhi ya Arusha – Ziwa Momela na Utalii wa kutembea katika Hifadhi za
Mahale na Gombe.
59.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa
kushirikiana na Sekta binafsi kupitia Baraza la Taifa la Biashara, imeandaa
mkakati maalum wa kukuza sekta ya utalii hasa kuondoa vikwazo vinavyokwamisha
kasi ya ukuaji wa sekta hii. Aidha, katika kukuza utalii wa ndani, Serikali inatumia fursa za maonesho na matamasha mbalimbali ya ndani
kuelezea vivutio vya utalii na imeandaa kijitabu cha utalii wa Utamaduni kwa
lengo la kutangaza vivutio vya utalii. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itatafsiri
tovuti ya Bodi ya Utalii pamoja na vielelezo mbalimbali kwa lugha za Kifaransa,
Kijerumani, Kichina na Kihispaniola ili zitumike kutangaza utalii kwa nchi
zinazotumia lugha hizo. Hatua hiyo
itasaidia kupanua wigo wa utalii katika masoko hayo yenye fursa kubwa.
Wanyamapori
60.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inaendelea na juhudi za kuhifadhi wanyamapori katika Hifadhi na Mapori ya
Akiba Nchini kwa nia ya kuwalinda na kuendeleza utalii. Katika mwaka 2013/2014,
Serikali imeendesha doria mbalimbali ndani na nje ya hifadhi zilizowezesha
kukamatwa watuhumiwa 391 pamoja na silaha 73 zikiwemo bunduki 22 za kivita.
Jumla ya kesi 277 zilifunguliwa ambapo kesi 123 zimemalizika na kesi 154
zinaendelea. Vilevile, katika kuhamasisha wananchi wanaoishi kando kando ya hifadhi
hizo kuzilinda, Halmashauri 38 zenye vitalu vya uwindaji zilipatiwa Shilingi
Bilioni 8.7 kama mgawo wa Asilimia 25 ya fedha zinazotokana na uwindaji wa
kitalii kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya wananchi.
61.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2014/2015, Serikali itaanza utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na
Ujangili. Mkakati huo umeainisha uwezo tulionao, upungufu uliopo na mahitaji
muhimu ambayo yataimarisha uhifadhi Nchini na kupunguza migongano iliyopo ya
matumizi ya ardhi. Vilevile, itaanzisha Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania
itakayosimamia shughuli zote zinazohusu uhifadhi wa wanyamapori ikiwa ni pamoja
na kukusanya mapato, kuendeleza hifadhi na kuimarisha ulinzi wa wanyamapori.
Sekta ya Madini
62.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2013/2014, Serikali imeimarisha ukaguzi kwenye uzalishaji na biashara ya
madini. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuweka Wakaguzi katika migodi yote
mikubwa na baadhi ya mitambo ya uchenjuaji madini. Aidha, imeanzisha dawati
maalum la kukagua madini yanayosafirishwa nje ya Nchi kupitia viwanja vya ndege
ili kudhibiti utoroshaji wa madini. Kutokana na jitihada hizo, madini ya
dhahabu na vito yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.9 yalikamatwa na
kuwasilishwa kwenye vyombo husika kwa hatua za kisheria.
63.
Mheshimiwa Spika, Serikali inathamini
mchango wa Wachimbaji Wadogo wa Madini katika kukuza uchumi wa Nchi yetu.
Katika mwaka 2013/2014, Serikali imewajengea uwezo wachimbaji wadogo kwa
kuwapatia mafunzo na mikopo ili kuongeza uzalishaji. Kutokana na juhudi hizo,
jumla ya kilo 237 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi Bilioni 14.5
zilizalishwa na kuingiza mrabaha wa Shilingi Milioni 519. Aidha, Serikali
imetenga maeneo mapya ya uchimbaji ya Isamilo na lwenge (Geita); Rwabasi
(Butiama) na Saza na Itumbi “B” (Chunya). Jitihada hizo zimefanya shughuli za
wachimbaji wadogo hasa katika uchenjuaji wa madini ya dhahabu kukua.
64.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2014/2015, Serikali itakamilisha Mkakati wa utekelezaji wa Sera ya Madini ya
mwaka 2009, Sheria ya Uongezaji Thamani Madini na Sheria ya Baruti pamoja na
Kanuni zake. Serikali pia itahamasisha uwekezaji kwenye sekta ya Madini na
kuziwezesha taasisi zake kama vile Tanzania Extractive Industrials Transporency
Initiatives (TEITI) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili ziweze kufanya
kazi kwa ufanisi. Vilevile, itatenga maeneo zaidi kwa ajili ya wachimbaji
wadogo na kuwawezesha kupata mitaji na teknolojia. Pia, itaboresha Mfumo wa
utoaji na usimamizi wa leseni za madini kwa kuanzisha huduma za kuomba leseni
kwa njia ya mtandao.
HUDUMA ZA KIUCHUMI
Ardhi
65.
Mheshimiwa Spika, ardhi ni msingi na kichocheo
muhimu cha maendeleo ikiwa itapangiwa matumizi bora, itapimwa na kusimamiwa
ipasavyo. Ili kufanikisha azma hiyo, Serikali
inachukua hatua madhubuti
kuhakikisha kuwa kila kipande
cha ardhi Nchini kinapangwa,
kupimwa, kumilikishwa na kutumiwa kwa mujibu wa Sheria. Katika
mwaka 2013/2014, Serikali imekamilisha sehemu ya kwanza ya ujenzi wa Mfumo
Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi (Integrated Land Management
Information System) na kurahisisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji
na matumizi mengine. Sambamba na hatua hiyo, Serikali inaboresha utunzaji wa
kumbukumbu za upimaji Ardhi kwa kuzibadili zilizopo kuwa katika mfumo wa
Kanzidata za Kielektroniki ili ziweze kuunganishwa na Mfumo Unganishi wa
Kutunza Kumbukumbu za Ardhi. Hatua hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa za upimaji ardhi na
kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Hadi mwezi Februari 2014, kumbukumbu
za ramani 5,000 za Jiji la Dar es Salaam zimebadilishwa na kuwekwa katika
ramani unganishi. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaandaa Kanzidata ya
viwanja 300,000 katika Miji mbalimbali Nchini.
66.
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu Sekta ya Ardhi
imekumbwa na tatizo la migogoro ya mara kwa mara inayotokana na matumizi
mbalimbali ya ardhi hususan baina ya wakulima na wafugaji. Aidha, migogoro hiyo
imekuwa ikihusisha wananchi na maeneo ya hifadhi, Vijiji kuwepo ndani ya maeneo
ya hifadhi, wananchi dhidi ya wawekezaji na
baina ya wananchi wenyewe kwa wenyewe. Migogoro hii
imekuwa ikiongezeka zaidi katika siku za hivi karibuni kutokana na kuongezeka
kwa idadi ya watu, mifugo na shughuli za kiuchumi zinazotegemea ardhi kama vile
madini, utalii, viwanda, kilimo na makazi. Migogoro ya ardhi ina athari kubwa
kwa wananchi ikiwemo uvunjifu wa amani, uharibifu wa mali na hata vifo.
Serikali imekuwa ikichukua hatua kudhibiti migogoro hiyo kila inapotokea. Ili kupata suluhisho la kudumu la
kushughulikia migogoro ya ardhi, Serikali imeanza kusimika mifumo ya kisasa kwa
ajili ya upimaji, umilikishaji na usimamizi wa sekta ya ardhi. Hii ni kwa
sababu uzoefu umeonesha kwamba ukosefu wa ramani, mipaka rasmi na miliki
kamilifu ndicho chanzo kikuu cha migogoro inayojitokeza mara kwa mara. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itatoa
kipaumbele katika Sekta ya Ardhi hasa kushughulikia maeneo yanayolenga kutatua
migogoro ya ardhi kama vile upimaji wa mipaka ya vijiji, kutoa hati miliki na
kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya Vijiji. Aidha, Serikali itajenga
Mfumo Unganishi wa Kutunza Kumbukumbu za Ardhi, kukamilisha usimikaji wa alama
za msingi za upimaji, kurasimisha hati milki na kupima mipaka ya Kimataifa.
Nishati
67.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha
huduma za upatikanaji wa umeme Nchini kwa kutekeleza miradi mbalimbali ili
kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata umeme. Mwaka 2013/2014, Serikali
imekamilisha kwa Asilimia 90 Awamu ya Kwanza ya Mradi Kabambe wa Usambazaji wa
Umeme unaotekelezwa katika Mikoa 16 Nchini. Pia, Mradi huo unajumuisha
usambazaji wa umeme Vijijini ambapo wateja 15,305 kati ya wateja 22,000
waliolengwa wameunganishiwa umeme. Vilevile, Wakala wa Nishati Vijijini
imesaini Mikataba 35 na Wakandarasi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya
usambazaji wa umeme Vijijini kupitia Mradi Kabambe wa Usambazaji wa Umeme
Vijijini. Aidha, tarehe 8 Septemba 2013, Mheshimiwa Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua mtambo
wa kufua umeme wa Megawati 60 unaotumia mafuta mazito katika eneo la Nyakato,
Mwanza. Mtambo huo umeongeza uwezo wa kufua umeme kwenye gridi ya Taifa na
kufikia Megawati 1,583. Mtambo huo umeimarisha upatikanaji wa umeme katika
Mikoa ya Mwanza, Geita na Mara. Kutokana na juhudi za kusambaza umeme Mijini na
Vijijini hadi mwezi Machi 2014, zaidi ya Asilimia 30 ya Watanzania wamepatiwa
huduma hiyo, na hivyo kuvuka lengo la Asilimia 30 lililotarajiwa kufikiwa mwaka
2015.
68.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kukua kwa
kasi kwa Sekta ya gesi, Serikali katika mwaka 2013/2014, imeandaa Sera ya Gesi
Asilia ambayo inatoa miongozo ya kusimamia rasilimali hiyo. Serikali pia
inatekeleza miradi mbalimbali chini ya sekta ndogo ya gesi ikiwa ni pamoja na
kuendelea na Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Gesi Asilia kutoka Mtwara
na Lindi hadi Dar es Salaam. Hadi sasa, mabomba yote kwa ajili ya kutekeleza
mradi huo wenye urefu wa Kilomita 542 yamewasili na kazi ya kuunganisha
inaendelea. Ujenzi wa Bomba la Kusafirishia Gesi pamoja na mitambo miwili ya
kuchakata gesi hiyo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2014. Aidha,
Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Kinyerezi utakaozalisha Megawati 150
kwa kutumia Gesi Asilia
umeanza kutekelezwa. Katika hatua nyingine, Serikali imepitia upya
miundo ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania na Shirika la Umeme Tanzania
kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi wa utendaji wa Mashirika hayo.
69.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2014/2015, Serikali itakamilisha mchakato wa Maboresho ya sera mbalimbali za
Nishati ikiwemo Sera ya Nishati ya Mwaka 2003; Sera Mpya ya Mafuta na Sera Mpya
ya Uwezeshaji Wazawa. Kukamilika kwa sera hizo kutaimarisha usimamizi wa Sekta
ya Nishati kwa maendeleo ya Nchi yetu.
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
70.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imekamilisha Awamu ya Kwanza na ya Pili ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
wenye urefu wa kilomita 7,560 ambao
pia unatoa maunganisho ya mawasiliano kwa Nchi jirani. Awamu ya Tatu ya ujenzi
itakayoziunganisha Unguja na Pemba na Mkongo wa Taifa imeanza mwezi Desemba,
2013 na inatarajiwa kukamilika katika miezi 18. Mkongo umesaidia watoa huduma
kufikisha huduma za mawasiliano kwa Wananchi
kwa uharaka zaidi, uhakika na kwa gharama nafuu. Hatua hiyo
inaharakisha maendeleo ya
Taifa kwa Wananchi kupata fursa
ya kutumia TEHAMA katika kupambana na umaskini na kujiletea maendeleo kwa kasi
zaidi. Pia, Serikali kwa kutumia ruzuku
imeendelea kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo yasiyokuwa na mvuto wa
kibiashara kwa kushirikiana na Sekta binafsi. Katika mwaka 2013/2014 jumla ya
Kata 52 zenye Vijiji 316 vimefikishiwa huduma za mawasiliano kupitia Mpango
huo. Aidha, Serikali imetia saini makubaliano na watoa huduma za mawasiliano
kufikisha huduma hizo katika Kata
nyingine163 zenye Vijiji 922. Watu 1,211,841 watanufaika na juhudi hizo. Katika mwaka
2014/2015, Serikali
itaendelea na ujenzi wa Mkongo maeneo ya mijini katika Miji ya Morogoro,
Arusha, Mwanza na Dodoma na
kuendelea kuunganisha
Unguja na Pemba na Mkongo huo.
Simu za Mkononi na Intaneti
71.
Mheshimiwa Spika, mazingira mazuri yaliyowekwa na
Serikali kwenye Sekta ya Mawasiliano yameonesha matokeo chanya na ya kuridhisha
sana. Idadi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano Nchini imeongezeka kutoka laini za simu za mkononi Milioni 2.96
mwaka 2005 hadi Milioni 27.45 mwaka 2013. Watumaji wa mfumo wa intaneti nao
wameongezeka kutoka Milioni 3.56 mwaka 2008 hadi Milioni 9.3 mwaka 2013. Pia,
kuna ongezeko kubwa la huduma
kupitia mawasiliano ya simu za
mkononi. Huduma hizo ni pamoja na miamala ya kifedha na ununuzi wa huduma na
bidhaa kwa kutumia
miamala ya kibenki. Hivi sasa wananchi wanaweza kufanya
malipo ya huduma mbalimbali wanazozitumia kupitia simu za kiganjani. Hatua hiyo imesaidia kuokoa muda na
kupunguza msongamano sehemu za kulipia na kupata huduma hizo.
Mfumo wa Kuhakiki na Kusimamia Huduma za Mawasiliano
72. Mheshimiwa Spika,
Serikali ililiahidi Bunge lako Tukufu kwamba ingesimika Mfumo wa
Kusimamia Mawasiliano ya Simu
Nchini. Lengo la kujenga Mfumo
huo ni kubaini takwimu zinazopita katika mitandao ya mawasiliano. Mfumo huo
unaweza kutoa takwimu za mawasiliano
yanayofanyika ndani na nje ya
Nchi; kutambua mapato na miamala ya fedha; kufuatilia na kugundua mawasiliano
ya ulaghai; na kutambua taarifa za laini ya
simu na za kifaa cha mawasiliano. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, tayari Mtambo wa kuwezesha Mfumo wa
Kusimamia Mawasiliano Tanzania umejengwa kwa gharama ya Dola za Marekani
Milioni 25 kwa kutumia utaratibu wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (Build, Operate and Transfer). Ili
kuweza kutumia Mfumo huo ipasavyo, Serikali imekamilisha Kanuni za Uhakiki na
Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na simu zinazoingia Nchini kutoka nje ya Nchi. Mfumo huo umeanza rasmi kutumika mwezi Oktoba, 2013 na kwa kipindi cha miezi mitatu ya Oktoba hadi
Desemba, 2013 umeingizia Serikali
Shilingi Bilioni 5. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea
kuboresha taarifa za kiutendaji zitakazowezesha kupunguza kasi ya udanganyifu
wa simu zinazoingia nchini kwa lengo la kuongeza mapato. Vilevile, Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania itasimamia miamala ya malipo ya fedha kupitia simu za
mkononi yanayofanywa na kampuni za simu.
Mfumo wa Utangazaji wa Digiti
73.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba, Serikali
ilianza kutekeleza awamu ya kwanza ya zoezi la kuhama kutoka mfumo wa
utangazaji wa Analojia kwenda Digiti tarehe 31 Desemba, 2012. Awamu hiyo ilihusisha Miji Saba ya Dar es
Salaam, Mbeya, Tanga, Mwanza, Arusha, Dodoma na Moshi. Uhamaji huo ulifanyika
kwa mafanikio makubwa na tathmini ilifanywa ili kuweka mazingira bora zaidi ya
kuendelea na zoezi hilo. Kufuatia tathmini hiyo, Awamu ya Pili ilianza
kutekelezwa kuanzia tarehe 31 Machi, 2014 na inatarajiwa kukamilika tarehe 30
Septemba, 2014. Miji kumi itakayohusika na zoezi hilo ni Singida na Tabora,
ikifuatiwa na Miji ya Musoma, Bukoba, Kigoma, Kahama, Iringa, Songea, Morogoro
na Lindi. Uzimaji wa mitambo ya utangazaji ya Analojia unahusisha maeneo yote
yanayopata huduma za matangazo kupitia mitambo ya kusimikwa ardhini tu, ambayo
ni Asilimia 24 ya eneo lote la Nchi
yetu. Maeneo yanayopata huduma za
matangazo kupitia mitambo ya Satellite
na Cable hayahusiki
na zoezi hilo.
Serikali imelenga ifikapo mwezi Oktoba, 2014 mitambo yote ya Analojia iwe
imezimwa Nchini. Napenda kurudia wito wangu kwamba, zoezi hili ni la muhimu na
lina lengo la kuifanya Nchi yetu iendane na mabadiliko yanayotokea duniani
ambayo hayakwepeki. Wadau wote watoe
ushirikiano kwa vyombo vinavyohusika.
Barabara na Madaraja
74.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2013/2014, Serikali imekamilisha ujenzi wa kilometa 505.7 za
Barabara Kuu na kukarabati kilometa 146.6. Aidha, imejenga kwa kiwango cha lami
kilometa 22.3 za Barabara za Mikoa na kukarabati kilometa 145.1 kwa kiwango cha
changarawe. Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi
wa madaraja ya Kigamboni – Dar es Salaam na Mto Malagarasi - Kigoma. Katika mwaka 2014/2015,
Serikali itajenga Barabara mpya zenye urefu wa kilometa 633 za Barabara kuu na
Barabara za Mikoa kwa kiwango cha lami. Vilevile, itakarabati kilometa 165 za
barabara za lami na kilometa 1,150 za barabara za changarawe katika Barabara
Kuu na Barabara za Mikoa. Aidha, itaendelea na ujenzi wa madaraja 57 ya barabara hizo.
Msongamano wa Magari Jijini Dar es Salaam
75.
Mheshimiwa Spika, msongamano wa magari katika Jiji la Dar es
Salaam umekuwa kikwazo katika utekelezaji wa shughuli za kila siku za kiuchumi
na kijamii. Katika kukabiliana
na tatizo hilo, mwaka 2013/2014, Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara za
lami za Ubungo Bus Terminal - Kigogo - Kawawa yenye urefu wa kilometa 6.4;
barabara ya Jet Corner –Vituka - Davis Corner yenye urefu wa kilometa 10.3 na barabara ya Ubungo Maziwa - Mabibo External yenye urefu wa kilometa 2.25 pamoja na daraja la External. Ujenzi
wa barabara ya Mzunguko wa Kigogo - Jangwani
yenye kilometa 2.72 na zile zitakazotumika kwa Mabasi yaendayo haraka unaendelea.
76.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itajenga barabara sita Jijini Dar es
Salaam kwa kiwango cha lami. Barabara hizo ni Tabata Dampo - Kigogo (km 1.6);
Kifuru - Kinyerezi (km 4); Goba - Mbezi Mwisho (km 7); Tangi bovu (Samaki) -
Goba (km 9); Kimara Baruti - Msewe (km 2.6) na Kimara - daraja la Maji Chumvi
External (km 3). Tayari Serikali imesaini mikataba na wakandarasi kwa ajili ya
ujenzi wa barabara hizo ambazo zinatarajiwa kukamilika kati ya miezi 8 hadi 18.
HALI YA UCHUKUZI
Reli ya Kati na TAZARA
77.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imefanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa ujenzi wa reli ya Arusha –
Musoma yenye urefu wa Kilomita 600. Lengo ni kuimarisha usafiri na usafirishaji
wa mizigo kwa Mikoa ya Kaskazini na Nchi jirani ya Uganda kupitia Bandari ya
Tanga. Vilevile, Serikali imekamilisha usanifu wa kina wa mradi wa ujenzi wa
reli kwa
kiwango cha kimataifa yenye urefu wa Kilometa 1,464
kutoka Dar es Salaam - Isaka - Keza - Kigali na Kilometa 197 kutoka Keza hadi Msongati.
78.
Mheshimiwa Spika, Mkataba wa Maelewano kati ya Tanzania na Burundi kwa ajili ya ujenzi wa
Reli ya Uvinza hadi Msongati umesainiwa. Kuhusu Reli ya TAZARA, Serikali
inatekeleza Makubaliano ya Itifaki ya 15 iliyosainiwa mwezi Machi, 2012 kati ya
Serikali ya Watu wa China na Serikali za Tanzania na Zambia ambapo ununuzi wa
vichwa vinne vya treni, vichwa vinne vya Sogeza umefanyika pamoja na ununuzi wa
mabehewa 18 ya abiria ya Reli ya TAZARA. Katika mwaka 2014/2015, Serikali
itaboresha Kilometa 308 za miundombinu ya Reli ya Kati na vituo vya Bandari
kavu vya kuhifadhi Makasha vya Ilala na Isaka. Aidha, Kampuni ya Reli (TRL) itakarabati vichwa
nane vya treni na kununua vichwa vipya 12 na mabehewa 204 ya mizigo na kukarabati majengo ya Stesheni.
Bandari
79.
Mheshimiwa Spika, kijiografia nchi yetu imejaliwa kuwa na eneo
kubwa la maziwa na bahari ambalo limetuwezesha kuwa na bandari zinazohudumia
pia Nchi jirani zisizopakana na bahari. Ili kutumia fursa hii kikamilifu, Serikali katika mwaka 2013/2014, imekamilisha upembuzi yakinifu kwa ajili ya
kuboresha Gati namba 1 hadi 7 katika Bandari ya Dar es Salaam. Vilevile,
inatekeleza miradi ya ujenzi wa magati kwenye Bandari za Ziwa Victoria,
Tanganyika na Nyasa. Aidha, kupitia Mfumo wa
Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa, Mamlaka ya Bandari
imevuka malengo kwa kuhudumia zaidi ya tani Milioni 13 za mizigo hadi Desemba
2013, ikilinganishwa na tani Milioni 12 kwa mwaka 2012. Vilevile, Serikali
imeanza kutekeleza utaratibu wa kufanya kazi
bandarini kwa saa 24 kwa siku zote za juma ili kuongeza kasi ya uondoshaji wa
mizigo inayotoka. Hatua hiyo
imesaidia kupunguza msongamano
wa mizigo katika Bandari ya Dar
es Salaam na kupunguza malalamiko kutoka
kwa watumiaji wa
bandari hiyo. Aidha, kumekuwa na
ongezeko la ufanisi katika kuhudumia wasafirishaji wa mizigo katika maeneo ya
mipakani, hususan Rusumo, Tunduma, Namanga, Kasumulo na Mtukula. Wasafirishaji
wanatumia muda mfupi hivi sasa ikilinganishwa na hapo awali. Kwa mfano, muda wa
huduma katika mpaka wa Rusumo, umepungua kutoka siku tatu hadi nusu saa.
80.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali
itaanza kuboresha Gati namba 1 hadi 7 ili kuwezesha Bandari ya Dar
es Salaam kuhudumia mizigo tani Milioni 18 kutoka tani Milioni 13.5 za sasa.
Aidha, itakamilisha ujenzi wa magati katika Bandari ya Mtwara, kukamilisha majadiliano
na kuanza ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na kuendelea na miradi ya ujenzi wa
magati kwenye Bandari za Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa. Vilevile, itakarabati meli za MV Umoja, MV Victoria, MV Butiama, MV
Serengeti, MV Liemba, MT Sangara, MT Ukerewe na meli ya MV Songea ili kuboresha
usafiri na usafirishaji katika maziwa.
Usafiri wa Anga
81.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeboresha
miundombinu ya viwanja vya ndege Nchini na kuviwezesha kutoa huduma kwa
kuzingatia Sheria na Kanuni za uendeshaji za kimataifa. Katika mwaka 2013/2014,
jumla ya viwanja vya ndege 13 ikiwemo
Viwanja vya Mwanza, Musoma, Bukoba, Kigoma, Tabora, Arusha, Tanga,
Lindi, Mtwara, Iringa, Songea, Nachingwea na Kilwa Masoko vilifanyiwa ukaguzi
na kupata leseni ya uendeshaji. Aidha, Serikali imeanza mradi wa ujenzi wa jengo jipya la tatu la abiria katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere utakaogharimu Shilingi
Bilioni 518. Mradi huo ambao umewekwa jiwe
la msingi na Mheshimiwa Dkt Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 24 Aprili, 2014
unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2015. Jengo hilo litakuwa na ukubwa
wa meta za mraba 70,000 ambao ni zaidi
ya mara nne ya ukubwa wa jengo lililopo sasa lenye ukubwa wa meta za mraba
15,000. Baada ya kukamilika kwa jengo hilo na miundombinu yake, Uwanja huo
utakuwa na uwezo wa kuegesha ndege kubwa za abiria. Aidha, utahudumia abiria
milioni sita kwa mwaka ikilinganishwa na abiria milioni 2.5 kwa sasa. Vilevile, Uwanja huo utatoa fursa
mbalimbali za kiuchumi, kibiashara na kukuza utalii nchini. Aidha, utazalisha
ajira mpya zaidi ya 7,000 kwa Watanzania.
82.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa
kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga ili kuimarisha huduma za usafiri
nchini pamoja na kuvutia uwekezaji na utalii. Kwa kuzingatia azma hiyo, mwezi
Oktoba 2013, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete alizindua rasmi Uwanja wa Ndege wa Mafia baada ya ujenzi wake kukamilika kwa kiwango
cha lami. Kuzinduliwa kwa uwanja huo
kumefungua fursa za kibiashara,
hususan ya utalii katika kisiwa hicho. Vilevile, mwezi Julai 2013, Mheshimiwa
Rais, aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege kwa
kiwango cha lami katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba. Katika
mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea na ujenzi wa jengo jipya la abiria katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kukamilisha ujenzi wa Uwanja
mpya wa Kimataifa wa Ndege wa Songwe, Mbeya. Serikali pia itakamilisha
ukarabati wa Viwanja vya ndege vya Mwanza, Bukoba, Kigoma na Tabora na kuanza
kukarabati viwanja vya ndege vya Shinyanga, Mtwara na Sumbawanga.
MAENDELEO YA SEKTA YA ELIMU
Elimu ya Msingi
83.
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa
utoaji wa elimu unafuata Sera, Miongozo na Mitaala, Serikali imeendelea kupitia
Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995. Aidha, kupitia
Mfumo wa
Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa katika elimu ya msingi, utaratibu wa kupima stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (K3) kwa
wanafunzi wa darasa la Kwanza na la Pili umeanzishwa kwa lengo la kupima na
kuweka msingi wa kuboresha stadi husika kabla ya kuingia darasa
linalofuata. Katika mwaka huu wa fedha,
Serikali imeajiri jumla ya walimu 17,928 wa
shule za msingi na kupangiwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kuajiriwa kwa walimu hao kutapunguza pengo la
walimu lililopo.
84.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2014/2015, Serikali kupitia Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa,
itaimarisha elimu ya msingi kwa kuongeza uwazi wa kiutendaji, kuwajengea walimu uwezo wa kutoa msaada wa kimasomo kwa
wanafunzi wenye uhitaji maalum, kuinua ubora wa mazingira ya kufundishia na
kujifunzia, kuongeza upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na
kuongeza uwajibikaji wa watendaji katika utoaji wa elimu.
Elimu ya Sekondari
85.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2013/2014, Serikali imeweka juhudi kubwa katika kuimarisha Elimu ya Sekondari
hasa ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, maabara, ununuzi wa madawati na
vitabu pamoja na kuboresha miundombinu na mazingira ya kujifunzia na
kufundishia. Aidha, Serikali imeajiri Walimu wapya wa Sekondari 18,410 na kutoa
mafunzo kazini kwa Walimu 12,476. Kati ya hao, Walimu 8,400 ni wa masomo ya
Sayansi na Hisabati. Hatua hizo zimechangia kuongeza ufaulu wa Wanafunzi
waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2013 kufikia Asilimia 58.25
ikilinganishwa na Asilimia 43.08 mwaka 2012. Katika mwaka 2014/2015, Serikali
itatoa kipaumbele cha uwekezaji kwenye miundombinu ya Shule za Sekondari,
Walimu, Ukaguzi na Vitendea kazi.
Mafunzo ya Ufundi Stadi
86.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Ufundi na
Mafunzo ya Ufundi Stadi wa mwaka 2013/2014 hadi 2017/2018. Mpango huo unalenga
kuongeza udahili katika ngazi mbalimbali za Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili
kujenga uwiano wa nguvukazi katika ngazi mbalimbali kwa kila fani. Vilevile,
unalenga kujenga nguvukazi yenye kuhimili ushindani wa soko la ajira kwa kuinua
ubora wa elimu na mafunzo ya ufundi ili kukidhi
mahitaji ya soko la ndani na nje ya Nchi. Ili kutekeleza mpango huo,
katika mwaka 2013/2014, Serikali ilianza kutumia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi
25 kutoa mafunzo ya masomo ya ufundi stadi ili kuongeza udahili wa wanafunzi. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaanza ujenzi wa vyuo
vya ufundi stadi katika Mikoa ya Rukwa, Geita, Simiyu na Njombe.
Elimu ya Juu
87.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeboresha mazingira ya kujifunzia
na kufundishia masomo ya sayansi na teknolojia kwenye Vyuo Vikuu nchini. Katika mwaka 2013/2014, kupitia Mradi wa
Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Serikali imekamilisha ujenzi wa vyumba 48
vya Mihadhara, Maabara 93 za sayansi na
Ofisi 302 za wafanyakazi katika Vyuo Vikuu mbalimbali vya Umma nchini.
Aidha, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na vya TEHAMA vilinunuliwa katika
Vyuo hivyo na kuziunganisha Taasisi 28 za elimu ya juu katika Mkongo wa Taifa
wa Mawasiliano.
88.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kuwepo
kwa malalamiko mengi kuhusu Vyuo Vikuu nchini kutoza ada tofauti kwa mafunzo ya
aina moja, Serikali imekamilisha Mwongozo wa Gharama
Halisi ya Kumsomesha Mwanafunzi wa Elimu ya Juu. Mwongozo huo unatoa ukomo wa ada
inayotakiwa kutozwa na chuo kwa kila programu au kozi kwa mwanafunzi. Lengo ni kuondoa upangaji na upandishaji wa ada
kiholela kwa wanafunzi wanaosoma elimu ya juu pasipo kuzingatia gharama halisi ya
kumsomesha mwanafunzi husika kulingana na kozi anayosoma. Katika mwaka 2014/2015, Serikali
itasimamia utekelezaji wa Mwongozo huo.
MAENDELEO YA SEKTA YA AFYA
Huduma ya mama na mtoto
89.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea
kuimarisha huduma ya afya ya Mama na Mtoto kwa kutekeleza Mpango Mkakati wa
Kuongeza Kasi ya Kupunguza Vifo vitokanavyo na Matatizo ya Uzazi na Vifo vya
Watoto wa mwaka 2008 hadi 2015. Katika kutekeleza Mkakati huo, Serikali
imeandaa Mpango Kazi wa Uzazi wa Mpango
Uliothaminiwa. Mpango Kazi huo unalenga kununua na kusambaza dawa na
vifaa vya uzazi wa mpango nchini. Aidha, Serikali imeimarisha mfumo wa rufaa
kwa mama wajawazito kwa kununua vyombo vya usafiri
kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii na kuvisambaza katika mikoa yenye kiwango
cha juu cha vifo vya mama vitokanavyo na matatizo ya uzazi. Vilevile, Serikali
inatekeleza
Mpango Mkakati wa Kutokomeza Maambukizi Mapya ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa
mtoto ambao ulizinduliwa tarehe Mosi, Desemba, 2012 na Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Awamu ya kwanza ya
Mpango huo ilianza mwezi Oktoba, 2013
na kuhusisha Mikoa tisa yenye uambukizo mkubwa wa VVU kwa wajawazito. Mikoa
hiyo ni Iringa, Njombe, Mbeya, Tabora, Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Geita na Kagera. Awamu ya pili imeanza mwezi
Januari, 2014 kwa Mikoa 16 iliyobakia.
90. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2014/2015, Serikali itakamilisha mapitio ya Mpango Mkakati wa Kuongeza Kasi ya
Kupunguza Vifo vya Mama vitokanavyo na Uzazi na Vifo vya Watoto na kutekeleza
afua nyingine za kipaumbele. Aidha, kupitia Mpango wa Kitaifa wa Uzazi wa
Mpango dawa na vifaa vyote vya uzazi wa mpango vitanunuliwa na kusambazwa ili
viweze kuwafikia wananchi wanaovihitaji. Lengo ni kufikia Asilimia 60 ya
kiwango cha utumiaji huduma za uzazi wa mpango kama ilivyoanishwa kwenye
Malengo ya Maendeleo ya Milenia.
Udhibiti wa Maambukizi ya Malaria
91.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa
malaria, Serikali
imeendelea kugawa vyandarua shuleni na kuhimiza matumizi endelevu. Katika mwaka
2013/2014, Serikali iligawa vyandarua 510,000 katika shule 2,302 za msingi na
Sekondari za Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kupitia Programu ya Wanafunzi
Shuleni. Aidha, kupitia mikakati na afua nyingine Serikali ilisambaza vyandarua
879,856 vyenye viuatilifu vya
muda mrefu kupitia Mpango wa Hati Punguzo kwa wajawazito na watoto wenye
umri chini ya mwaka mmoja.
92.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa
kushirikiana na Serikali ya Cuba, inatekeleza Mpango wa kuangamiza Viluwiluwi
vya Mbu kwa kutumia njia za Kibaiolojia katika Jiji la Dar es Salaam. Mpango
huo pia, utatekelezwa katika Mikoa mingine mitano. Aidha, Serikali kwa kushirikiana
na wadau iliendelea na zoezi la kupulizia dawa ya ukoko katika kaya 838,000
zilizopo kwenye Mikoa ya Kagera, Mara na Mwanza ambapo zaidi ya Wananchi
4,505,752 wamekingwa dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa malaria. Pia, Serikali
imekamilisha kusambaza kipimo cha
malaria kinachotoa majibu ya
haraka katika vituo
vyote vya kutolea
huduma Nchini. Vilevile, jumla ya dozi 14,655,000 za Dawa
Mseto na Vitendanishi 9,853,710 vimenunuliwa na kusambazwa katika vituo vya
huduma na hivyo kuimarisha upatikanaji wa dawa na vitendanishi Nchini.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015,
Serikali itaendelea kugawa vyandarua Milioni 7.2 vyenye viuatilifu vya muda
mrefu kupitia Mpango wa Hati Punguzo, na kuendeleza kampeni maalum ya kugawa
vyandarua kwa jamii katika ngazi ya kaya. Aidha, zoezi la kugawa vyandarua kwa
wanafunzi shuleni litaendelezwa kwa Mikoa ya Kusini. Sambamba na hatua hizo,
mradi wa kuangamiza viluwiluwi vya mbu katika mazalia utapelekwa katika Mikoa
mingine mitano kwa kutumia viuatilifu (Biolarvicides) vitakazozalishwa katika
kiwanda kinachojengwa Kibaha, Mkoa wa Pwani ambacho kinatarajiwa kuanza kazi
mwaka huu wa 2014.
Huduma kwa Wazee na Watu Wenye Ulemavu
93.
Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya
Wazee ya mwaka 2003 na Sera ya Taifa ya Huduma na Maendeleo kwa Watu Wenye
Ulemavu ya mwaka 2004 zinasisitiza kuwa makundi hayo yana haki ya kupata
matunzo katika jamii. Katika mwaka
2013/2014, Serikali ilitoa huduma za msingi kwa wazee na watu wenye ulemavu
wasiojiweza wanaotunzwa na kulelewa katika Makazi 17 ya Serikali. Jumla ya
wahudumiwa 1,235 walipatiwa huduma za msingi ikiwemo chakula, malazi, mavazi
pamoja na kuwapatia vifaa yakiwemo magodoro, mashuka, vitanda na nyenzo za
kujimudu. Vilevile, Serikali iliratibu
huduma za matunzo katika Makazi 24 yanayoendeshwa na Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali ili kupunguza malalamiko kuhusu upungufu wa huduma zinazotolewa.
94. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kusisitiza kuwa,
wazee na watu wenye ulemavu na wasiojiweza wanahitaji kupatiwa matunzo katika
jamii zao. Huduma zinazotolewa kwenye
vituo na taasisi za Serikali na zisizo za Serikali ni hatua ya mwisho pale
ambapo itathibitika kuwa mzee au mlemavu huyo hana mtu kabisa wa kumtunza katika
familia na jamii. Natoa rai kwa wananchi kuendeleza utamaduni wa kuwatunza
wazee wetu na watu wenye ulemavu. Huu ni
utamaduni mzuri sana. Aidha, nazikumbusha Halmashauri kutenga fedha za
kuyahudumia makundi hayo. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itazindua Baraza na
Mfuko wa Taifa wa Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ili kuwajengea na kuongeza
uwezo wao katika kuzifikia fursa za maendeleo na kuimarisha utawala bora.
Lishe
95.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2013/2014, Serikali imeendelea kusimamia Kanuni za Uongezaji wa Virutubishi
katika vyakula ambapo viwanda vikubwa sita vya kusindika unga wa ngano na
viwanda vitatu vya kusindika mafuta ya kula vinaweka virutubishi katika vyakula
vinavyotengenezwa. Takwimu zinaonesha kuwa, takribani watu milioni 10 wanatumia
unga wa ngano uliorutubishwa na Milioni 4 wanatumia mafuta ya kupikia
yaliyorutubishwa na vitamin A. Vilevile, Serikali imeandaa Mpango wa Uongezaji
wa Virutubishi kwenye vyakula Ngazi ya jamii ambapo utekelezaji wake ulishaanza
katika Mikoa ya Iringa, Njombe, Arusha na Dar es Salaam. Mpango huo unalenga
uwekaji virutubishi kwenye unga wa mahindi unaozalishwa na wajasiriamali wadogo
na kusagwa kwenye viwanda vya kati na vidogo.
96.
Mheshimiwa Spika, Sekta binafsi
inashirikishwa kikamilifu katika mapambano dhidi ya utapiamlo nchini. Mwezi Mei
2013, Serikali ilikabidhi tani nane za Madini joto kwa Muungano wa Wasindikaji
wa Chumvi katika maeneo mbalimbali Nchini kama sehemu ya mchango wa Serikali wa
kuimarisha Sekta Binafsi katika mapambano dhidi ya utapiamlo. Serikali pia
imeimarisha Maabara za uwekaji madini joto katika chumvi kwa kununua na kugawa
vitendanishi katika Maabara 13 za Mikoa. Lengo ni kupanua wigo wa Wananchi
wanaopata vyakula vyenye virutubishi. Natoa wito kwa Viongozi katika ngazi
zote. Kusimamia juhudi hizo za Serikali na kuhakikisha zinaendelezwa katika
maeneo yao. Aidha, ninawasihi Wafanyabiashara wote wenye viwanda vya chakula
kutekeleza jukumu hilo kikamilifu. Kwa wale ambao hawajakamilisha taratibu za
ufungaji wa mashine za kuongeza virutubishi wafanye hivyo mapema iwezekanavyo.
HALI YA UPATIKANAJI WA MAJI NCHINI
Huduma ya Maji Vijijini
97.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inatekeleza Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 inayolenga kuboresha huduma ya
maji Mijini na Vijijini kwa kushirikisha Wananchi na Sekta Binafsi. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali iliweka
lengo la kutoa huduma za maji kwa Asilimia 65 Vijijini katika umbali usiozidi
mita 400. Ili kuongeza kasi ya kufikia lengo hilo, katika mwaka 2013/2014,
Serikali iliongeza bajeti ya maji kwa Shilingi Bilioni 184 kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maji.
98.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mradi
wa Maji kwa Vijiji Kumi kwa kila Halmashauri upo katika hatua mbalimbali za
utekelezaji ambapo ujenzi na ukarabati wa miradi ya maji 248 katika Vijiji 270
umekamilika. Pia, jumla ya vituo 10,393
vya kuchotea maji vinavyohudumia Watu 2,598,250 vimejengwa. Ujenzi wa
miundombinu ya maji kwenye Vijiji 613 upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji
na miradi katika Vijiji 374 inafanyiwa tathmini ya zabuni. Aidha, katika
kipindi hicho, vyombo vya watumia maji 373 vimeundwa. Vilevile, katika kipindi cha miezi sita ya utekelezaji wa miradi ya maji chini ya
BRN! kinachoishia Desemba 2013, Wanavijiji 2,390,000 wamefikishiwa huduma za
maji safi na salama, ikilinganishwa na Wanavijiji 300,000 hadi 500,000
waliokuwa wakipatiwa huduma za maji safi Vijijini kabla ya mpango huo kuanza.
99.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia
inatekeleza Awamu ya Pili ya mradi wa maji wa Chalinze ambao utatoa huduma ya
maji kwa Vijiji 47 vyenye Watu 197,684 katika Wilaya za Bagamoyo, Pwani. Hadi
kufikia Desemba 2013, utekelezaji wa mradi ulikuwa umefikia Asilimia 88.
Vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi wa mabwawa katika maeneo mbalimbali
hususan maeneo kame kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma ya maji kwa matumizi
ya nyumbani na mifugo. Ujenzi wa mabwawa ya Iguluba (Iringa Vijijini) na Wegero
(Butiama, Mara) na ukarabati wa Bwawa la Ingodini –Longido Arusha umekamilika.
Ujenzi wa mabwawa ya Kawa (Nkasi, Rukwa), Sasajila (Chamwino, Dodoma), Mwanjoro
(Meatu, Shinyanga) na Kidete (Kilosa, Morogoro) umekamilika kwa zaidi Asilimia
75. Mabwawa yaliyokamilika kwa wastani wa Asilimia 50 ni Habiya (Itilima,
Simiyu), Sekeididi (Kishapu, Shinyanga) na Matwiga (Chunya, Mbeya). Natoa wito
kwa Wananchi kulinda vyanzo na miundombinu ya maji. Vilevile, natoa wito kwa
Viongozi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia vyema Vyombo vya watumia
maji ili miradi hii iwe endelevu.
Huduma ya Maji Mijini
100.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka za Majisafi
na Usafi wa Mazingira katika miji mikuu ya mikoa zinatoa huduma ya maji kwa
wakazi wake kwa wastani wa Asilimia 80. Katika Jiji la Dar es Salaam,
upatikanaji wa huduma ya maji utaongezeka zaidi mara baada ya upanuzi na ujenzi
wa bomba kuu la maji kutoka Ruvu Juu na Ruvu Chini kukamilika. Kazi ya kulaza
bomba la maji kutoka mtambo wa Ruvu Chini hadi Dar es Salaam lenye urefu wa
kilometa 55.5 umekamilika kwa Asilimia 60.5 na kazi ya kupanua mtambo wa Ruvu Juu
na kulaza bomba hadi Dar es Salaam imeanza mwezi Februari, 2014. Katika mwaka
2014/2015, Serikali itaanza kutekeleza Mpango Maalum wa Kuhifadhi na Kutunza
Vyanzo vya Maji wa Miaka Mitano (2014/2015 – 2018/2019) ili kuimarisha
ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za uhifadhi, utunzaji na ulinzi wa
rasilimali za maji. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza Mradi wa Maji kwa
Vijiji Kumi kwa kila Halmashauri.
UTAMADUNI NA MICHEZO
Utamaduni
101. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeendelea na urasimishaji wa tasnia za
filamu na bidhaa zake kwa kushirikiana
na taasisi zinazohusika ili kuiongezea Serikali mapato na kulinda kazi za
wasanii. Moja ya hatua zilizochukuliwa ni
kufanyika kwa operesheni ya kufuatilia matumizi ya stempu za kodi za
Mamlaka ya Mapato Tanzania ambapo zaidi ya
stempu milioni moja za bidhaa za filamu zimetolewa. Jumla ya operesheni nane za kufuatilia filamu zilizoingia
sokoni kinyume na taratibu zimefanyika na jumla ya filamu 301 zilibainika
kuingia sokoni kinyume na taratibu na wahusika kuchukuliwa hatua. Natoa wito
kwa mamlaka husika kuhakikisha kuwa zoezi hili linafanyika Nchi nzima na
linakuwa endelevu. Vilevile, natoa rai kwa wananchi kununua bidhaa za filamu zenye viwango zinazothibitishwa
na uwepo wa stika maalumu.
Michezo
102. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa maendeleo ya
michezo imetekeleza Mradi wa Kimataifa wa Kukuza Ari ya Michezo wenye lengo la kuimarisha ushiriki wa vijana na
watoto katika michezo bila kujali jinsia ama uwezo. Kutokana na juhudi hizo,
katika mashindano ya Kombe la Dunia kwa Watoto wa Mitaani yaliyofanyika Nchini
Brazil mwezi Aprili 2014, Timu yetu ya Watoto wa Mitaani ya Mkoani Mwanza
imetwaa Kombe la Dunia la Watoto wa Mitaani. Napenda kuwapongeza Vijana hao kwa
kuiletea Nchi yetu heshima kubwa. Vijana hao wanapaswa kuendelezwa ili waweze
kutuwakilisha vyema katika mashindano mengine ya Kimataifa. Aidha, mafanikio
hayo yawe chachu ya kuendeleza michezo
mingine Nchini. Ni muhimu tukakumbuka kwamba vipaji vya michezo viko vingi na
vimejificha. Kinachotakiwa ni kufanyika jitihada za dhati kuviibua na
kuvitumia. Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ishirikiane kwa
karibu na Maafisa Utamaduni wa Halmashauri zote nchini kubuni mkakati maalum wa
kuibua vipaji vya michezo kuanzia ngazi ya kitongoji.
USHIRIKIANO
WA KIMATAIFA NA KIKANDA
103.
Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imeendelea kufanya
vyema katika medani za Kimataifa kufuatia kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutunukiwa
Tuzo tarehe 9 Aprili, 2014 kwa kuwa Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa Zaidi katika
Maendeleo Barani Afrika kwa mwaka 2013, huko Jijini Washington, Marekani. Tuzo
hiyo ya heshima kubwa inayotolewa kwa Viongozi wa Afrika ambao hutoa mchango
mkubwa zaidi wa kiuchumi na kijamii kila mwaka kwa watu wao, hutolewa na jarida
maarufu la kimataifa la African Leadership Magazine Group. Tuzo hiyo imetolewa
kutokana na mwelekeo wake thabiti na wenye mafanikio makubwa kwa masuala ya
utawala bora.
Vilevile, napenda kumpongeza Dkt. Stergomena Lawrence Tax kwa
kushinda kinyang’anyiro cha nafasi ya Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Nchi za
Kusini mwa Afrika (SADC) mwezi Agosti, 2013. Namtakia kila la kheri katika
kutekeleza majukumu yake na kuendelea kupeperusha vyema bendera ya Nchi yetu.
104.
Mheshimiwa Spika, tarehe 1 hadi 2 Julai, 2013 Watanzania walipokea ugeni mkubwa wa Kiongozi
wa Taifa la Marekani, Rais Barack Obama aliyeambatana na mamia ya
Wafanyabiashara. Kupitia ziara hiyo, Marekani ilizindua
Mpango wa Umeme
Afrika (Power Africa), ambao utaongeza kwa mara mbili upatikanaji wa umeme katika Bara la
Afrika. Tanzania ni miongoni mwa Nchi zitakazonufaika na Mpango huo unaolenga
kuzalisha zaidi ya Megawati 8,000 za umeme katika Nchi za Afrika Kusini mwa
Jangwa la Sahara. Serikali ya Marekani imeahidi kutoa zaidi ya Dola za Marekani
Bilioni 7. Kampuni za Marekani, Ulaya,
Asia na Afrika ziliahidi kutoa zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 9 kwa ajili ya
Mradi huo kwa miaka mitano ijayo. Nchi yetu pia kupitia ziara hiyo ilipata
fursa ya kujitangaza na kujiweka katika nafasi nzuri ya kukuza Uchumi,
Biashara, Utalii na Uwekezaji.
105. Mheshimiwa Spika, utekelezaji mzuri wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia ambayo yatafikia
ukomo wake mwaka 2015 umeifanya Nchi
yetu izidi kung’ara Kimataifa na hivyo kuwa kati ya Nchi 30 zitakazounda
kikundi kazi kitakachoandaa Malengo ya Maendeleo Endelevu
yatakayotekelezwa baada ya
mwaka 2015. Aidha,
katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi (WEF) uliofanyika mjini Davos, Uswisi
mwezi Februari 2014, Mpango wa WEF wa kuvutia uwekezaji katika miundombinu
muhimu ulijadiliwa ambapo Bandari ya Dar es Salaam ilichaguliwa kuwa miongoni
mwa Bandari zitakazonufaika na Mpango huo. Tayari Timu ya Wataalam imefika
Nchini kufanya tathmini ya awali ya mradi huo. Aidha, Kongamano maalum
lililohusisha Nchi kadhaa zinazohusika na Mpango wa Uchukuzi wa Ukanda wa Kati
lilifanyika tarehe 15 Aprili, 2014. Kongamano hilo lilizinduliwa na Mheshimiwa
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MASUALA MTAMBUKA
Vita Dhidi ya Rushwa
106. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeendelea na mapambano dhidi ya rushwa
kwa kutoa elimu kuhusu rushwa, athari zake na wajibu wa wananchi katika
mapambano dhidi ya rushwa kupitia semina, midahalo, maonesho ya kitaifa,
vipindi vya Radio na Televisheni pamoja na machapisho. Aidha, tuhuma 3,872
zikiwemo tuhuma mpya 679 zilichunguzwa, ambapo hadi sasa uchunguzi wa tuhuma
589 umekamilika. Majalada 4 ya tuhuma za rushwa kubwa yalifikishwa kwa
Mkurugenzi wa Mashtaka kwa hatua za
kisheria. Katika mwaka 2014/15, TAKUKURU itaendelea kuchunguza tuhuma 3,193
zilizopo na mpya zitakazojitokeza na kuendesha kesi 635 zilizopo Mahakamani
hivi sasa na zitakazoendelea kufunguliwa. Vilevile, itaendelea na uchunguzi wa tuhuma zitokanazo na taarifa
za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali za mwaka 2011/2012.
Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi
107. Mheshimiwa Spika, Serikali imetekeleza Awamu ya Kwanza ya Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za
Serikali kwa Uwazi. Lengo ni kuendesha shughuli zake kwa uwazi zaidi ili kuimarisha
utoaji wa huduma kwa Wananchi, kusikiliza Wananchi, kupambana na rushwa na
kujenga dhana ya kuaminika kwa Wananchi. Katika mwaka 2013/2014 Serikali imechapisha, Bajeti yake kwa lugha rahisi za
Kiswahili na Kingereza na kuiweka katika Tovuti ya Wizara ya Fedha ili iweze
kusomwa na Wananchi wote. Aidha, imeanzisha Tovuti ya Serikali (Government
Portal) yenye anuani ya http://www.egov.go.tz/ na Kituo Maalum cha
Mawasiliano kwa masuala ya OGP Nchini pamoja na kuimarisha Tovuti ya Ofisi ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaanza kutekeleza Awamu
ya Pili ya Mpango huo kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kutunga Sheria ya Uhuru wa Habari; kukamilisha na kuimarisha Mfumo wa Kuweka
Wazi Taarifa na Takwimu kwenye Tovuti.
Maafa
108. Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imeendelea
kukumbwa na Maafa ambayo yameleta athari kwa Wananchi na mali zao. Katika mwaka
2013/2014, ukame umesababisha upungufu wa Chakula kwa Watu 828,063 katika
Wilaya 54 za Mikoa 14 Nchini. Serikali ilitoa tani 26,663 za chakula cha msaada
chenye thamani ya Shilingi Bilioni 15.2 pamoja na Shilingi Bilioni 2.2 kwa
ajili ya kukisafirisha hadi kwa walengwa. Mafuriko makubwa pia yametokea katika
maeneo mengi hususan, Mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Pwani, Mbeya, Tanga,
Kilimanjaro, Lindi, Dodoma, Iringa, Kagera na Mara na kusababisha vifo,
majeruhi na uharibifu wa mali na miundombinu. Katika kukabiliana na athari
zilizojitokeza, Serikali na wadau mbalimbali
imetoa misaada ya dharura ya kibinadamu kwa waathirika na imechukua
hatua za kurejesha miundombinu ya maji, elimu, afya, barabara na madaraja na
umeme. Nitumie fursa hii kulipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania, TANROADS,
Wakandarasi, Wadau mbalimbali pamoja na
Wananchi wote kwa kazi kubwa waliyoifanya na misaada waliyoitoa kwa Waathirika wa
Maafa yaliyojitokeza. Napenda kurudia wito
wangu kwa Wananchi
wote wanaoishi katika maeneo
hatarishi hasa mabondeni, kutii maagizo ya Serikali kuondoka katika maeneo hayo na kuhamia maeneo yaliyoainishwa ambayo
ni salama kwa maisha yao.
Aidha, ninatoa wito kwa Wananchi wote kufuata Sheria ili kuepuka uvunjifu
wa amani na kusababisha maafa kutokana na mapigano, hasa ya kugombea ardhi na
malisho.
Mafunzo ya Kukabili Maafa
109. Mheshimiwa Spika, mafunzo ya kuijengea jamiii uwezo wa kukabiliana na maafa ikiwemo kupokea
na kugawa misaada wakati wa maafa yametolewa katika ngazi za Mkoa na Wilaya kwa
Mikoa ya Mara, Geita, Singida, Simiyu, Shinyanga, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma,
Tabora na Arusha. Pia, Mipango ya Kujiandaa Kukabili Maafa katika Halmashauri za Wilaya za Maswa,
Bariadi, Meatu, Mwanga na Same imeandaliwa. Katika mwaka 2014/2015, Serikali
itafanya Tathmini ya Maafa yanayoweza kutokea na uwezo wa kuyakabili pamoja na
mipango ya kujiandaa na kukabiliana na maafa katika Halmashauri za Wilaya za
Mtwara Mjini, Mtwara Vijijini, Masasi, Mvomero na Kilosa. Vilevile, itaanza
Ujenzi wa Kituo cha Dharura cha Utendaji na Mawasiliano (Emergency Operation
and Communication Centre) katika eneo la
Mabwepande Wilayani Kinondoni.
Udhibiti wa Dawa za Kulevya
110. Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa
na Serikali dhidi ya uingizaji na utumiaji wa Dawa za Kulevya, tatizo hili
limeendelea kuwa kubwa kutokana na wanaojihusisha na Dawa hizo kubuni mbinu
mpya za kukwepa mkono wa Sheria. Katika
mwaka 2013/2014, Serikali
imeendeleza mapambano dhidi ya dawa hizo kwa kuelimisha Umma kuhusu madhara ya dawa hizo. Serikali pia
imepanua huduma za matibabu kwa
watumiaji wa dawa za kulevya kwa kutumia dawa ya Methadone. Huduma za tiba hiyo
zinapatikana katika kliniki zilizopo katika Hospitali ya Muhimbili,
Mwananyamala na Temeke. Vilevile, imeendesha operesheni zilizowezesha kilo 12,820
za mirungi kukamatwa, ekari 127 za mashamba ya bangi, na kilo 3,445 za mbegu za
bangi na magunia 1,107 ya bangi kavu kuteketezwa. Pia, kilo 236.5 za Heroin na kilo tatu za Cocaine zilikamatwa.
111. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali
itaendelea kutoa elimu kwa umma na huduma za matibabu kwa watumiaji wa Dawa za
Kulevya. Serikali pia itaendelea kuwachukulia hatua kali wahalifu
wote wanaojihusisha na biashara haramu ya Dawa za Kulevya. Vilevile, ili kuondoa mianya inayojitokeza katika
kupambana na uhalifu utokanao na biashara ya Dawa za Kulevya, Serikali itakamilisha kutunga Sheria mpya ya Kuzuia na
Kupambana na
Dawa za Kulevya itakayowezesha kuimarisha mapambano dhidi ya
tatizo hilo.
Mazingira
112. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Serikali imeandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira
wa mwaka 2013 hadi 2018, utakaoziwezesha sekta zote kujumuisha masuala ya
mazingira kwenye majukumu yao na mipango yao ya maendeleo. Sambamba na hatua
hiyo, Serikali iliratibu utekelezaji wa miradi ya kuhimili
mabadiliko ya tabianchi. Moja ya miradi hiyo ni Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya
Tabianchi (African Adaptation Programme)
wenye thamani ya Dola za Marekani
Milioni 2.5 unaofadhiliwa
na Serikali ya
Japan.
Fedha hizo zimetumika kuanzisha miradi ya majaribio ya kuhimili mabadiliko
ya tabianchi katika Wilaya za Misenyi (Kagera), Mbinga (Ruvuma), Igunga
(Tabora) na Zanzibar. Mradi mwingine ni Mradi wa Vijiji vya Mfano vya Mazingira (Eco-Village) wenye thamani ya Euro
Milioni 2.2 unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya chini ya utaratibu ujulikanao
kama Climate Change Alliance Initiative. Hadi sasa mradi umeainisha Vijiji vya
mfano na kutekeleza miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika Mikoa ya
Morogoro, Kigoma, Dodoma na Pemba. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kutoa elimu ya hifadhi ya mazingira kwa umma kuhusu Sera, Sheria na
Mikataba ya Kimataifa ya kuhusu Mazingira pamoja na kuendelea kuhamasisha kampeni ya
upandaji miti Nchi nzima.
Udhibiti wa UKIMWI
113. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka
2013/2014, Serikali
imeanza kutekeleza Mkakati wa
Tatu wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI wa
mwaka 2013 hadi 2018. Mkakati huo una shabaha ya kufikia Malengo ya Kimataifa
ya Sifuri Tatu, ikimaanisha Kutokuwa na
Maambukizi Mapya, Kutokuwa na Vifo
Vitokanavyo na UKIMWI na Kuondokana
kabisa na Unyanyapaa na Ubaguzi. Hadi Desemba 2013, kati ya watu 1,261,931 walioandikishwa kuwa wanaishi na
VVU, watu 669,730 walianzishiwa dawa. Aidha, ili
kurahisisha upimaji wa VVU, Serikali imeipatia Mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Katavi
na Rukwa mashine kubwa za kupima kiwango cha kinga (CD4). Serikali pia
imeidhinisha kuanzishwa kwa Mfuko wa UKIMWI, utakaojulikana kama AIDS Trust
Fund. Kuanzishwa kwa Mfuko huo kutawezesha kupunguza utegemezi wa Wahisani
kwenye shughuli za UKIMWI kwa wastani wa Asilimia 40.
114. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kuimarisha kampeni za
uraghibishaji zinazolenga mabadiliko ya tabia ili kuachana na mila na desturi
hatarishi. Vilevile, Serikali imepanga
kuimarisha kampeni za kinga
kwa vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 24 dhidi
ya maambukizi ya VVU kwa kutoa elimu.
Juhudi zaidi zitaelekezwa kwenye mikoa 10 yenye maambukizo zaidi ya
wastani wa Kitaifa
wa Asilimia 5.1. Mikoa hiyo ni
Njombe (14.8), Iringa (9.1), Mbeya (9.0), Shinyanga (7.4), Ruvuma (7.0), Dar es Salaam (6.9). Rukwa
(6.2), Katavi (5.9), Pwani (5.9) na Tabora (5.1). Aidha, Serikali itakamilisha maandalizi ya Sheria ya Mfuko wa UKIMWI.
Mamlaka
ya Ustawishaji Makao Makuu
115. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali
imeendeleza miundombinu muhimu
katika Manispaa ya Dodoma. Ujenzi wa Barabara zenye urefu wa kilomita
47.55 kwa kiwango cha lami katika maeneo ya Kisasa, Chang’ombe, Kikuyu, Area A pamoja na
eneo la Uwekezaji la Njedengwa umekamilika.
Aidha, ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa kilomita 6.4
katika eneo la Nkuhungu na Mwangaza umekamilika. Serikali pia imefungua
barabara zenye urefu wa kilomita 105 kwenye maeneo yaliyopimwa ya Miganga,
Iyumbu na Ndachi. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itajenga mitaro ya maji ya
mvua katika maeneo ya Ilazo, Kisasa na Ipagala na kupima viwanja vipya 1,850.
Pia ,Serikali itaandaa mpango wa matumizi ya ardhi katika maeneo ya Mkonze
Mashariki, C-centre, Nkuhungu na maeneo yanayozunguka Chuo Kikuu cha Dodoma.
HITIMISHO
116.
Mheshimiwa Spika, kwa muhtasari nimeelezea
baadhi ya shughuli ambazo zimetekelezwa na Serikali katika mwaka 2013/2014.
Aidha, nimetoa Mwelekeo wa Kazi zitakazotekelezwa katika mwaka 2014/2015. Kwa
kuhitimisha, napenda kusisitiza mambo yafuatayo:
a.
Uchumi wetu unakua kwa
kasi nzuri, kwa mfano katika mwaka 2011 ulikua kwa asilimia 6.4, mwaka 2012
ulikua kwa asilimia 6.9 na mwaka 2013 kwa asilimia 7.0. Ukuaji huu ni mkubwa
ikilinganishwa na Nchi nyingine za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo
Wastani wa ukuaji wa uchumi kwa nchi hizo ulikuwa asilimia 4.6 mwaka 2011,
asilimia 3.5 mwaka 2012 na asilimia 4.5 mwaka 2013. Takwimu zinaonesha pia
kwamba kiwango cha ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni cha juu ikilinganishwa na
wastani wa ukuaji wa uchumi kwa Nchi za Afrika Mashariki. Kwa mfano, uchumi wa
Kenya ulikua kwa asilimia 4.4 mwaka 2011, asilimia 4.6 mwaka 2012 na asilimia
5.0 mwaka 2013. Uchumi wa Uganda ulikua kwa asilimia 6.6 mwaka 2011, asilimia
4.6 mwaka 2012 na asilimia 6.3 mwaka 2013. Takwimu hizo zinadhihirisha kwamba
uchumi wetu unaendelea kuimarika ikilinganishwa na nchi nyingine, jambo
tunalopaswa kujivunia. Mabadiliko makubwa yanayoonekana Nchini katika sekta za
mawasiliano, ujenzi, viwanda na biashara ni matokeo ya ukuaji huu wa uchumi.
Tunahitaji kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kuhakikisha kwamba ukuaji huu
unakuwa endelevu na kuelekeza juhudi zaidi katika sekta nyingine hususan
kilimo, ufugaji na uvuvi kwani ndizo zinazotegemewa na Watanzania wengi.
b.
Tumeadhimisha Miaka 50
ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa amani na utulivu. Muungano huu ni wa
kipekee na wa kupigiwa mfano duniani kote. Aidha, ni kielelezo kamili cha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa
wananchi jambo lililowezesha kuwepo kwa amani na usalama Nchini. Muungano
umetuletea maendeleo makubwa katika miaka 50 ya uhai wake. Ni wajibu wetu
kuendelea kuenzi, kulinda na kudumisha Muungano huu kwa nguvu zetu zote.
c.
Tumeingia katika kipindi
muhimu katika historia ya Nchi yetu ambapo Bunge Maalum la Katiba limeanza
mjadala wa kutunga Katiba Mpya. Ni matumaini yangu kuwa Bunge Maalum
litakamilisha kazi ya kuandaa Rasimu ya Tatu itakayopelekwa kwa Wananchi kwa ajili
ya kupigiwa kura ya maoni. Ninawasihi Wananchi wawe watulivu katika kipindi
hiki maalum na kufuatilia kwa makini mjadala wa Katiba kwa kupima mawazo
yanayotolewa wakati wa mjadala ili hatimaye kupiga kura ya maoni vyema. Ni
matarajio yangu kuwa Katiba Mpya itakayopatikana itatusaidia kuleta mabadiliko
makubwa kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa kupata muafaka wa kitaifa wa
uendeshaji wa Nchi yetu katika miaka mingi ijayo.
d.
Sote tumeshuhudia juhudi
za Serikali katika kuimarisha upatikanaji na usambazaji wa nishati Nchini.
Mradi wa Ujenzi wa Mitambo ya Kusafisha Gesi Asilia na Bomba la kusafirishia
gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam unaoendele kujengwa utasaidia sana
kuongeza umeme wa gharama nafuu kwenye Gridi ya Taifa. Natoa wito kwa wananchi
wote kushirikiana na Serikali kufanikisha miradi hiyo kwa kulinda miundombinu
yake pamoja na kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na uwepo wa miradi hiyo.
117. Mheshimiwa Spika, kabla ya kumaliza Hotuba yangu, nimwombe Mheshimiwa Hawa Abdulrahman
Ghasia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa atoe maelezo ya Mapitio ya Kazi zilizofanyika mwaka 2013/2014 na
Mwelekeo wa Kazi za Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa kwa mwaka 2014/2015.
SHUKRANI
118.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii sasa
kuwashukuru Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa ushirikiano walionipa katika kipindi
hiki. Aidha, nawashukuru Watumishi wote wa Serikali na Taasisi zake chini ya
Uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi
Ombeni Yohana Sefue kwa kusimamia Shughuli za Serikali vizuri.
Nawashukuru Watanzania wote na Washirika wetu wa Maendeleo kwa michango yao
ambayo imewezesha Serikali kutoa huduma mbalimbali kwa Wananchi.
119. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Mheshimiwa Dkt. Mary
Michael Nagu, Mbunge wa Hanang na
Waziri wa Nchi (Uwekezaji na Uwezeshaji); Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi,
Mbunge wa Ismani na Waziri wa Nchi (Sera, Uratibu na Bunge); Mheshimiwa Hawa
Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini na Waziri wa Nchi, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa; Mheshimiwa
Aggrey Joshua Mwanri, Mbunge wa Siha, Naibu Waziri, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; na Mheshimiwa Majaliwa
Kassim Majaliwa, Mbunge wa Ruangwa, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu)
kwa ushirikiano walionipa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nawashukuru pia
Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa kusimamia shughuli za Serikali vyema
katika Mikoa na Wilaya.
120.
Mheshimiwa Spika, ninawashukuru vilevile Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya
Uongozi wa Makatibu Wakuu, Dkt. Florens M. Turuka na Bwana Jumanne A. Sagini,
kwa kazi nzuri wanayoifanya. Ninawashukuru Naibu Makatibu Wakuu, Bibi Regina L.
Kikuli, Bwana Kagyabukama E. Kiliba,
Bwana Zuberi M. Samataba, Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Dkt. Deo M. Mtasiwa, Naibu Katibu
Mkuu (Afya) kwa ushauri wao wa kitaalam ambao wamenipa mimi na Waheshimiwa
Mawaziri wa Nchi katika kipindi hiki. Ninawashukuru kwa kukamilisha maandalizi
yote ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka
2013/2014.
121.
Mheshimiwa Spika, ninapenda kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri
na maelekezo anayonipatia katika kutekeleza majukumu yangu. Pia, ninamshukuru
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi kwa ushirikiano wao mkubwa. Vilevile, ninawashukuru
Waheshimiwa Wabunge wote, Viongozi wote wa Kitaifa na wa ngazi nyingine zote
kwa ushirikiano wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Ninawashukuru sana
Wapiga Kura wangu wa Jimbo la Katavi kwa ushirikiano wanaonipa katika kuleta
maendeleo ya Jimbo letu.
122. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee, naomba uniruhusu kutumia fursa hii kumshukuru sana Mama
Tunu Pinda na Familia yangu yote kwa kuniombea, kunitia moyo na kunivumilia kwa
kila hali katika utekelezaji wa majukumu yangu ya Kitaifa. Ninawashukuru sana!!
MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU, OFISI YA WAZIRI MKUU - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA NA OFISI YA BUNGE YA MWAKA 2014/2015
123. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2014/2015, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi
zake inaliomba Bunge lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja na Tano, Milioni Mia Tano
Ishirini na Saba na Ishirini na Nne Elfu (105,527,024,000).
Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Themanini, Milioni Mia Saba Sitini na Tano na Ishirini
na Tisa Elfu (80,765,029,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Ishirini na Nne, Milioni Mia Saba Sitini na Moja,
Mia Tisa Tisini na Tano Elfu (24,761,995,000) ni za Miradi ya Maendeleo.
124.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu
- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Taasisi zake inaombewa jumla ya
Shilingi Bilioni Mia Nne Sabini na Tisa,
Milioni Mia Mbili Ishirini na Nne na Sitini na Mbili Elfu (479,224,062,000).
Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia
Mbili Sabini na Tatu, Milioni Sitini na Tano, Mia Nane Tisini na Tano Elfu
(273,065,895,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Mia Mbili na Sita, Milioni Mia Moja
Hamsini na Nane, Mia Moja Sitini na Saba Elfu (206,158,167,000) ni za
Miradi ya Maendeleo.
125. Mheshimiwa Spika, Ofisi za Wakuu wa Mikoa zinaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Mbili Sitini na Saba, Milioni
Mia Tisa na Tisa, Mia Tatu Tisini Elfu (267,909,390,000). Kati ya fedha
hizo, Shilingi Bilioni Mia Mbili na
Mbili, Milioni Mia Tatu na Kumi, Mia Mbili Themanini na Sita Elfu
(202,310,286,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Sitini na Tano, Milioni Mia Tano na
Tisa, Mia Moja na Nne Elfu (65,509,104,000) ni za Miradi ya Maendeleo. Halmashauri zote zinaombewa jumla ya Shilingi Trilioni Nne, Bilioni Mia Mbili Thelathini
na Moja, Milioni Mia Nne Arobaini na Mbili, Mia Tisa Sabini na Nne Elfu
(4,231,442,974,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Trilioni
Tatu na Bilioni Tisini, Milioni Mia Tatu Sabini, Mia Tatu na Nane Elfu
(3,090,370,308,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Mia Sita Themanini na Mbili, Milioni Mia Sita na
Mbili na Arobaini na Nne Elfu (682,602,044,000) ni za Miradi ya
Maendeleo. Aidha, jumla ya Shilingi Bilioni
Mia Nne Hamsini na Nane, Milioni Mia Nne Sabini, Mia Sita Ishirini na Mbili
Elfu (458,470,622,000) ni mapato ya ndani ya Halmashauri zote.
126. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano inaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Thelathini na Mbili, Milioni Mia Sita
Tisini na Sita, Mia Nane Tisini na Nne Elfu (132,696,894,000) kwa ajili ya
Mfuko wa
Bunge ambapo Shilingi Bilioni
Mia Moja Ishirini na Tatu, Milioni Mia Tisa Arobaini na Moja, Mia Nne Hamsini
na Tano Elfu (123,941,455,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi
Bilioni Nane, Milioni Mia Saba Hamsini na Tano, Mia Nne Thelathini na Tisa Elfu
(8,755,439,000) ni za Miradi ya Maendeleo.
EmoticonEmoticon