Swanepoel alisema kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka riba iliyotolewa kama gawio ilipanda hadi asilimia 11 ikiwa ni matokeo mazuri ya viwango vilivyopokelewa katika mfuko wa fedha uliowekwa katika benki mbalimbali za biashara nchini Tanzania.
“Riba hii ni malipo kwa wateja binafsi, mawakala wa reja reja, mawakala wakubwa na wabia wengine wa kibiashara wa Tigo ambao kila mmoja anapokea malipo kulingana na thamani ya fedha zilizohofadhiwa katika pochi ya kielektroniki ya Tigo Pesa,” Swanepoel alifafanua.
Swanepoel aliongeza, “Tunayo furaha sana kuwatangazia ongezeko hili la gawio la riba kwa mara ya 11 mfululizo, hali inayoleta nafuu kwa mamilioni ya watumiaji wa Tigo Pesa kwa kuwasaidia kukabiliana na majukumu mbalimbali ya kifedha. Hii inaonesha jinsi tulivyojikita katika kutoa huduma ya fedha inayowafikia wateja wetu na nchi kwa ujumla kupitia huduma yetu ya Tigo Pesa.”
Alibainisha kuongezeka kwa faida kuwa ni kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya soko na kasi ya kuongezeka kwa idadi ya watumiaji wa Tigo Pesa kama kichocheo kikubwa katika ongezeko kubwa la gawio la riba hususani kwa upande wa wafanya biashara. Tigo Pesa hivi sasa ina mtandao mkubwa wa wafanya biashara zaidi ya 55,000 wanaowezesha malipo ya miamala nchini kote.
Kama ilivyokuwa awali kwa mujibu wa Swanepoel malipo kwa wateja yanakokotolewa kwa kuzingatia wastani wa salio la kila siku linalokuwa katika pochi ya kielektroniki ya simu na kwamba mgawanyo wa gawio hili la faida ni kulingana na waraka wa Benki Kuu uliotolewa Februari 2014.
Tigo Pesa inakuwa ni huduma ya kwanza ya fedha kwa njia ya simu duniani ambayo mwaka 2014 iligawa gawio la hisa lililozalishwa kutoka katika akaunti ya dhamana ya pesa katika simu katika mfumo wa gawio wa robo mwaka kwa wateja wake.
EmoticonEmoticon