Mpina awataka wakulima wa pamba Kisesa kuhifadhi chakula

 Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina akizungumza na baadhi ya  wananchi wa kijiji cha  Mwagayi katika kata ya Itinje Mkoani Simiyu wilayani Meatu, Jimboni Kisesa leo kuhusu ongezeko la bei ya pamba ambapo kwa sasa inanunuliwa kwa kiasi cha shilingi 1,200 kwa kilo.
Naibu Waziri Ofisi ya makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina, akiongena na Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mwagayi kuhusu Ongezeko la bei ya pamba leo wananchi hao walimsimamisha Naibu Waziri Mpina alipokuwa katika ziara yake ya kikazi jimboni Kisesa.

Na Evelyn Mkokoi - Meatu
NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina amewataka wananchi wa Jimbo la Kisesa wilayani Meatu mkoani Simiyu kutumia vizuri fedha wanazopata kwa kuuza pamba kununua chakula cha kutosha na kukihifadhi ili kuondokana na uhaba wa chakula.
Akizungumza Leo na wananchi wa Kijiji cha Mwagayi Kata ya Itinje  Wilaya ya Meatu, Mpina alisema uamuzi uliofanywa na Rais Dk John Pombe Magufuli kusimamia ongezeko la bei ya pamba umelenga kuboresha maisha ya wananchi wanyonge waliodhulumiwa kwa miaka mingi hivyo ni muhimu wakulima hao kutumia vizuri ongezeko hilo la bei kuboresha maisha yao ikiwa ni pamoja na kununua ziada ya chakula.
Mpina alisema Rais Magufuli amesimamia na kuweka msimamo usioyumba katika suala la pamba ambapo kwa sasa bei ya pamba imefikia shilingi 1200 kwa kilo tofauti na hapo awali ambapo wakulima walikuwa wakidhulumiwa kwa kulipwa shilingi 600 kwa kilo na kusababisha wananchi kuishi maisha duni na kushindwa kunufaika na zao hilo.
“Rais Magufuli ameweka msimamo kwamba pamba isinunuliwe chini ya shilingi 1000 na kwamba kampuni itakayoshindwa kununua kwa bei hiyo izuiliwe kununua pamba na kufutiwa usajili wa kutonunua tena zao hilo sehemu yoyote nchini”alisema Mpina.
Pia Mpina ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisesa  (CCM) aliwataka wananchi hao kutumia mabadiliko hayo ya bei ya pamba kama fursa ya kuboresha maisha badala ya kutumia vibaya fedha hizo kwa mambo ya anasa ikiwemo kuongeza idadi ya wake.

Alisema Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli imedhamiria kwa dhati kuboresha maisha ya wananchi wanyonge na ndio sababu ya kuwekwa msimamo huo kuhusu bei ya pamba kwani kwa miaka kumekuwa hakuna msimamo wa Serikali kuhusu zao hilo na hivyo kusababisha wanunuzi wa pamba kujipangia bei wenyewe na kuwakandamiza wakulima.
Kuhusu maendeleo ya jimbo hilo, Mpina alisema juhudi zinaendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na kumaliza kero ya maji ambapo kila kata ya jimbo hilo itapata visima vinne vya maji ambavyo vitamaliza kero kubwa ya maji kutokana na maeneo mengi ya jimbo hilo kuwa na ukame hasa nyakati za msimu wa kuangazi.
Aidha Mpiana alisema kauli mbiu yake ya ‘Sitapumzika hadi maendeleo ya kweli yapatikane jimbo la Kisesa’ haijabadilika na kuwahakikishia kuwa hajawahi kuchoka,kuogopa wala kushindwa kazi yoyote na kuwasihi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya awamu ya tano ili iendelee kuleta mabadiliko ambayo wananchi wameanza kuonja matunda ya utawala wa Rais Magufuli.

Powered by Blogger.